Serikali
imeagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuondoa matuta kwenye
barabara kuu, ambayo yametajwa kuwa chanzo cha ajali.
Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, ametoa agizo hilo jana wakati wa
ufunguzi wa Wiki ya Usalama Barabarani katika Viwanja vya Kalangalala
mkoani Geita.
Alisema matuta yaliyoko kwenye barabara kuu, yamekuwa
moja ya vyanzo vya ajali nyingi nchini na kusisitiza kuwa hali ya ajali
iliyopo ni vyema suala la usalama barabarani kuwa ajenda ya kitaifa.
Pia
alivitaka vvyombo vya usalama, kuwachukulia hatua kali na stahiki wale
wote wanavunja sheria za Usalama Barabarani bila kumuogopa au kumuonea
mtu yeyote.
Alisema ajali za barabarani zimekuwa ni tatizo kubwa na
kuwa takwimu za miaka mitatu kuanzia Januari 2013 hadi Desemba 2015,
zinaonesha kuwa ajali zilizotolewa taarifa ni 46,536 ambazo zimeua watu
11,230.
Masauni alisema kuwa kundi linaloongoza kwa kuathirika na
ajali hizo ni abiria ambapo watu 3,444 wamekufa, wakifuatiwa na watembea
kwa miguu 3,328.
Alisema wapanda baiskeli wanashika nafasi ya tatu
kwa watu 2,493 kupoteza maisha, huku madereva waliokufa ni 813 na
wasukuma mikokoteni zaidi ya 400 wamepoteza maisha.
“Takwimu za miezi
sita tangu Januari mpaka Agosti mwaka huu, ajali 6,971 zimetokea na
kusababisha vifo 2,217 na kati ya hivyo 1,809 ni vile vilivyotokana na
pikipiki. Hali ya ajali sio nzuri na ni vyema suala la usalama
barabarani likawa ajenda ya kitaifa,” alisema.
Alisisitiza kutolewa
elimu ya watumiaji wote kuhusu matumizi sahihi ya barabara, wamiliki na
madereva kuacha kuendesha vyombo chakavu na kufanyika kwa ukaguzi wa
mara kwa mara.
“Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pia linatakiwa kuendelea kufanya ukaguzi wa matairi, bodi na vipuri vya mabasi,” alisema.
Aidha,
Masauni aliwataka watumiaji wote wa barabara, kufuata sheria na kanuni
za barabarani, kuacha kushabikia mwendo kasi, kuvuka kwenye vivuko vya
watembea kwa miguu na waendesha baiskeli na mikokoteni kuacha kuendesha
barabarani na watoto kuvuka barabara wakiwa chini ya uangalizi.
Naibu
Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ambaye pia ni
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Edwin
Ngonyani, alisema kutokana na kukithiri kwa ajali, Baraza lilikuja na
mikakati ya miezi sita ya kupunguza ajali hususan zinazotokana na makosa
ya kibinadamu.
Alisema makosa ya kibinadamu yamekuwa yakichangia
ajali kwa asilimia 80 na kufuatiwa na mwendokasi ambao unachangia kwa
asilimia 12, mazingira ya barabara yanachangia kwa asilimia 6 na
asilimia 2 zinatokana na sababu nyingine.
“Tumekuja na mikakati
ambayo inatekelezwa kwa miezi sita, lengo kuu ni kuondoa makosa ya
kibinadamu yanayochangia ajali, na Februari mwakani tutatathmini
mafanikio ya mikakati hiyo,” alisema.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani katika Jeshi la Polisi, Mohammed Mpinga, ambaye pia ni Katibu
Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, alisema katika Wiki
ya maadhimisho hayo watoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara, na kutoa
elimu kwa waendesha pikipiki 300 na walimu 100, na pia watakagua vyombo
vya moto na kupima afya za madereva kwa kutumia zahanati mwendo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment