Dodoma. Serikali imetangaza kuanza utafiti kujua viashiria na matokeo ya Ukimwi katika ngazi ya kaya utakaofanyika mwezi ujao.
Utafiti
huo utakaofanyika nchini kote, una lengo la kuiwezesha Serikali kupanga
mipango endelevu ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.
Akizungumza
mjini hapa jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu ambaye alisema utafiti huo utahusisha kaya 16,000
kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy, matokeo ya utafiti huo yataeleza hali halisi ya maambukizi ya VVU ilivyo nchini.
Waziri
huyo alikuwa akifunga mafunzo ya wasimamizi na wadadisi wa utafiti wa
viashiria na matokeo ya Ukimwi Tanzania, yaliyofanyika katika Hospitali
ya Benjamin Mkapa mjini hapa.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kipindi chote cha utafiti ili kufanikisha mpango huo.
Mafunzo
hayo yaliyodumu kwa siku 49, yalihusisha jumla ya wauguzi 187 kutoka
mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani na kusimamiwa na Ofisi ya Taifa
ya Takwimu.
Waziri
Ummy aliwaomba wakuu wa kaya zitakazohusika katika utafiti kutoa
ushirikiano ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango endelevu ya
kupambana na Ukimwi nchini.
Alisema
taarifa zote zitakazotolewa na kukusanywa katika utafiti huo zitabaki
kuwa siri kwa kuwa wadadisi watakaoifanya kazi hiyo wamekula kiapo cha
maadili cha kutunza siri.
Mkurugenzi
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa alisema lengo la utafiti
huo ni kutathmini ukubwa wa tatizo la Ukimwi nchini, kiwango cha
utumiaji wa huduma za kujikinga na maambukizi, tiba kwa waathirika
pamoja na huduma zinazoendana na mapambano ya Ukimwi.
“Pia,
utafiti huu utajikita katika kubaini kiwango cha maambukizi mapya
katika ngazi ya kitaifa, CD4, homa ya ini pamoja na huduma nyingine
zinazohusiana na Ukimwi ikiwamo kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto,” alisema Dk Chuwa.
Mkurugenzi
wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Leonard Maboko,
aliwataka wadadisi hao kuwa waadilifu wakati wa kukusanya taarifa.
0 comments:
Post a Comment