KAMATI ya Utendaji ya Taifa ya Chama cha Wananchi (Cuf), imeandaa
ajenda ya kumfikisha Profesa Ibrahim Lipumba mbele ya Baraza Kuu la
Uongozi wa chama hicho ili ajieleze na kujitetea ni kwa nini
asichukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kitendo chake cha kuvamia
ofisi akiwa na wafuasi wake na kusababisha uharibifu wa mali za chama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa chama
hicho, Nassor Ahmed Mazrui, kutokana na kitendo cha kuvamia Ofisi Kuu ya
chama hicho iliyoko Buguruni, Dar es Salaam na kusababisha uharibifu wa
mali, Kamati ya Utendaji ya Taifa imeitisha kikao cha Baraza Kuu la
Uongozi Taifa kitakachofanyika kesho.
“Kikao hiki kimeitishwa kwa mujibu wa Ibara ya 85(5) na Ibara ya 108
ya Katiba ya Cuf ya mwaka 1992, toleo la mwaka 2014. Kitafanyika kuanzia
saa 4:00 asubuhi kwenye Makao Makuu ya Cuf Zanzibar,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 12 (6), (7) na (16) ya Katiba ya Cuf
ya mwaka 1992, toleo la mwaka 2014, Kamati ya Utendaji ya Taifa imeandaa
ajenda na kumfikisha Profesa Lipumba mbele ya Baraza hilo ili ajieleze
kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa mambo aliyoyafanya.
Katika hatua nyingine, Mazrui alisema kamati hiyo imekataa maoni na
ushauri uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Fransis
Mutungi.
Alisema baada ya kupitia maoni na ushauri wa Msajili wa Vyama vya
Siasa nchini juu ya malalamiko yaliyowasilishwa katika ofisi yake na
Profesa Lipumba na wanachama wenzake waliochukuliwa hatua za kinidhamu
na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Kamati hiyo inakataa na kupinga kwa
hoja thabiti ushauri na maoni yaliyopendekezwa na Msajili.
Alisema kamati hiyo inaendelea kusimamia uamuzi wa Mkutano Mkuu
Maalum wa Taifa wa Agosti 21, mwaka huu uliokubali kujiuzulu kwa Profesa
Lipumba kama Mwenyekiti wa Chama na uamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi
Taifa uliofikiwa katika kikao chake cha Agosti 28 mwaka huu.
Alisema, uamuzi huo ni wa kuwasimamisha uanachama Profesa Lipumba,
Magdalena Sakaya, Maftah Nachuma, Abdul Kambaya, Masoudi Mhina, Thomas
Malima, Ashura Mustafa, Kapasha Kapasha, Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa,
Haroub Shamis na kumfukuza uanachama Shashu Lugeye.
Alisema Katiba ya Cuf haina kifungu chochote kinachompa mamlaka
Msajili wa Vyama vya Siasa kupokea rufaa kuhusu uamuzi wa vikao vya
chama wala kubatilisha uamuzi wa vikao hivyo.
Baada ya kupitia hoja 11, Jaji Mutungi alimrejesha katika wadhifa
wake wa Uenyekiti Profesa Lipumba, hali iliyosababisha mchumi huyo
kuingia ramsi juzi ofisini kwa chama hicho, Buguruni na kuzua tafrani
kutoka kwa wanachama wanaompinga.
.............................................................................................................................
HOJA 11 zilizotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji
Francis Mutungi, zimetosha kumrejesha katika wadhifa wake, Mwenyekiti
‘aliyejiuzulu’ wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Mbali ya Lipumba viongozi wengine ambao msimamo wa Msajili
unawarejesha madarakani moja kwa moja baada ya kusimamishwa na Baraza
Kuu la Uongozi la CUF, katika kikao chake cha Agosti 30, mwaka huu
kilichofanyika jijini Dar es Salaam ni Naibu Katibu Mkuu Bara Magdalena
Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua na Naibu Mkurugenzi wa Habari
Taifa, Abdul Kambaya.
Wengine ni Mbunge wa Mtwara, Maftaha Nachuma, wajumbe wa Baraza Kuu
Taifa, Masudi Omari Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa na Kapasha
Kapasha. Pia Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa na Haroub Shamis ambao
wataendelea kuhesabika kama wanachama halali wa chama hicho.
Katika barua yake kwa viongozi wa CUF, Msajili alieleza kuwa amefikia
msimamo wake huo baada ya kupata nafasi ya kusikiliza pande zote
zinazosigana katika mgogoro huo wa uongozi ndani ya chama hicho.
Alisema katika kufikia maamuzi hayo amezingatia Mamlaka na wajibu wa
Msajili kushughulikia mgogoro huo, Kujiuzulu kwa Profesa Lipumba,
Profesa Lipumba kutengua barua yake ya kujiuzulu, Uhalali wa Mkutano
Mkuu Maalumu wa CUF wa Agosti 21, mwaka huu na baadhi ya wajumbe wa
Mkutano Mkuu Maalumu kuhitaji Profesa Lipumba aitwe katika chumba cha
mkutano kujieleza.
Nyingine ni uhalali wa kura zilizopigwa kukubali au kukataa Profesa
Lipumba kujiuzulu, uhalali wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
la Agosti 28, mwaka huu, utaratibu wa kuchukua hatua za kinidhamu,
uhalali wa kamati iliyoundwa na Baraza Kuu la Uongozi la Agosti 28 ili
kufanya kazi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Taifa na mwisho ni
kuhusu uhalali wa uteuzi wa viongozi wa kitaifa uliofanywa na kikao cha
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha Agosti 28, mwaka huu.
Kutokana na hoja hizo, Jaji Mutungi katika taarifa yake kwa vyombo
vya habari jana alisema: “Hivyo, baada ya upembuzi kama nilivyobainisha
hapo juu, msimamo na mwongozo wangu ni kwamba Profesa Ibrahim Lipumba
bado ni Mwenyekiti halali wa Taifa wa CUF na walalamikaji wanachama
waliosimamishwa na waliofukuzwa uanachama wote bado ni wanachama halali
wa CUF.
“Aidha viongozi ambao uongozi wao uliathirika na maamuzi yasiyo
halali ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha Agosti 28, mwaka
huu, bado ni viongozi halali. Natumia fursa hii kuwapa angalizo kwamba,
kwa kuwa kamati iliyoundwa kuongoza chama na viongozi walioteuliwa na
kikao hicho si halali na kwa kifungu cha 88 (2) cha Sheria ya Vyama vya
Siasa Sura ya 258, hawaruhusiwi kufanya shughuli yoyote ya chama.”
Msajili kushughulikia mgogoro
Msajili akifafanua hilo alisema kwa kifungu cha 10 (f) cha Sheria ya
Vyama vya Siasa Sura ya 258 kinahitaji chama cha siasa kuwasilisha
orodha ya viongozi wake wa kitaifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kwa
kuwa Kifungu 8A (1) kinampa mamlaka Msajili kuhifadhi taarifa za
viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa na kwa kuwa Kanuni ya 5 (1) ya
Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa toleo namba 111 la mwaka 1992
inakitaka kila chama kuwasilisha taarifa kwa Msajili panapotokea
mabadiliko ya uongozi wa kitaifa wa chama husika.
“Hivyo kwa mustakabali wa majukumu yanayotolewa na vifungu hivyo,
Msajili wa Vyama vya Siasa anao wajibu wa kuhakikisha taarifa za
mabadiliko ya uongozi anazoletewa na chama cha siasa ni sahihi, kwa
maana ya kujiridhisha kuwa mabadiliko hayo ya uongozi yamefanyika na
mamlaka halali ya chama na pia yametekelezwa kwa mujibu wa Katiba na
Kanuni za chama husika. “Kwa mantiki hiyo basi na nikijielekeza kwenye
vifungu vya sheria nilivyoainisha, ni dhahiri kwamba Msajili wa Vyama
vya Siasa anayo mamlaka na wajibu wa kisheria, kuchunguza na
kujiridhisha kuhusu usahihi wa mabadiliko katika uongozi wa kitaifa wa
chama yaliyofanyika na masuala yote yanayohusiana na mabadiliko hayo,”
alisema Msajili.
Kujiuzulu kwa Profesa
Lipumba Kuhusu hilo Msajili alisema kwa mujibu wa Ibara ya 117 (2),
kiongozi wa Chama cha CUF, hata kama mhusika amebainisha tarehe ya
kujiuzulu katika barua yake ya kujiuzulu, atahesabika kuwa amejiuzulu
baada tu ya mamlaka iliyomchagua au kumteua kukubali.
Alisema kwa mujibu wa Ibara hiyo, ni sahihi kusema kwamba Profesa
Lipumba alikuwa bado ni Mwenyekiti halali wa Taifa wa CUF hata wakati wa
kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Agosti 21, hivyo hata yeye kujiita
Mwenyekiti wa Taifa mstaafu kabla ya kujiuzulu kwake kukubaliwa na
mamlaka husika si sahihi.
Kutengua barua yake ya kujiuzulu
Akizungumzia hilo Msajili alisema, “Katiba ya CUF iko kimya kuhusu
hilo, hivyo hapakuwa na kizuizi kwa Profesa Lipumba kutengua barua yake
ya kujizulu kwa kuzingatia ukimya huo kwa upande wa uongozi wa CUF
kuchukua hatua pindi walipopokea barua yake ya kujiuzulu na hivyo kutoa
mwanya kwa mhusika kuitengua barua yake ya kujiuzulu.
“Si hivyo tu, bali pia barua yake ya kutengua kujiuzulu haikukataliwa
na uongozi wa CUF.Alichoelezwa Profesa Lipumba ni kwamba asianze kazi
tarehe aliyopanga kuanza kazi ili asubiri kwanza Katibu Mkuu ashauriane
na wanasheria wa chama, ambapo mpaka suala hili linawasilishwa mbele
yangu, Profesa Lipumba alikuwa bado hajapewa mwongozo wowote kuhusiana
na barua yake ya kutengua kujiuzulu,” alisema Msajili.
Uhalali wa hoja
Msajili akitoa msimamo wake kuhusu hoja ya uhalali wa Mkutano Mkuu wa
Agosti 21, alisema pamoja na malumbano kuhusu akidi ya wajumbe lakini
kwa vyovyote vile mkutano huo ulikidhi matakwa ya Ibara ya 114 inayosema
kuwa ili akidi kutimia idadi ya wajumbe waliohudhuria kikao inapaswa
kuzidi nusu ya wajumbe wote, na hivyo idadi ya wajumbe 700 ilikidhi
matakwa ya Katiba.
Kuhusu hoja ya baadhi ya wajumbe kuhitaji Profesa Lipumba aitwe
katika chumba cha mkutano kujieleza, Msajili alisema hata kama Profesa
Lipumba angekuwa si mjumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu ili mradi uwepo wake
yalikuwa ni matakwa ya wajumbe wa mkutano huo, basi alipaswa kupewa
fursa katika mkutano huo kuthibitisha kuwa, barua iliyosomwa na Katibu
Mkuu kuhusu kujiuzulu kwake ni yake na kueleza sababu za kujiuzulu na
hivyo kumkatalia ilikuwa ni kukiuka Ibara ya 116 ya Katiba ya chama
hicho.
Kwa hoja za uhalali wa kura zilizopigwa kukubali au kukataa Profesa
Lipumba kujiuzulu, Msajili alisema zoezi la kupiga kura za kukubali au
kukataa kujiuzulu kwa Profesa Lipumba lilifanyika katika mazingira ya
vurugu na hivyo kufanya zoezi hilo kukosa uhalali na kutoa mfano kuwa
zoezi la kujua idadi ya wapiga kura kabla ya kupiga kura halikufanyika,
ukizingatia kuwa baada ya vurugu kuzuka, kuna wajumbe walitoka nje ya
ukumbi kuogopa vurugu na watu wasio wajumbe kuingia ndani ya ukumbi.
Kuhusu uhalali wa uteuzi wa viongozi wa kitaifa uliofanywa na kikao
cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha Agosti 28, Msajili alisema kwa
mujibu wa Ibara ya 115 (1) iwapo nafasi ya kiongozi yeyote ipo wazi,
basi mamlaka yake ya uteuzi itamteua mtu wa kukaimu nafasi hiyo.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 91 (1) (m) mamlaka ya uteuzi wa Naibu Katibu
Mkuu ni Baraza Kuu la Taifa, hivyo laiti uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu
la Uongozi Taifa cha Agosti 28 ungekuwa si batili, basi uteuzi wa Joran
Bashange kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu ungekuwa sahihi, kwa maana ya
kwamba Baraza Kuu la Uongozi lina mamlaka hayo.
“Hata hivyo kwa upande mwingine, uteuzi wa Mbaraka Maharagande kuwa
Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma una
dosari nao si sahihi kwa sababu kwa mujibu wa Ibara ya 91 (1) (f)
mamlaka yake ya uteuzi ni Mwenyekiti wa Taifa na si Baraza Kuu la
Taifa,” alisema Msajili na kusema adhabu kwa mtu anayefanya shughuli za
chama bila kufuata taratibu ni kifungo cha miezi sita, faini isiyozidi
Sh milioni moja au vyote kwa pamoja.
Lipumba atinga ofisini kwa mdundiko
Katika tukio lingine mchana jana Profesa Lipumba alifika katika ofisi
za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam huku akiandamana
na umati wa wafuasi wa chama hicho huku wakisindikizwa na ngoma maarufu
katika ukanda wa Pwani ya Mdundiko.
Wafuasi wa Profesa
Lipumba walianza kukusanyika katika ofisi hizo kuanzia asubuhi baada
ya kupata taarifa za kuwepo kwa barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya
Siasa, ikimtambua mwanasiasa huyo kama Mwenyekiti halali wa chama hicho
kwa mujibu wa Katiba ya chama.
Ilipotimu saa saba mchana Profesa Lipumba alifika katika eneo zilipo
ofisi hizo akiwa na kundi la wafuasi wake waliokuwa wakicheza kwa ustadi
ngoma ya mdundiko, lakini walikumbana na kizuizi cha kuingia ndani
kutokana na geti kuu kuwa limefungwa.
Zuio hilo lilidumu kwa muda usiozidi dakika nne, ambapo baadaye
baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo waliamua kuruka ukuta ili kuingia
ndani kumfungulia geti kumwezesha kuingia ndani.
Wakati matukio hayo yakiendelea, polisi waliokuwa wamefika mapema ili
kudhibiti usalama katika eneo hilo walikuwa wakishuhudia wakiwa ndani
ya magari matatu yaliyokuwa yamesimama kando ya geti, wakiwatazama
wafuasi hao wakitumia nguvu ili kuingia ndani ya ofisi hizo.
Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kuingia ndani ya ofisi hizo kwani
wakati wakiendelea kuruka ukuta, zilisikika risasi zikipigwa na askari
wa kampuni binafsi ya ulinzi aliyekuwa analinda ofisi hizo, lakini
alidhibitiwa baadaye na wafuasi hao ambao walimnyang’anya silaha na
kuikabidhi kwa polisi.
Baadaye wafuasi hao walianza kumpa kichapo askari huyo wa ulinzi
kabla ya wazee wa chama hicho kujitokeza na kumuokoa na kulazimika
kumfungia katika choo kimojawapo cha ofisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuingia ofisini
kwake, Profesa Lipumba alisema kurejea kwake kunatokana na uamuzi
uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, huku akieleza hatua mbalimbali
alizochukua tangu alipoandika barua ya kujiuzulu, barua ya kutengua
uamuzi wake na yaliyotokea katika vikao mbalimbali vya chama hicho,
ambazo kimsingi zinamfanya kuwa na sifa ya kuendelea kuwa Mwenyekiti
halali kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.
CUF wajibu mapigo
Hata hivyo jana jioni Chama cha CUF kilitoa taarifa kwa vyombo vya
habari kikisema kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992
haimpi mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa
ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya
vikao vya chama.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui ilisema
katika taarifa ya chama hicho kuwa, “Chama kimepokea kutoka Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na Ushauri wa
Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa Chama
cha Civic United Front (CUF)” ambao uliwasilishwa Ofisi Kuu ya Chama,
Buguruni, jana usiku. Chama hakikuomba ushauri kwa Msajili na hivyo
tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe.”
Alisema chama hicho kinawataka wanachama wake na wananchi wote
kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri
yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya
siasa na kuyatolea uamuzi na kwamba uwezo huo ni wa Mahakama pekee.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment