WAKATI
taifa likiwa katika majonzi kutokana na vifo 17 vilivyotokana na
tetemeko la ardhi na kuacha majeruhi zaidi ya 253 mkoani Kagera wiki
iliyopita, siri ya kushindwa kupimwa matetemeko nchini imebainika.
Imeelezwa
kuwa vituo vitatu vikubwa vya kupima matetemeko vimefungwa baada ya
kuhujumiwa na vingine vidogo 38 navyo vimefungwa baada ya wafadhili
kujitoa.
Hayo
yalielezwa jana na Jiolojia Mwandamizi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania,
Gabriel Mbogoni alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.
“Kwa
kweli wanajiolojia tunapata changamoto kubwa katika kupima na kujua
iwapo tetemeko litatokea katika eneo fulani na hiyo inatokana na
kuhujumiwa baadhi ya mashine katika vituo vyetu.
“Tulikuwa
na vituo zaidi ya 10 vya kupima matetemeko, hivi sasa vimebaki tisa
pekee na ili kupata uhakika kama kuna tetemeko kwenye eneo fulani lazima
uwe na vituo zaidi ya vitatu,” alisema.
Alisema vituo vilivyofungwa baada ya kuibwa vilikuwa katika mikoa ya Morogoro, Dodoma (Ntuka) na Arusha eneo la Longido.
“Ili tuweze kusimika mashine za kupima tetemeko tunahitaji kupata eneo ambalo lina mwamba mgumu.
“Zamani
tulikuwa tukitafuta maeneo yenye miamba migumu huko vijijini, tukipata
tunawasiliana na viongozi wa kijiji na tunaweka walinzi wa kulinda
mashine hizo.
“Lakini
zimeibwa hali iliyosababisha kufungwa vituo hivyo…tulipeleka kesi
mahakamani mwisho tukaona ni vema sasa tuanze kuzifunga mashine hizo
katika maeneo ya magereza kwa usalama wake isipokuwa kile cha Mtwara na
Dodoma,” alisema.
Alisema wezi hao, wamekuwa wakiiba mashine hizo wakidhani wanaweza kunufaika, wakizifananisha na madini.
“Wengi
wanadhani zinamilikiwa na Wizara ya Nishati na Madini kwamba wakiziiba
watauza wapate faida. Unajua mashine hizi zipo kama sanduku, wanapoziiba
huwa hawawezi kuziuza popote kwa sababu zinatambulika,” alisema.
Mbogoni
alisema vituo vikubwa vilivyobakia vipo katika mikoa ya Mtwara, Dodoma,
Geita, Arusha, Babati, Singida, Mbeya na Manyara.
Akizungumzia
vituo vidogo 38 vilivyofungwa, alisema hiyo ilitokana na kumalizika
mradi wa kupima matetemeko uliokuwa ukifanywa na wakala huo kwa
kushirikiana na Chuo cha Pennyslvania State cha Marekani.
“Siwezi
kutaja tumepata hasara kiasi gani kwa sababu sijui mashine hizo
zilinunuliwa kiasi gani na sasa zinauzwa kiasi gani. Huwa tunazipata
kutoka kwa ufadhili wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Awamu ya kwanza wa mradi ulianza 2007 hadi 2008 halafu ukaanza tena 2013 hadi April 2015 ambako uliisha,” alisema.
Mbogoni alisema matetemeko mengine madogo yataendelea kutokea kwa muda.
“Ni
hali ya kawaida linapotokea tetemeko kubwa huwa baadaye yanatokea
mengine madogo madogo, yanaweza yakadumu hata kwa wiki au hadi miezi
minne.
“Hii
ni kwa sababu ile nguvu ya mgandamizo inayotokea ambayo husababisha
miamba kumeguka huwa bado haijaisha na ndiyo maana tetemeko huendelea
kutokea,” alisema.
Juzi,
tetemeko kubwa lilitokea katika maeneo ya Kanda ya Ziwa hususan mkoani
Kagera lilisababisha zaidi ya vifo 15 huku likiacha majeruhi zaidi ya
253.
Tetemeko
hilo limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840
kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa, yakiwamo majengo 44 ya taasisi
mbalimbali za umma.
WANANCHI
Wakati
huohuo, baadhi ya wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi mkoani
Kagera wiki iliyopita wameiomba Serikali kuwasaidia kujenga mahema
haraka weweza kujihifadhi kutokana na nyumba zao kuanguka
Wakizungumza
na MTANZANIA kwa nyakati tofauti mjini Bukoba jana, wananchi hao
walisema hivi sasa wanalazimika kulala nje bila kuwa na kitu chochote
cha kuwahifadhi.
Mmoja
wa wananchi hao, Evodius Gozbert mkazi wa Bukoba mjini, alisema
anakabiliwa na hali ngumu kutokana na nyumba yake yote kubomoka.
“Nimepoteza
nyumba zangu, tunahitaji msaada wa haraka kutoka serikalini, wasiwasi
wetu hapa mvua ikianza kunyesha tutakimbilia wapi.
“Kama
ulivyosikia juzi saa 4.00 usiku na jana asubuhi tetemeko lilijirudia,
hii inaonyesha wazi bado lipo, lazima tuwe na sehemu za kijikinga ndugu
yangu,”alisema
Naye Joyce Ndukeke alisema tangu kutokea tetemeko hadi jana jioni alikuwa hajapata msaada kutoka serikalini.
“Mimi
ni mzazi wa watoto wanne, nyumba zote zimeanguka, nasikitika mume wangu
yuko safarini, hatuna pa kulala hapa si umeona limejirudia tena, hapa
tumetawaliwa na hofu,”alisema.
Mutalemwa
Emmanuel alisema wamekumbwa na hofu kubwa kwa sababu hata wanashindwa
kutafuta vyumba vya kupanga katika nyumba nyingine, kwa sababu nazo
zinaweza kuanguka.
Naye
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Rwome, Ashiraph Alphonce alisema wameanza
kuzungukia maeneo yote kuorodhesha nyumba zoye zilizobomoka na zile
zenye nyufa.
“Tunapita kwenye mtaa wangu kuona nyumba zilizoanguka, mpaka leo (jana) nimehakiki kaya 58.
“Naiomba
Serikali ilete msaada wa haraka kwa wananchi kwa sababu hadi sasa
hakuna msaada wowote, wananchi wanaangaika wenyewe, tunaomba angalau
wapatiwe mahema wapate pa kuishi,” alisema Alphonce.
DC
Akijibu
malalamiko ya wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus
Kinawiro, amewataka wawe watulivu wakati huu ambao Serikali inaendelea
na kazi ya kuhakiki ili wapate msaada haraka iwezekanavyo.
“Nimeunda
kamati ya kufuatilia wananchi walioathirika wale walengwa kabisa, mpaka
sasa kwenye wilaya yangu kuna watu kama 3,000 hawana makazi,” alisema.
RC KIJIU
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Salum Kijuu alisema mpaka jana mchana
hakuna vifo vilivyoongezeka ingawa majeruhi waliokuwa wamelazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamepungua kutoka 253 hadi 61.
Alisema hakuna upungufu wa dawa na vifaa tiba vingine vinavyohitajika na huduma inaendelea kutolewa.
Chanzo: Gazeti Mtanzania
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment