Na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM.
WAZIRI Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ametoa tathmini ya mwaka mmoja
tangu ulipofanyika Uchaguzi Mkuu, huku akisema maisha yamezidi kuwa
magumu.
Lowassa ambaye alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072,848,
alitoa tathmini hiyo jana Oktoba 25 siku ambayo mwaka jana zaidi ya watu
milioni 23 walipiga kura ya kuchagua Rais, wabunge na madiwani.
Katika uchaguzi huo Rais Dk. John Magufuli alitangazwa mshindi na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kupata kura 8,882,935 sawa na
asilimia 58.46
“Pamoja na mafanikio machache katika baadhi ya maeneo maisha yamezidi
kuwa magumu na ajira imeendelea kuwa bomu linalosubiri kulipuka na
kwamba elimu bure iliyoahidiwa siyo inayotekelezwa huku utumishi wa
umma umekuwa kaa la moto,” alisema Lowassa.
Alisema anasononeka kuona viongozi wanavyoshindana kuwasweka ndani
madiwani na viongozi wengine wa kuchaguliwa hasa wanaotokana na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wabnanchi (UKAWA).
Akizungumzia kuhusu siku hiyo Lowassa alisema ilikuwa siku muhimu kwa Watanzania na kwake binafsi.
“Tarehe kama ya leo (jana) mwaka jana, ilikuwa siku muhimu sana kwa
Watanzania na kwangu binafsi. Niliwaongoza Watanzania kupiga kura
nikiwa mgombea wa upinzani.
“Naamini nilileta sura na msisimko mpya katika siasa za Tanzania.
Nilishirikiana na wenzangu kuionesha nchi yetu demokrasia maana yake ni
nini,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Ninapogeuka nyuma kuingalia siku ile, nasikia faraja kubwa sana hasa
kwa jinsi Watanzania walivyotuunga mkono na kuonesha matumaini makubwa
kwetu. Ujasiri na ushapavu wa hali ya juu aliouonesha mke wangu Regina
(Regina Lowassa) wakati wa kampeni, ulinipa nguvu kubwa.
“Chini ya Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe,tuliendesha kampeni za
kiungwana kama tulivyoahidi. Upepo ule ulivuma kwa kasi mpaka visiwani
ambako Maalim Seif (Aliyekuwa mgombea urais Zanzibar kupitia Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Sharif Hamad) aliporwa dhahiri ushindi,” alisema
Lowassa.
“Kwa mujibu wa Tume isiyo huru ya uchaguzi, tulishindwa uchaguzi ule.
Hatutaki kuendelea kuyalilia maziwa yaliyokwisha mwagika ambayo
hayazoleki, lakini kile ambacho tulikisema wakati ule kwanini tunataka
mabadiliko, hivi sasa kila mtu anakiona,” alisema.
Lowassa alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa imani waliyomwonyesha yeye pamoja na Ukawa.
“Kumalizika kwa uchaguzi ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwengine, kwa hiyo
mapambano ndiyo kwanza yameanza. Kasi, nguvu, ari na hamasa niliyonayo
ni kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” alisisitiza Lowassa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment