WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu ameonesha hofu kutokana na kukithiri kwa mimba za utotoni na
kusema serikali itaweka mikakati ya kupambana nazo kutokana na kuathiri
maisha ya wasichana kuanzia miaka 14 hadi 17 ambao wengi wapo hatarini
kupata Virusi Vya Ukimwi.
Ameyasema hayo jana mjini Dodoma wakati anafunga mafunzo ya
wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi
Tanzania wa Mwaka 2016, yaliyokuwa yakifanyika katika Hospitali ya
Benjamin Mkapa iliyopo Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM).
Amesema serikali itakuja na mkakati ili kulinda maisha ya watoto wa
kike, ambayo yamekuwa yakiathiriwa na mimba za utotoni ili kufanikisha
jitihada za serikali katika kupambana na umasikini.
“Kiashiria kikubwa ambacho wizara yangu iko katika kuweka mikakati ya kupambana nacho ni mimba za utotoni,” amesema Waziri Ummy.
Amesema takwimu za mwaka 2012 zinaonesha kwamba robo ya wasichana
wote nchini wenye mri wa miaka 14 na 17, tayari walikuwa wameshajifungua
angalau mara moja. Aliitaja mikoa inayoongoza kwa tatizo hilo kuwa ni
Rukwa kwa asilimia 24.5 na Katavi kwa asilimia 27.6.
“Tunajua tatizo la mimba za utotoni ikiwa ni pamoja na uwezekano wa
maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na matatizo mengine ya kiafya,” amesema
na kuongeza,
“Tusipowazungumzia wasichana hakuna maendeleo kwao watapata mimba
watabaki mitaani hawataweza kuajiriwa au kujiajiri na hawataweza kulisha
watoto wao.”
Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mara nyingine inafanya
utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi na utafiti wa mwaka huu
utahusisha watu wote kuanzia watoto wadogo hadi wenye umri wa miaka 50
na kuendelea, wakati tafiti tatu zilizotangulia zimekuwa ziwahusisha
wananchi wenye umri kati ya miaka 15 na 49.
Amesema tofauti na tafiti zilizotangulia, utafiti wa mwaka huu ni wa
kipekee kwani kwa mara ya kwanza unahusisha wananchi wa rika zote katika
kaya zilizochaguliwa.
Amesema pia ni utafiti wa kwanza kukusanya taarifa zinazohusu
maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), kiasi cha VVU mwili kwa watu
wanaoishi na VVU na kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wa rika zote,
wingi wa chembechembe za kinga mwilini.
Amesema katika tafiti zilizopita kiwango cha maambukizi ya VVU
kimeonekana kupungua kutoka asilimia saba mwaka 2003 mpaka asilimia 5.1
mwaka 2011.
Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema utafiti huo ni wa
aina yake kufanyika nchini ingawa umewahi kufanyika utafiti unaofanana
na huo.
Alisema taarifa zinazokusanywa katika kila kaya ni siri na hakuna
mdadisi yoyote atakayeruhswa kutoa siri ya mtu yeyote hadi
yatakapofanyiwa uchambuzi wa kina na kutoa matokeo ya jumla ya hali
halisi ya maambukizi ya Ukimwi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, Leonard Maboko
alisema ukusanyaji sahihi wa takwimu unaweza kusaidia taifa kufahamu
idadi ya waathirika na kwa kiwango gani.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment