Veronica Romwald Na Harieth Faustine -DAR ES SALAAM
HATUA ya wafadhili wa miradi ya afya nchini kufunga miradi yao kuna
hatari ya kuadimika kwa mipira ya kiume (kondomu) pamoja na dawa za
kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV’s).
Kitendo hicho kinaonekana huenda kikaigharibu Serikali hasa baada ya
kutangaza mapambano na baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikisambaza
vilainishi kwa lengo la kuzuia maambukizi ya Ukimwi hali iliyotafsiriwa
kwamba inakwenda kinyume na haki za binadamu kwa kuingilia kazi za NGO.
Taarifa iliyotolewa juzi kwa umma na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
la Tanzania Markenting and Communications (T-Marc Tanzania), Diana
Kisaka ilieleza kufungwa kwa mradi huo ambao ulikuwa unafadhiliwa na
Shirika la Kimataifa la Msaada la Marekani (USAID).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa shirika hilo lilikuwa likifanya kazi ya
kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na maendeleo nchini ambapo kazi
hiyo walikuwa wakifanya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa lengo la kuhakikisha zinapatikana
bidahaa bora za afya nchini.
“Bidhaa zinazosambazwa na T-Marc ni pamoja na miradi tunayoiendesha
nchini ambayo ni kuboresha afya ya uzazi ya mama na mtoto, lishe bora,
kupunguza maambukizi ya magonjwa hatari kama ukimwi na malaria.
“Mbali na hilo pia tulikuwa tunahamasisha upatikanaji wa matumizi ya
maji safi na salama, saratani ya mlango wa kizazi na utoaji elimuya
hedhi pamoja na vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi kwa wasichana,”
ilieza taarifa hiyo
Mkurugenzi huyo katika taarifa yake alisema kuwa wamekuwa
wakitekeleza mradi wa Tanzania Social Marketing (TSMP) kwa kushirikiana
na Population Services Internation (PSI) na kufadhiliwa na Shirika la
Msaada la Marekani (USAID) kwa kipindi cha miaka sita toka 2010 hadi
2016.
Novemba mwaka jana shirika hilo lilizindua aina mbili mpya za mipira
ya kiume aina ya Dume Extreme na Dume kama njia ya kupunguza utegemezi
ya ruzuku kutoka kwa wafadhili katika shughuli za wasambazaji wa mipira
hiyo.
“Lengo la tangazo hili ni kutoa taarifa ya kufungwa kwa mradi wa TSMP
ifikapo Desemba 31, mwaka huu na T-Marc itakamilisha malipo yote
yanayohusiana na mradi huu. Hivyo taasisi, watu binafsi wanaombwa
kuwasilisha Ankara za madai pamoja na nyaraka muhimu kabla ya tarehe
tajwa,” ilieleza taarifa hiyo.
Hatua hiyo huenda ikazidi kuitikisa sekta ya afya baada ya muda wa
miradi mikubwa iliyokuwa inatekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la USAID
kufika mwisho.
Akizungumza na MTANZANIA jana kuhusu hali hiyo Msemaji wa Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Nsachris Mwamwaja
alisema hana taarifa za kufungwa kwa mradi huo na kuahidi kuzungumzia
suala hilo hii leo.
“Sina taarifa za kufungwa kwa mradi, ndiyo kwanza unaniambia hizo
taarifa, bahati mbaya umenipigia saa hizi nimeshatoka ofisini najua
tarifa hizo kesho (leo) zitatoka, nipigie kesho mapema nitazungumza,”
alisema.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubsya alisema. “Wadau hawa
walikuwa katika miradi ambayo ilikuwa chini ya USAID katika kupambana
na malaria na mfumo wa utoaji na usambazaji wa dawa za kupambana na
Ukimwi kupitia mradi wake wa SCMS.
Miradi hiyo mikubwa ni pamoja na ile ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba
na misaada ya ufundi katika sekta hiyo, utoaji wa elimu kwa wanazuoni,
usambazaji na usimamizi wa vifaa vya tiba kwa miaka 10 iliyopita.
“Walikuwa wanatoa huduma hizo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za
afya nchini ikiwamo Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na
Bohari Kuu ya Dawa (MSD),” alisema.
Dk. Ulisubsya alisema miradi hiyo imesaidia kuongeza idadi ya watu
wanaotumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (Arv’s) kutoka watu
150,000 miaka 10 iliyopita hadi kufikia watu 800,000 hivi sasa,”
alisema.
Katibu mkuu huyo aliweka wazi kuwa wadau kama hao wanapoondoka nchini
baada ya muda wao wa kusimamia miradi kuisha, miradi hiyo hutetereka
katika uendeshaji na hata kufa.
Hatua ya kuondoka kwa wafadhili hao zinaweza kuwa pigo kubwa kwa
katika sekta ya afya nchini kutokana na miradi hiyo kutegemea wafadhili
wa nje kwa asilimia 90 huku Marekani ikiwa kinara wa ufadhili huo.
Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa baadhi ya miradi ambayo wafadhili waliwahi kujitoa, imedorora au imekufa.
Miradi hiyo ni pamoja na Mpango wa Taifa wa Damu Salama ambao awali
ulikuwa ukifanya vizuri, lakini hivi sasa umetetereka baada ya wadau
kujitoa na kuukabidhi kwa Serikali.
Hivi karibuni, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ilisimamisha ghafla
matibabu ya bure kwa wagonjwa wa seli mundu (sickle cell) ambao
walikuwa wakitibiwa kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia
Shirika la Welcome Trust.
Shirika hilo lilifadhili matibabu hayo kwa miaka 10 na ulikuwa
ukisimamiwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) tangu
mwaka 2004 na ulihitimishwa Machi, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, ofisini kwake,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alizitaka taasisi zisizo za kiserikali na asasi za kiraia
kuendelea kutoa huduma za afya kwa makundi maalumu, lakini si kusambaza
vilainishi.
Tamko hilo linakuja zikiwa zimepita siku chache baada Waziri wa
Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe kupiga marufuku vitendo vya
ushoga, kwani ni kinyume na sheria za nchi.
Alisema katika utoaji wa huduma kwa makundi maalumu kwa wenye maambukizi
ya virusi vya Ukimwi, maambukizi yameshuka na kufikia asilimia 5.1
ambapo awali ilikuwa asilimia 7.2 .
“Kumekuwa na baadhi ya taasisi na asasi ambazo zinachapisha
vipeperushi, matangazo na kusambaza vilainishi ili kuchochea ushoga na
ndoa za jinsia moja.
“Makundi yanayoathirika zaidi na maambukizi ya VVU ni wavulana,
wasichana walio katika umri wa kubalehe, yatima, wafungwa, wakimbizi,
madereva wa magari makubwa na wafanyakazi wa mashambani,” alisema.
Alisema katika watu 1000 watu 51 kati yao wanaishi na maambukizi na vijana wenye miaka 15-24 wana asilimia 35 ya maambukizi.
Alisema wasichana wanaofanya ngono wanapata maambukizi kwa asilimia
26 huku wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya ni asilimia 36.
“Wadau watakuwa wakipangiwa maeneo ya kutolea huduma za afya na
mganga mkuu kulingana na maambukizi, si kuchagua wenyewe kama ilivyokuwa
hapo awali ambapo mtu anatoa huduma sehemu moja tu” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment