LIGI Kuu Tanzania bara inaendelea leo kwa nyasi za viwanja vitatu
kuwaka moto huku vigogo vya soka Simba na Yanga vikishuka dimbani kusaka
pointi tatu muhimu.
Mchezo wa Yanga na Ndanda unaopigwa katika dimba la Nangwanda Sijaona
unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na kila timu kutaka kutunza
rekodi yake ambapo Yanga wanaingia uwanjani kwa lengo moja tu kusaka
pointi tatu zitakazowapa faida ya kutetea ubingwa wao wakati Ndanda
inatunza heshima ya kutofungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Ndanda imepanda daraja msimu wa mwaka 2014/2015, na kusalia kucheza
kwa mara ya tatu ligi msimu huu huku rekodi ikionesha kuwa wameshatoka
sare ya bila kufungana mara mbili na Yanga, kunyukwa mara moja na
kuinyuka Yanga bao 1-0.
Yanga iliyokuwa inakabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho,
inashuka dimbani kucheza mechi ya pili baada ya ile dhidi ya African
Lyon iliyoshinda mabao 3-0 ikiwa nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi
Kuu na pointi zake tatu.
Ndanda imeshacheza mechi mbili inashika nafasi ya 15 katika msimamo
wa ligi ikiwa imepoteza mechi zote za ugenini. Kwa upande wa Yanga,
wachezaji wake waliotemwa kwa madai kuwa walishuka kiwango leo wataivaa
timu yao hiyo ya zamani wakiwa Ndanda.
Wachezaji hao ni Kiggi Makasi, Jackson Chove na Salum Telela. Aidha
katika mechi ya leo, Yanga itawakosa nyota wake sita kutokana na sababu
mbalimbali, hao ni Deogratius Munishi, Geofrey Mwashiuya, Pato Ngonyani,
Haruna Niyonzima na Vicent Bosou.
Mechi nyingine leo itakuwa ni kati ya Simba ikiikaribisha Ruvu
Shooting kwenye Uwanja wa Uhuru maarufu ‘Shamba la Bibi’ ukiwa ni mchezo
wa kwanza kupigwa kwenye uwanja huo baada ya kufungwa kwa zaidi ya
mwaka mmoja ukifanyiwa matengenezo.
Simba imejipanga kutembeza kichapo kwa maafande wa Ruvu Shooting,
baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na maafande wa JKT Ruvu
katika mechi yake ya pili.
Kocha msaidizi wa wekundu hao Jackson Mayanja aliiambia HabariLeo
kuwa wamefanya marekebisho kwenye baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza
katika mechi ilizopita ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zao
zijazo.
“Tumejipanga vizuri kwenye mchezo wetu dhidi ya Ruvu tumeyafanyia
kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi zetu ili kuhakikisha
tunaondoka na pointi zote tatu,” alisema Mayanja. Nayo Azam itakuwa
mgeni wa Prisons kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment