TIMU ya soka ya Mbeya City imetoa onyo kwa Simba kuwa hawatatoka
salama kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kesho, kwani wamejipanga
kuifunga na kubakiza pointi tatu.
Msemaji wa Mbeya City, Dismas Ten aliliambia gazeti hili jana kuwa
Simba isitegemee kushinda kwa urahisi kama ilivyofanya katika mechi zake
zilizopita kwani hata wao wamejipanga na wanahitaji ushindi. Alisema
wanaifahamu ni timu nzuri na wanawaheshimu, lakini ubora wao
hauwaogopeshi katika kujituma na kupata ushindi.
“Simba wajiandae vya kutosha kwa sababu tumedhamiria kufunga magoli
mengi, tunajua tabia zao wanapofungwa, lazima wakae,” alisema.
Ten alisema kinachohitajika ni waamuzi wachezeshe mchezo kwa kufuata
sheria 17, ili mashabiki wapate burudani na kufurahia ushindi kwa timu
yao.
Timu hiyo inajivunia kufikisha pointi 12 katika michezo minane
iliyocheza hadi sasa ikishika nafasi ya nne, kwenye msimamo wa ligi.
Kwa upande wa Simba, huo utakuwa ni mchezo wake wa kwanza nje ya mkoa
wake, ikitarajiwa kuendelea ushindi walioanza nao tangu kuanza kwa
msimu na kutesa kileleni kwa pointi 17 katika michezo saba iliyocheza.
Msemaji huyo wa Mbeya City alisema wachezaji wake waliokuwa majeruhi
Haruna Shamte na Sankhani Mkandawile wameanza mazoezi tayari kuivaa
Simba kesho.
“Shamte na Mkandawile wamekuwa sehemu ya kikosi kilichofanya mazoezi
jana hii ni tafsiri kuwa kikosi chetu kimetimia, Simba ni timu ambayo
tunaijua, hatuna shaka nao mara kadhaa wamekuja hapa wakapata kipigo,
tunafahamu wamekuwa na mwanzo mzuri wa msimu lakini kucheza na City ni
jambo tofauti inawalazimu kujipanga sana, waje nasisi tupo tayari,”
alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment