Taarifa tulizozipokea kutoka kwa viongozi wa
CUF katika ngazi mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na taarifa
iliyotolewa na viongozi wa CHADEMA hivi karibuni zinaonyesha kuwa zaidi ya
wanachama na viongozi 408 wa vyama vyetu wamekamatwa na kushikiliwa na jeshi la
polisi baadhi yao wakifunguliwa mashtaka na wengine wakiachiwa bila kufikishwa
mahakamani kote nchini. Mbunge wa Tanga mjini-CUF Mhe. Mussa Mbarouk ni
miongoni wa viongozi waliokabiliana na kadhia hii. Hali hii haionyeshi muelekeo sahihi wa
kujenga umoja, mshikamano wa kitaifa, amani na utulivu, na maendeleo endelevu
ya Taifa letu.
Madhumuni ya harakati za kupigania uhuru wa
nchi yetu miaka ya 1953-1961 yalikuwa na lengo la kutuondoa watanganyika kutoka
katika utumwa, unyonyaji, unyanyasaji, ukandamizaji, ubepari na ubeberu wa
rasilimali za Taifa letu na watu wake. Jeshi la mkoloni lilikuwa likitumika
kuwadhalilisha wazee wetu. Leo hii baada ya miaka 55 ya kujitawala, tukiwa
ndani ya mfumo halali wa kisheria wa demokrasia ya vyama vingi nchini, serikali
ya CCM kwa kumtumia Rais John Magufuli inaturudisha nyuma na kufanya vitendo
vibaya zaidi kwa raia wake kuliko ilivyokuwa ikifanywa na wakoloni!
Chakusikitisha takwimu hazionyeshi wapi jeshi la polisi lilipotumia nguvu kubwa
kupambana na raia pindi wakifungua mashataka mahakamani, Serikali (Jeshi la
polisi) likashinda kesi hizo. Mauaji ya mwandishi David Mwandosya ni ushahidi
wa hili na kesi nyingine nyingi hazina hesabu ambazo zikifikishwa mahakamani haki
inaangukia kwa washtakiwa.
Serikali ya CCM chini ya Rais Magufuli
imekuwa ikitumia vibaya rasilimali za nchi kuandaa operesheni za kupambana na
vyama vya siasa vilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria. CUF Chama cha wananchi
hakikubaliani na matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi inayotumika kuminya
demokrasia nchini, kuzuia vyama vya siasa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa
sheria, kupiga marufuku mikutano ya hadhara, kuzuia kufanyika kwa vikao/semina,
makongamano ya vyama vya siasa. Suali
hili halikubaliki. Tunamtaka Rais Magufuli atambue kuwa kamwe hatoweza kuzuia
nguvu ya umma iliyo tayari kuleta mabadiliko sahihi ya kisiasa, kiuchumi,
kijamii, na kuboresha hali za maisha na kipato cha mtanzania kwa kutumia vyema
rasilimali za nchi yetu.
Tuna kila sababu ya kuunganisha nguvu zetu
kama watanzania kumzuia Rais kwa njia ya amani asiendelee kuikanyaga katiba ya
nchi aliyoapa kuilinda. Tunahitaji Taifa letu liwe salama na hatuhitaji kwa
namna yeyote ile uvunjwaji wa sheria na matumizi ya nguvu kubwa za vyombo vya
dola yanayoandaliwa kwa madhumuni ya kuwajengea hofu watanzania na umwagaji wa
damu unaopangwa kufanywa na vyombo hivyo.
Juhudi za katibu mkuu wetu Maalimu Seif sharif Hamad za kutumia njia za
kidiplomasia kudai haki ya maamuzi halali ya wazanzibar waliyoyafanya tarehe
25/10/2015 kwa kukipa ridhaa chama cha wananchi CUF kuongoza serikali ni
ushahidi tosha wa dhamira njema ya chama chetu kuhakikisha AMANI ya Taifa letu
ni suala la msingi lisilopaswa kufanyiwa mchezo.
TUNAUNGA MKONO JUHUDI ZA VIONGOZI WA DINI;
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF –Chama Cha
Wananchi) kinaunga mkono juhudi za viongozi wa dini, na asasi nyingine nchini
katika kutafuta ufumbuzi na maridhiano juu ya kuondokana na amri ya serikali
isiyozingatia katiba , sheria na kanuni za uendeshaji wa nchi yetu zinazotoa
uhuku, haki na wajibu kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila kuingilia
na vyombo vya dola. Uhuru wa wananchi kupata habari na taarifa mbalimbali zihusuzo
mwenendo wa serikali yao.
Tunawapongeza viongozi wa CHADEMA pamoja
Mgombea wa urais wa UKAWA mwaka 2015 Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa kuongoza
busara, hekima na usikivu wa wito uliotolewa na viongozi wa dini kusitisha
Operesheni UKUTA iliyopangwa na CHADEMA kufanyika jana tarehe 1/9/2016. Hakika
watanzania hawakufanya makosa kukuunga mkono na kukuchagua kwa kura nyingi.
Tunawaomba viongozi wa dini wasimamie haki,
ukweli na kuharakisha kupatikana kwa muafaka juu ya suala hili. Pamoja na
kumuombea Rais Magufuli aongozwe na busara na hekima katika utendaji wake pia
wampe ushauri sahihi wa namna ya kuliongoza Taifa letu na kuheshimu katiba na
sheria za nchi.
KUHUSU KUFUNGIWA KWA VYOMBO VYA HABARI;
RADIO5 NA MAGIC FM
Tarehe 29 Agosti, 2016 Serikali ya CCM
kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndugu Nape Nnauye alitoa tamko la Serikali
kuvifungia kwa muda usiojulikana vituo Radio 5 ya Arusha na Magic FM ya Dar es
Salaam wakati huohuo gazeti la Mseto na gazeti la Mawio yakiwa tayari kwenye
kifungo, magazeti haya yalikuwa yakiandika habari za kiuchunguzi na kufichua
mambo mengi maovu ya serikali ya CCM. Serikali ya awamu ya tano haitaki
kukosolewa, inataka kusifiwa pekee na maovu yake yafichwe. Inataka kutengeneza
hofu kwa wananchi na wamiliki wa vyombo vya habari wasiwe na uhuru wa kuripoti
taarifa sahihi zinazoihusu serikali ya CCM na mapungufu yake. Huwezi simamia
kauli ya hapa kazi tu bila ya kujenga misingi ya demokrasia ya kweli. Lazima
hizo kazi zitafanywa kwa ubabaishaji na ukiukwaji wa taratibu.
Chama cha wananchi CUF tunaamini Tasnia ya
Habari ni muhimili muhimu katika ujenzi wa demokrasia na maendeleo endelevu kwa
Taifa letu. Ukosefu wa kupashana habari/taarifa ni sawa na kuishi gizani au
kufungiwa mahabusu. Kifungu cha 18 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
yamwaka 1977 na hatimaye kufanyiwa marekebisho mwaka 2005 inampa haki mtu uhuru
wa kujieleza na kutoa mawazo, kutafuta, kupata na kueneza habari. Inampa haki
pia ya mtu kuwasiliana bila kubughudhiwa.
DHANA YA SERIKALI YA KIIMLA NA UHURU WA HABARI:
Mchambuzi
maarufu na Mwandishi wa vitabu wa
Marekani Bluce Coville alishawahi kusema
“Namna yoyote ile ya uratibu wa
kuzuia taarifa kuwafikia umma kwa
maslahi ya Serikali ni mbinu za utawala wa kiimla” Hoja hii inaungwa mkono na wataalamu wa siasa
za kiimla. Utawala wa nchi wanaweza kuwa hawajajitangaza kama wao ni madikteta
tena wakajiita ni serikali ya kidemokrasia na kujali haki za binadamu lakini
matendo yake yote ni ya kiimla. Serikali yoyote ya kiimla watawala ndio wenye
sauti kuliko wananchi na kiongozi mkuu anafanya kilambinu wananchi wasiweze
kuhoji. Na ili umnyime mwananchi uwezo wa kuhoji ni kuzuia upatikanaji wa
taarifa isipokuwa zile zilizoandaliwa makhsusi. Na ndio mana leo serikali ya
CCM imeliweka Bunge la Jamhuri ya Muungano gizani na kuendesha Operesheni za
vitisho.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha
Wananchi) kinatambua umuhimu na nguvu ya habari na wanahabari katika kuleta
chachu ya mabadiliko na maendeleo ya nchi yetu. CUF inawahimiza na kuwatia moyo
wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari wote kwa ujumla kwamba wasikubali
kurudi nyuma, kutishwa na kufungwa midomo na kupokonywa kalamu zao. Ni wakati
muafaka wa kuunganisha nguvu kwa pamoja ili kudai haki zetu za kikatiba,
kulinda na kutetea maslahi mapana ya Taifa letu na wananchi wake.
Kinawataka watanzania wote bila ya kujali
itikadi za vyama vyetu kusimama imara kutetea misingi ya uongozi wa Taifa letu
kwa kuilinda na kuihifadhi katiba na sheria za nchi yetu mpaka turidhike kuwa
zinaheshimiwa, zinafuatwa na kuhuifadhiwa na kila mmoja wetu. Ni suala lililo
wzi kwa kila mmoja wetu sasa kuwa serikali ya awamu ya tano imejawa na hofu ya
nguvu ya mabadiliko inayotokana na wananchi na sasa imeamua kutumia vitisho kwa
kuliamuru jeshi la Polisi kufanya mazoezi ya kijeshi hadharani na kutumia
silaha nzito, lengo likiwa ni kutaka kuwaogopesha kuendeleza harakati za kudai
haki zetu za kidemokrasia. Lazima tuendelee na mapambano hayo ya kudai haki
mpaka ipatikanwe.
Tunawahakikishia watanzania wote kuwa daima
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) itaendelea kusimama imara na
kuendelea kuimarisha umoja na mashirikiano baina yetu ya KUDAI HAKI SAWA KWA
WOTE NA DEMOKRASIA YA KWELI kwa maslahi mapana ya Taifa letu kwa kizazi cha
sasa na kijacho.
Mbarara Maharagande
K/Naibu Mkurugenzi Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
-CUF Taifa
0784 001 408
0 comments:
Post a Comment