JARIDA mashuhuri duniani la Forbes, limezitaja ndege aina ya
Bombardier Dash8 Q400, ambazo tayari Tanzania imezinunua kuwa ni zenye
usalama, zinazotumia mafuta kidogo. Limetabiri kuwa zitakuwa nguzo
muhimu kwa usafiri wa bei nafuu kwa nchi mbalimbali.
Kwa mujibu wa makala iliyochapishwa na jarida hilo ikiwa na kichwa
cha habari “Can Bombardier’s Q400 Save Regional Air Service in the US?”,
mwandishi anafafanua faida ya ndege hizo, ikilinganishwa na ndege
nyingine zinazofanya usafiri wa ndani nchini Marekani.
“Bombadier ina kasi nzuri na ya kutosheleza mahitaji ya safari za
ndani kwa kiwango cha kuwa na faida zaidi kibiashara, ikilinganishwa na
ndege nyingine za aina yake kama ATR,” linaandika jarida hilo la Forbes.
Aidha, jarida hilo linataja faida nyingine ya ndege hizo kuwa ni
uwezo wa kutumia mafuta kidogo, jambo litakalosaidia kupunguza gharama
za usafiri huo wa ndege nchini kwa wasafiri wa ndani. Jarida hilo
linafafanua kuwa kiwango kidogo cha mafuta, kinachotumiwa na ndege hizo,
kunazifanya kuwa na ufanisi wa asilimia kati ya 48 mpaka 50 zaidi ya
ndege nyingine.
Forbes linasisitiza kuwa kutokana na gharama za matengenezo kupanda
na gharama nyingine za uendeshaji, ikiwemo mishahara mizuri kwa
marubani, kuna uwezekano mkubwa kwa Bombardier kuendeshwa kwa bei rahisi
na ikauza tiketi kwa bei rahisi zaidi kuliko ndege nyingine.
“Kwa sasa tunakadiria kuwa ndege aina ya Bombardier, ndizo zitakuwa
mbadala na zitashika njia nyingi za ndani (Marekani) kwa kiasi cha
asilimia 50 hadi 60 na zitasaidia kurejesha usafiri uliositishwa
kutokana na gharama kubwa kwa ndege nyingine katika viwanja takribani
20,” linafafanua jarida hilo.
Akikaririwa katika makala hayo, Mike Arcamone, Rais wa Masuala ya
Biashara wa Bombardier anasema wasiwasi wa awali wa abiria kuhusu ndege
hizo kutumia mfumo wa turbo, sasa umeondoka kwa kuwa injini na miundo ya
kisasa ya ndege hizo, inaifanya isiwe na kelele kama ilivyodhaniwa.
“Wanunuzi wengi wa ndege hizi, wamebaini kuwa hazina kelele na
watumiaji wengi wanaamini kuwa zinaweza kuwa mbadala wa ndege nyingine
za bei nafuu,” anasema ofisa huyo, kauli inayokubaliwa na wachambuzi wa
Forbes.
Tayari Serikali ya Tanzania imeahidi kuleta ndege nyingine ya pili
wiki hii, baada ya ile ya kwanza kuwasili nchini wiki iliyopita ukiwa ni
mkakati na utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli ya kulifufua
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Kuwasili kwa ndege hizo, pia kunaonesha Rais Magufuli anavyojitahidi, akiwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake.
Mbali na kuleta ndege hizo, yapo mambo mengi makubwa ambayo Rais
Magufuli ameanza kuyatekeleza, aliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi
mkuu mwaka jana, hatua ambayo imewavutia watu wengi ndani na nje ya
nchi.
Shirika letu la ndege lilikuwa na hali mbaya kutokana na kushindwa
kujiendesha kutokana na gharama kubwa za uendeshaji na abiria wachache,
wanaotumia usafiri wa anga.
Uchambuzi wa ndege
Wachambuzi mbalimbali nchini, wakiwemo wasomi na wafanyakazi wa
zamani wa ATCL, wamechambua faida na unafuu wa Tanzania kutumia ndege
hiyo kuliko ndege nyingine ambazo zina gharama kubwa.
Wanasema bei halisi ya ndege ya Boeing ambayo inaliliwa na watanzania
wengi ni dola za Marekani milioni 296, wakati ndege ya Bombardier Q400
inauzwa dola za Marekani milioni 35 tu.
Wachambuzi hao wamebainisha kuwa badala ya Tanzania kununua Boeing
moja, ni bora kuongeza kiasi cha dola za Marekani milioni 19 na kununua
ndege aina ya Bombardier tisa.
Kuhusu kasi ya ndege hizo, wachambuzi hao wanakiri kuwa kasi ya ndege
aina ya Boeing ni kubwa kuliko Bombardier kutokana na uchomaji wa
mafuta, kwani kasi ya Boeing ni 590mph kwa saa wakati kasi ya Bombardier
ni 414mph au 667kilometa kwa saa. Kama kutoka Dar es Salaam kwenda
Mwanza ni kilometa 1,100, maana yake Bombardier itatumia saa 1.45 wakati
Boeing itatumia saa 1.15, tofauti yake ikiwa ni dakika 25 tu.
Aidha, Boeing inatumia dumu moja la mafuta la lita nne kwa sekunde
moja, kwa hiyo kwa saa moja ndege hiyo inatumia lita 14,400. Kwa mfano
mafuta ya ndege kwa lita, yakiuzwa Sh 2,000 maana yake ili tutoe mafuta
ya kuelekea safari ya Songea inayochukua takriban saa moja, zinahitajika
lita milioni 28,800,000(14,400×2000) Na itahitajika abiria 96
watakaolipa Sh 300,000 ili kuweza kulipia gharama za mafuta tu, gharama
hizo ni nje ya gharama za huduma na wafanyakazi na faida kwa ujumla.
Kwa upande wa Bombardier, inatumia lita 1.187 ya madumu ya mafuta kwa
maili moja, yaani ukikadiria inatumia lita moja ya mafuta kwa maili
moja.
Kwa mfano, Songea kwenda Dar es Salaam ni takribani kilometa 537, kwa
hiyo itatumia lita 398.386875 ambazo ukizizidisha kwa gharama ya Sh
2,000 kwa lita unapata Sh 796,773. Kwa sasa kumezuka mjadala mkubwa
kuhusu uhalali wa serikali, kununua ndege hizo, huku hoja kubwa zikiwa
ni usalama na gharama za uendeshaji wa ndege hizo. Wiki iliyopita
Serikali iliingiza nchini ndege ya kwanza kutoka Canada aina ya
Bombardier, ilikotengenezwa . Ndege hiyo ya kwanza ilitua kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA)
ikitokea nchini Canada.
Baada ya kutua ndege hiyo, ilipatiwa heshima maalumu ambayo hutolewa
kwa ndege yoyote mpya inayotua katika nchi yake (Water Salute) na kisha
kuegeshwa katika eneo la ndege za jeshi (Airwing Ukonga).
Akizungumza baada ya kuwasili kwa ndege hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamriho alisema ndege ya
pili inatarajiwa kuwasili baada ya wiki moja.
“Baada ya kuwasili ndege ya pili ndipo yatafanyika mapokezi rasmi,
yatakayoongozwa na Rais Magufuli kwa tarehe itakayotangazwa baadaye,”
alisema Chamriho.
Katika taarifa ya awali iliyotolewa na ATCL mwishoni mwa wiki,
ilieleza kuwa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 76 ikiwa na
marubani wanne kutoka Canada ilianza safari ya kuja nchini tangu wiki
mbili zilizopota ikipitia miji ya Reykjavík, Southampton, Malta, Luxor
na Addis Ababa nchini Ethiopia. Ilieleza kuwa ndege hizo, zitaanza
kufanya safari zake mara tu baada ya kukamilisha mchakato wa kusajiliwa
na Mamlaka ya Usalama wa Anga Tanzania (TCAA).
“Kwa kuwa zitakuja zikiwa na usajili wa nchini Canada, tutalazimika
kutumia siku mbili hadi tatu kuziingiza kwenye usajili wa TCAA pamoja na
kukamilisha taratibu zingine za kisheria ili ziweze kupata ruhusa ya
kufanya safari za hapa kwetu,” ilieleza.
Iliongeza kuwa safari ya kwanza ya ndege hiyo inatarajiwa kufanyika Septemba 27, mwaka huu kwenda jijini Mwanza.
“Tutakuwa na madaraja mawili yaani daraja la uchumi (Economy Class)
litakalohusisha abiria 70 na daraja la biashara (Business Class)
litakalohusisha abiria sita kwa kila ndege,’’ ilibainisha. Baadhi ya
mikoa ambayo shirika hilo litaboresha zaidi safari zake kuwa ni Dodoma,
Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara,
Zanzibar, Pemba, Bukoba na Visiwa vya Comoro. Ujio wa ndege hizo
unatajwa kuwa utaleta mapinduzi makubwa kihuduma na kiutendaji kwa
shirika hilo.
Home
News
Slider
JARIDA mashuhuri duniani la Forbes, limezitaja ndege aina ya Bombardier Dash8 Q400 kuwa ni zenye usalama
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment