Image
Image

Ustaarabu unahitajika zaidi kuelekea mechi ya watani

MECHI ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Soka Tanzani Bara kati ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga itanatarajiwa kufanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Mbali na mtanange huo kuwa na ushindani ndani ya uwanja, ni mchezo unaovuta hisia za wanachama na mashabiki wengi wa soka hapa nchini tofauti na mechi nyingine zinazofanyika katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kuelekea mchezo huo, serikali tayari imeshatangaza utaratibu wa kutumia mfumo mpya wa tiketi za kielektroniki.
Uamuzi huo unamaanisha kuwa, kila shabiki ambaye atahitaji kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo, ajiandae kununua tiketi kwa mfumo huo wa kisasa na kuacha kufikiria kununua tiketi za 'vishina' kama ilivyokuwa katika mechi zilizopita.

Kila shabiki atatakiwa kukubaliana na uamuzi huo wa serikali ambao unaaminika utasaidia kudhibiti wizi wa mapato ya milangoni na hatimaye wachezaji ambao ndiyo hutumia nguvu katika kucheza, kufaidika na jasho lao.
Hakuna jambo lisilowezekana, miundo mbinu na maandalizi kuelekea mfumo huo mpya yamefanyika na kinachofuata ni utekelezaji.

Kama iliwezekana wapiga kura kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na hatimaye kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa kupata Rais, Wabunge na Madiwani mwaka jana, mashabiki wa soka vile vile wanatakiwa kujiandaa kutumia mfumo huo wa kisasa.
Ili kuachana na fikra za 'kizamani', na kwenda na kasi ya maendeleo, mashabiki na wadau wa soka wanatakiwa kujipanga kuukubali mfumo huo na kusaidia wale ambao wanaoupinga kuchana na dhana hiyo.
Hakika kila jambo huwa na mwanzo wake, na mfumo huu mpya sasa umefika wakati utaanza kutumika na kumaliza 'kelele' za wizi wa mapato.

Kufaulu au kushindwa kwa mfumo huu, kutatokana na ushirikiano utakaotolewa na mashabiki wa soka nchini ambao ndiyo wadau wa mchezo huo.
Endapo mashabiki wa soka watakuwa tayari kuukubali mfumo huo kwa kununua tiketi mapema na kufika uwanjani mapema, tunaamini vita dhidi ya ulanguzi wa tiketi ukatomeshwa na hatimaye dawa ya makusanyo itakuwa imepatikana.
Katika kipindi hiki cha Hapa Kazi Tu, ni vyema pia wadau wa soka wakaendana na kauli hiyo ya Rais John Magufuli kwa kujiandaa kuukubali mfumo huo mpya ukatekelezeka badala ya kujipanga kuonekana kwamba ni ndoto hapa nchini kutumika.
Sheria ni msumeno, tayari uamuzi huo umeshafanyika na kinachotakiwa ni kuunga mkono na haitakuwa busara kuona mashabiki wanafika uwanjani na kulazimisha kutaka kuingia uwanjani kwa kutumia utaratibu ambao si rasmi kwa kigezo cha kupinga mfumo huo.
Kama zilivyo huduma nyingine, shabiki ambaye atanunua tiketi yake mapema na kufika uwanjani mapema, atakuwa na uwezo wa kuingia na kushuhudia mchezo huo bila bugudha ya aina yoyote.
Mpira ni furaha, haitapendeza kuona siku hiyo ya mchezo, mashabiki wanafanya uharibifu wa miundombinu iliyopo kwenye uwanja huo wa kisasa ambao umejengwa kwa kodi za wananchi.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment