GAVANA wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndullu, amekiri kupotea kwa
fedha kwenye mikono ya watu na kueleza hali hiyo imesababishwa na fedha
kuhama kutoka katika mikono haramu.
Asema hali hiyo imechagizwa na uamuzi wa Serikali kubana shughuli za
watu ‘misheni town’ na badala yake fedha zimekwenda kwenye matumizi
halali na sahihi kwa umma.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari, ambapo alisema pamoja na hali hiyo hakuna
mdodoro wa uchumi.
Profesa Ndullu alifananisha kipindi cha sasa na kile kilichoitwa
‘ukata’ enzi za utawala wa Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, wakati
anapambana na rushwa na kusema kwamba alifanikiwa kuinua uchumi.
Alisema Serikali imechukua hatua kubwa ya kuongeza mapato kwa
kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi.
“Serikali katika matumizi yake imebana shughuli za wale waliokuwa wa
‘misheni town’ na sasa shughuli hizi zinafanyika kwa uwazi na kwa
uhalali.
“Kiuchumi hakuna fedha iliyopotea bali fedha zimehama na kwenda kwa
wale wanaofanya shughuli za kuhudumia umma kiuhalali na tunaita
‘redistribution’ (mabadiliko ya mgawanyo).
“Ila wapo watakaolalamika kwamba fedha zimepotea. Wale ambao walikuwa
wanapata fedha kwa shughuli ambazo Serikali imezibana hatuwezi kusema
fedha haijapotea. Ni kweli kwa wao fedha imepotea, lakini kitaifa fedha
haijapotea.
“Katika kutambua fedha haijapotea tunaangalia fedha zinazotolewa na
BoT, ambapo katika kila Sh 100 inayotolewa Sh 36 huwa zinaenda mikononi
mwa mabenki na taasisi za fedha, wakati Sh 64 zinakuwa mikononi mwa watu
na nje ya mfumo, hakuna mabadiliko makubwa katika hilo,” alisema.
Profesa Ndullu alisema kinachoelezwa kwamba ni kupungua kwa fedha
zinazopelekwa benki, kumetokana na Serikali kuhami sha uwekaji wa
fedha za mashirika yake kutoka katika benki binafsi na kwenda BoT.
Alisema sababu za kufanya hivyo ni kuweka wazi mapato na matumizi ya mashirika ya Serikali.
Hata hivyo alisema si kwamba fedha hizo hazirudi kwenye benki za biashara kwani hufanya malipo kwa mashirika kupitia benki hizo.
“Wakati wa matumizi huwa tunatumia benki hizo si kwamba tunalipa moja kwa moja kwenye mashirika yetu,” alisema.
KUPOROMOKA UCHUMI
Akizungumzia kuhusu dhana ya kuporomoka kwa uchumi alisema kwa
kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu uchumi umekua kwa asilimia 5.5.
“Kiuchumi ukuaji huo tunaufananisha na wa mwaka jana kipindi kama
hicho ambapo kwa mwaka jana ulikua kwa asilimia 5.7 hivyo kuna
mabadiliko kidogo,” alisema Prof. Ndulu.
Alisema wapo watu waliotafsiri tofauti hiyo kuwa itaathiri ukuaji wa uchumi kwa mwaka suala am- balo si sahihi.
“Robo ya kwanza ya mwaka jana ukuaji ulikua asilimia 5.6 lakini
ukuaji wa mwaka ukawa asilimia 6.9. Tunatarajia ukuaji wa mwaka huu
utakuwa asilimia 7.2 kutokana na viashiria ambavyo tunaviona,” alisema.
VIASHIRIA
Alitaja viashiria hivyo kuwa ni ukuaji wa uzalishaji wa umeme kwa
asilimia 14.5 katika kipindi cha nusu mwaka (Januari-Juni 2016) ambapo
uzalishaji umefikia kWh trilioni 3.4 kutoka kWh trilioni 3.0.
Kiashiria kingine ni kuongezeka kwa uzalishaji na matumizi ya saruji
kwa asilimia 7 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu. “Pia
kuna ongezeko la mali ghafi za viwandani kutoka nje kwa asilimia 19
na hii inaonyesha kuwa ukuaji wa viwanda unaenda kwa kasi.
Aliongeza viashiria vingine ni kuongezeka kwa mauzo ya nje ya
bidhaa za viwandani kwa asilimia 15.6, kuongezeka kwa makusanyo ya kodi
na kuongezeka kwa mikopo inayotolewa na mabenki ya biashara kwa Sh
trilioni 1.1 kip- indi cha nusu mwaka.
MIRADI MIKUBWA
Profesa Ndullu alisema uwepo wa miradi mikubwa inayotarajiwa
kuanza mwaka huu ni kiashiria mojawapo cha ukuaji mzuri wa uchumi.
Alitaja baadhi ya miradi kuwa ni ujenzi wa reli ya kati km 200,
ujenzi wa bomba la mafuta ku- toka Uganda hadi Tanga, ujenzi wa bandari
ya Dar es Salaam, ujenzi wa kituo cha biashara Kurasini, ujenzi wa
mitambo ya kufua umeme ya Kinyelezi II, upanuzi wa viwanja vya ndege na
ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula.
Alisema miradi hiyo itatumia fedha nyingi, mali ghafi zinazozalishwa pamoja na kutumia nguvu kazi hivyo kutoa ajira nyingi.
DENI LA TAIFA
Profesa Ndullu alisema deni la Taifa, mfumuko wa bei na thamani ya
shilingi ni miongoni mwa mambo yanayoonyesha hali ya uchumi ilivyo na
Serikali inafanya vizuri katika mambo hayo.
Akizungumzia kuhusu deni la taifa alisema licha ya kuendelea kuongezeka bado ni stahimilivu likilinganishwa na pato la taifa.
“Kwa kuangalia uwiano wa mapato na deni la taifa bado ni stahimilivu
na kwa asilimia 20 ya pato la taifa na ikilinganishwa na ukomo wa
asilimia 50,” alisema Profesa Ndullu na kusisitiza: “Bado tuna nafasi
kubwa ya a kukopa bila kuathiri ustahilivu wetu.”
Alisema licha ya deni hilo kuendelea kuongezeka lakini kasi ya
kuongezeka imepungua kwa kipindi cha nusu mwaka hususani deni la nje
ambalo limeongezeka kwa asimilia 2.6 tu kufikia Juni mwak huu kutoka
Desemba mwaka jana.
Hata hivyo alisema deni la ndani limezidi kuongezeka kwa kasi zaidi
na kufikia zaidi ya Sh bil- ioni 10 hadi Juni mwaka huu kuto- ka bilioni
8 Desemba mwaka jana.
Kuhusu mfumuko wa bei alisema uko vizuri kwani kwani Agosti mwaka huu
umefikia asilimia 4.9 ikilinganishwa na asilimia 6.8 Desemba mwaka
jana.
Kwa upande wa mwenendo wa thamani ya shilingi ya Tanzania alisema imeendelea kuwa tulivu katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016.
“Mpaka sasa mfuko wa bei ni asilimia 4.9 ambao uko vizuri na
tunaendelea kuudhibiti. Tanzania ni kati ya nchi 10 za Afrika ambazo
uchumi wake unakuwa vizuri. Lakini pamoja na hali juhudi zimefanyika
kudhibiti matumizi hivyo kufanya bajeti kutekelezwa bila tatizo,”
alisema Profesa Ndulu
Gavana Ndullu alisema akiba ya fedha za kigeni ni Dola za
Marekani bilioni 4, ambazo zinaweza kuhudumia mahitaji ya bidhaa na
huduma
kutoka nje kwa miezi minne. Septemba 6, mwaka huu Kiongozi wa Chama cha
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alitoa maazimio ya kikao cha Kamati Kuu
ambapo chama hicho kilijadili hali ya uchumi nchini.
Alisema kwa kipindi ambacho Rais Magufuli amekuwa madarakani kasi ya
ukuaji wa uchumi ambayo ilikuwepo awali imepungua kwa asilimia nne
kutoka asilimia tisa hadi asilimia tano, jambo ambalo halijawahi kutokea
kwa kipindi kirefu katika historia ya Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment