HATUA ya Serikali kuwa katika maandalizi ya kuliondoa fao la kujitoa
imezua taharuki miongoni mwa wafanyakazi ambao wengi wao ni wanachama
wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Hali hiyo imekuja baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kuandaa muswada wa
mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambao kwa sasa upo
katika hatua za mwisho, huku ikielezwa kuondolewa kwa fao la kujitoa na
badala yake kuletwa fao la kutokuwa na ajira.
Taarifa za kuondolewa kwa fao hilo zimesambaa kwenye mitandao ya
kijamii, hivyo kuzua mjadala mkubwa kwa wafanyakazi wa sekta mbalimbali
nchini.
Katika mapendekezo hayo inaelezwa kuwa mfanyakazi ambaye amechangia
zaidi ya miezi 18, atalipwa asilimia 30 ya mshahara wake wa mwisho baada
ya kupoteza ajira.
Mbali na hilo, pia atalipwa kwa miezi sita mfululizo, kisha malipo
hayo yatasitishwa. Anayestahili malipo hayo ni yule ambaye hakuacha kazi
kwa hiari yake (resignation).
Inaelezwa katika mapendekezo hayo ya awali kuwa baada ya miaka mitatu
tangu kusitishwa kwa fao la kujitoa, mfanyakazi atakayekuwa hajapata
ajira ataruhusiwa kuhamisha michango yake kutoka kwenye mfuko wa lazima
(Compulsory Scheme), kwenda mfuko wa hiari (Supplementary Scheme).
Kutokana na mabadiliko hayo, mfanyakazi atakuwa na hiari kuchukua
fedha zake kulingana na mfuko wa hiari aliojiunga nao na pia atakuwa na
haki ya kuendelea kuchangia.
“Na kwa mfanyakazi aliyeachishwa kazi akiwa amechangia chini ya miezi
18, atakuwa na haki ya kuchukua asilimia 50 ya michango yake mara baada
ya ajira kukoma,” ilieleza sehemu hiyo ya mapendekezo ya sheria hiyo.
Kutokana na taharuki hiyo ya kuondolewa kwa fao la kujitoa, MTANZANIA
ilimtafuta Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka ambaye alikiri kuwapo kwa
muswada huo ambao bado upo katika hatua za awali.
Alisema hatua ya kufanyika kwa marekebisho hayo inatokana na mifuko ya hifadhi ya jamii kutokuwa na sheria ya fao la kujitoa.
“Sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii hazina fao la kujitoa, ila kwa
sasa suala hilo lipo katika ngazi ya mapendekezo, ikiwamo upande wa
Serikali. Na baada ya kukamilika yatachukuliwa na kwenda kwa wadau na
kujadiliwa kabla halijaridhiwa.
“Na linafanyika hili kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuweza
ku-access (kupata). Hivyo ni vema tusubiri kwanza Serikali iliridhie
ndiyo tunaweza kusema.
“SSRA tunawaomba Watanzania wasubiri maelekezo ya Serikali kwanza, na hawana haja ya kuhamaki kwa suala hilo,” alisema Irene.
KAULI YA SERIKALI
MTANZANIA ilipomtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,
Uratibu, Bunge Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu, Jenista
Mhagama kuzungumzia suala hilo, alisema kwa sasa bado wanaendelea na
kazi ya kushauriana na wadau na ikikamilika atatoa taarifa kwa umma.
“Kwa sasa bado tunaendelea na kuzungumza na wadau ili kuweza kupata
maoni yao, na tukikamilisha kazi hii tutatoa taarifa kwa umma,” alisema
Jenista.
WAZIRI KIVULI
Akizungumzia muswada huo, Waziri Kivuli wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Uratibu, Bunge Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu, Esther
Bulaya (Chadema), alisema muswada huo hauna dhamira njema na badala
yake unataka kuwafunga watu kwa hiari.
“Muswada huu hauna dhamira njema kwa wafanyakazi na ndiyo maana
unataka kupelekwa bungeni kwa njia za panya… Utakumbuka huko nyuma wadau
walioukataa. Sasa inakuwaje maoni ya wadau yafanywe siri katika suala
linalohusu haki za wafanyakazi?
“Tunajua namna Serikali inavyokopa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii
kwa ajili ya miradi ya maendeleo, leo kutaka kuondoa fao hili ni sawa na
kuwafunga kwa hiari.
“Huku nyuma mtu aliweza kufanya kazi na kama aliacha aliamua kuchukua
fedha zake ili zimsaidie kwenye miradi, sasa kuja na utaratibu wa
muswada huu haikubaliki,” alisema Bulaya ambaye bado anatumikia adhabu
yake ya kutohudhuria vikao vya Bunge.
TUCTA WAPINGA
Akizungumzia muswada huo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholaus Mgaya, aliitaka Serikali
kuliacha fao la kujitoa kwa sababu linaweza kuwasaidia wafanyakazi
kujiunga na mfuko wanaoutaka ili waweze kupata faida.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa simu, alisema kuwa miongoni mwa
mambo ambayo shirikisho hilo lilikuwa likiyapigia kelele ni pamoja na
kuanzishwa kwa fao hilo ambalo linaweza kuwasaidia wafanyakazi.
“TUCTA tuliwasilisha mapendekezo ya kuitaka Serikali kuanzisha fao la
kujitoa ili kutoa fursa kwa wafanyakazi kujiunga na mfuko wanaotaka,
ambao wanaona wanaweza kupata faida zaidi, jambo ambalo limesaidia hata
baadhi ya wabunge kutuunga mkono,” alisema Mgaya.
Alisema TUCTA inapinga uamuzi wa Serikali kutaka kuwalipa wafanyakazi
ndani ya miezi sita halafu wanawaacha, kwa sababu wanaweza
kuwasababisha waendelee kuwa masikini.
Mmoja wa wadau alihoji ni namna gani mfanyakazi anayelipwa mshahara
wa Sh 180,000 ataweza kumudu gharama za maisha baada ya kupoteza ajira
kwa kulipwa asilimia 30 ya mshahara wake.
“Mfanyakazi anayelipwa mshahara wa Sh 180,000 kama akilipwa asilimia
30 ya mshahara wake ni sawa na Sh 54,000 kwa mwezi baada ya kupoteza
ajira yake, huyu ni vipi ataweza kumudu gharama za maisha?” alisema.
Aprili 13, mwaka 2012 Bunge lilifanya marekebisho na kuondoa fao la
kujitoa (withdrawal benefits) – mafao ambayo yalikuwa yakitolewa pindi
mwanachama alipokuwa anaacha kazi na kulazimu kupata mafao pale
atakapofikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55), kwa lazima (miaka
60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu.
Kutokana na marekebisho hayo, Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM) –
kwa wakati huo, aliwasilisha muswada binafsi bungeni wa kutaka sheria ya
mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2012, hususan kipengele
kinachomtaka mfanyakazi kupata mafao yake baada ya kufikisha umri wa
kustaafu kwa hiari miaka 55 au 60 kirekebishwe.
Jafo ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI),
alifikia uamuzi huo baada ya kuona kukiwa hakuna dalili kwa Serikali
kuwasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya sheria kama ilivyoahidi.
Hatua hiyo ya Jafo, aliichukua baada ya aliyekuwa Mbunge wa Ubungo –
sasa Kibamba, John Mnyika (Chadema), kuwasilisha kwa Katibu wa Bunge
kusudio la kuwasilisha muswada binafsi wa sheria hiyo kwa hati ya
dharura.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment