SERIKALI imetakiwa kuwatia moyo wawekezaji binafsi katika vituo na
shule za michezo kwa kutoa msamaha wa kodi na ushuru wa vifaa
vinavyohusu michezo mashuleni na katika vituo vinavyokuza maendeleo ya
michezo.
Hilo ni moja ya pendekezo lililowasilishwa Serikalini na wadau wa
michezo mbalimbali waliokutana hivi karibuni mjini Kibaha, Pwani,
kujadili kushuka kwa maendeleo ya michezo nchini.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi,
alisema tayari wamewasilisha mapendekezo kadhaa Serikalini
yatakayoingizwa katika sera mpya ya michezo.
Alisema wadau wamependekeza kuwa kutokana na shule, vyuo na vituo vya
michezo nchini kutotumika kikamilifu kuchangia ukuaji wa michezo na
uwezo wa kushinda katika michezo ya mashindano, ni wakati mwafaka wa
kufanya uamuzi wa kuvitumia.
“Vyuo vya mafunzo ya walimu wa michezo kama vile Malya na Butimba,
vipewe jukumu la msingi la kimkakati la kuzalisha walimu wa michezo
mashuleni na katika vilabu vya michezo, viboreshwe ikiwezekana viongezwe
na kupangwa kwa kanda,” alisema.
Alisema wadau pia wameishauri Serikali ihamasishe
kuwepo kwa somo la elimu ya masoko katika michezo (Sports Marketing),
kwenye vyuo vya michezo.
“Timu na vyama vyetu vya michezo havijaweza kufanikiwa kutumia masoko
katika michezo kwa faida inayostahili, hii inatokana na uelewa na
utaalamu mdogo katika nyanja za masoko katika michezo, Tanzania inayo
wataalamu wachache sana katika eneo la masoko katika michezo.
“Kama nchi tunaweza kufanikiwa kuifikisha michezo kwenye manufaa
makubwa bila kutegemea fedha za Serikali endapo tutawekeza kuwa na
wataalamu na kuwatumia wataalamu wa masoko katika michezo,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment