KOCHA mkuu wa timu ya Simba, Joseph Omog, amesema sasa anaweza
kuufikiria mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani wao wa
jadi Yanga, baada ya kikosi chake kupata ushindi wa kishindo mbele ya
Majimaji FC.
Simba juzi ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji
katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ambapo kocha huyo
raia ya Cameroon, ametangaza kuanza kuifungia kazi Yanga.
Omog alisema baada ya kutoa kipigo
kikali, sasa wanaanza kujipanga kwa pambano la kukata na shoka la
Jumamosi, huku akidai kikosi hicho tayari kimetua mkoani Morogoro.
Alikiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa pande zote kutokana na kila timu kuhitaji ushindi wa pointi tatu muhimu.
Naye kocha msaidizi wa timu hiyo, Mganda Jackson Mayanja, alisema
matokeo ya ushindi mnono waliyoyapata dhidi ya Majimaji, yataongeza
hamasa kwa wachezaji na mashabiki wa timu hiyo kuelekea pambano hilo.
“Tumefurahi kwa matokeo haya yanayotufanya tuendelee kufanya vizuri
ligi kuu, lakini kazi kubwa iliyobaki ni kuutazama mchezo mwingine
unaotukabili mbele yetu dhidi ya Yanga ambao utakuwa wa ushindani wa
hali ya juu.
“Hakika huu ni ushindi wa faraja kwetu, kwani wachezaji wangekuwa
kwenye wakati mgumu sana kama tungekosa ushindi kisha tukaanza
maandalizi ya kupambana na mahasimu wetu,” alisema Mayanja.
Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajia kukutana na mahasimu wao Yanga
kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu huu wa ligi, huku wakiwa
wamepania kulipiza kisasi cha kufungwa na ‘Wanajangwani’ hao msimu
uliopita.
Matokeo ya mchezo wa juzi yaliiwezesha Simba kuendelea kushika usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufikisha pointi 16.
Wakati huo huo, kocha msaidizi wa timu ya Majimaji, Petter Mhina,
alisema kipigo cha Simba kitakuwa cha mwisho kwa kikosi chake kwani
hawataruhusu nyavu zao kutikiswa tena kutokana na wachezaji kupata
mahitaji muhimu waliyokuwa wameyakosa.
“Awali timu ilikuwa inakabiliwa na ukata, hali iliyochangia kushindwa
kufanya vyema katika michezo yote iliyopita, lakini sasa hatutakubali
kufungwa tena,” alisema Mhina.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment