MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi imezuia kupigwa mnada
mali za Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe, hadi uamuzi wa pingamizi lililowasilishwa na Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) kuhusu maombi yake utakapotolewa.
Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa jana mbele ya Jaji Sivangilwa
Mwangesi baada ya kusikiliza hoja za sheria kuhusu maombi ya zuio la
muda yaliyowasilishwa na Mbowe na pingamizi lililowasilishwa na NHC.
Katika maombi hayo namba 722 ya 2016, Mbowe anawakilishwa na Mawakili
Peter Kibatala na Omari Msemo wakati NHC inawakilishwa na Mawakili
Aloyce Sekule na Mariamu Mungula.
Mbowe Hotels Limited imewasilisha maombi chini ya hati ya dharura
dhidi ya NHC na Kampuni ya Udalali ya Poster and General Traders.
Wanaomba mahakama iamuru wadaiwa wamrudishe mdai katika ghorofa
namba 007 lililopo Plot No. 725-726/24 Mtaa wa Mkwepu/Indira Gandhi
(Makunganya), Manispaa ya Ilala yenye hati namba C. T No. 186018/15 and
C. T No. 186018/10 kwa vile walimuondoa kwa makosa.
Kibatala anadai wadaiwa wote wawili, Septemba mosi bila ridhaa ya
mahakama walimuondoa mteja wake wakati usuluhishi ukiendelea kuhusu
mkataba wa ubia walioingia Mbowe Hotels Limited na NHC kuhusu jengo
hilo.
Inadaiwa notisi ya kumuondoa ndani ya jengo hilo ilipelekwa kwa
Kampuni ya Free Media Limited ya Tanzania Daima wakati yeye ni Mbowe
Hotels hivyo waliiomba mahakama iamuru NHC na Kampuni ya Udalali
warudishe vitu walivyopora.
Maombi hayo yaliwasilishwa kwa hati ya dharura na yaliambatanishwa na kiapo kilichoapwa na Freeman Aikael Mbowe.
NHC na Kampuni ya Udalali waliwasilisha pingamizi la awali wakidai
kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo ya Mbowe
kwa sababu hakuna kesi ya msingi.
Wadai wakijibu pingamizi hilo walidai wanaomba mahakama itoe amri ya
muda huku wakisubiri usuluhishi kujua iwapo kweli Mbowe anadaiwa kodi
ama la.
Awali, Kibatala aliomba pingamizi hilo na maombi yasikilizwe kwa
pamoja kwa sababu anahofia kuna mbinu za kuchelewesha kesi kwa vile
hata pingamizi hilo ni njia mojawapo ya ucheleweshaji wa kesi.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Mwangesi aliamuru wadaiwa wasiuze
mali za Mbowe hadi uamuzi wa pingamizi utakapotolewa Septemba 16 mwaka
huu.
Kampuni ya udalali ilipewa na NHC kazi ya kumwondoa Mbowe katika
jengo hilo kwa madai ya kushindwa kulipa kodi ya pango, Sh bilioni 1.2.
Mbowe aliondolewa kwenye jengo hilo Septemba Mosi, siku chache baada
ya NHC kutangaza orodha ya wapangaji wake ambao ni wadaiwa sugu,
ikiwamo kampuni hiyo ya Mbowe.
Katika hati yake ya kiapo, Mbowe anadai kuwa yeye ni mmoja wa
wamiliki wa jengo hilo na kwamba analimiki kwa ubia baina yake na NHC.
Mbowe anadai analimiki jingo hilo kwa asilimia 75 huku NHC ikiwa na umiliki wa asilimia 25 tu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment