AGIZO la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo la kutaka madai sugu ya
walimu katika Jiji la Arusha yalipwe ndani ya siku 14 limezaa matunda,
kwani madai yao yote yaliyofikia zaidi ya Sh milioni 169.7, yamelipwa.
Gambo alitoa agizo hilo alipokutana na walimu wa shule za msingi na
sekondari mkoani Arusha waliompa malalamiko mengi, likiwemo la madai
sugu ya walimu na hapo hapo Mkuu huyo aliagiza halmashauri zote na Jiji
mkoani humo kulipa madeni hayo ndani ya siku 14.
Katika kutekeleza agizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel
Daqarro alisema Jiji limetekeleza ndani ya siku mbili na kufanikiwa
kulipa kiasi hicho cha fedha kwa walimu wote wa msingi na sekondari.
Daqarro alisema Jiji la Arusha lina jumla ya walimu 701 wa msingi na sekondari na madai yao yote yamelipwa ndani ya muda huo.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli
inawajali na kuwalinda walimu wote na kuwapa stahili zao za msingi kwa
wakati bila ya kipingamizi chochote.
Mkuu huyo alisema walimu walikuwa wakidai stahili zao za muda mrefu,
ikiwa ni pamoja na fedha za kujikimu, likizo, nauli, matibabu na
upandishwaji madaraka na fedha hizo zote wamelipwa.
Alisema kwa sasa serikali ya wilaya ya Arusha inataka kuona walimu
wakifanya majukumu yao ya msingi katika kupandisha elimu ikiwa ni pamoja
na kufundisha wanafunzi bila ya kuwa na mawazo.
Akizungumzia upatikanaji wa fedha hizo kwa muda huo mfupi alisema
Halmashauri ya Jiji la Arusha iliamua kusitisha malipo yasiyokuwa ya
lazima au kuondoa malipo ambayo yako kinyume na taratibu na ndiyo maana
fedha hizo zimepatikana.
Mkuu huyo alisema si kwamba fedha za kuwalipa walimu zilikuwa hazipo,
bali zilikuwa zikilipa vitu vilivyo nje ya utaratibu na kutokana na
usimamizi wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia ameweza
kubana mianya yote ya ulaji fedha.
“Fedha nyingi za Jiji la Arusha zilikuwa zikilipwa kiholela holela na
kufanya walimu kuteseka na kuumia pasipokuwa na sababu za msingi. Kwa
sasa mianya hiyo imezibwa na ndio maana sasa fedha zinaonekana na
zinalipa wahusika wenye kudai madeni yao ya muhimu kama haya ya walimu,”
alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment