KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imetoa ofa ya mwezi moja kwa abiria
wanaosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kulipa nauli ya Sh
160,000 kwa safari moja.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Ofisa
Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Lily Fungamtama wakati akizungumza na Idara
ya Habari (MAELEZO).
Fungamtama alisema ndege za kampuni hiyo, zimeanza kutoa huduma
kuanzia Jumamosi iliyopita, kama ilivyobainisha kupitia vyombo vya
habari.
Safari hizo zilianza kwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria kuelekea
nchini Comoro, na hapa nchini inatoa safari katika mikoa ya Mwanza,
Arusha na Kigoma.
Alisema kwa kuanzia walianza na mazoezi ya vitendo kwa marubani na
wafanyakazi wa ndani ya ndege, na hatimaye walianza safari za biashara
ya kusafirisha abiria Oktoba 15, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Aliongeza kuwa ATCL imeboresha huduma zake kwa kiasi kikubwa kwa
kuwapatia wateja wake ofa ya kubeba kilo 20 za mizigo na kilo saba za
mzigo wa mkononi bure pamoja na kutoa vinywaji na ubadilishaji wa tiketi
ni bure ndani ya mwezi.
Alikanusha taarifa potofu kuwa zimekwama kuanza safari zilizopangwa.
Alisema habari hizo sio za kweli, kwani hivi sasa wameshaanza huduma
katika mikoa hiyo mitatu.
ATCL kwa sasa ina ndege tatu, zikiwemo mbili aina ya Bombadier
Dash8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, na Dash8-Q300
yenye uwezo wa kubeba abiria 50.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment