OFISI ya Msajili wa Vyama ya Siasa imetoa orodha ya vyama vya siasa
vyenye usajili wa kudumu na viongozi wa vyama hivyo ambako inasisitiza
kuwa Profesa Ibrahim Lipumba ndiye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF) na Katibu Mkuu ni Seif Shariff Hamad.
Kwa mujibu wa barua hiyo ya Oktoba 4, 2016 iliyoandikwa kwenda kwa
makatibu wakuu wa vyama vyenye usajili wa kudumu, Profesa Lipumba ambaye
Baraza Kuu la chama hicho limetangaza kumfukuza uanachama, anaonekana
kwenye orodha hiyo kama Mwenyekiti wa CUF.
Jina la Profesa Lipumba ambaye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo mwaka
jana, limerejeshwa kwenye orodha na Msajili wa Vyama ya Siasa baada ya
yeye mwenyewe kutangaza kutengua barua yake ya kujiuzulu.
Kwa hatua hiyo ya Msajili, uteuzi wa Julius Mtatiro ambao umefanywa
na Baraza Kuu kuongoza Kamati ya Uongozi ya CUF hautambuliwi na Ofisi ya
Msajili wa Vyama ya Siasa.
Uamuzi huo wa Ofisi ya Msajili umekuwa unalalamikiwa na upande
unaoongozwa na Maalim Seif kuwa unakiuka Katiba ya CUF wakati yeye
akisisitiza kuwa yuko sahihi kumtambua Profesa Lipumba kwa mujibu wa
Katiba hiyo.
"Baada ya zoezi la uhakiki na utekelezaji wa masharti ya usajili na
matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa kwa vyama vyenye usajili wa
kudumu kukamilika, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imehuisha
taarifa za vyama vya siasa zilizopo katika orodha ya vyama vya siasa.
"Hivyo pamoja na barua hii, nawasilisha orodha ya vyama ya siasa
ilivyo leo tarehe 4 Oktoba 2016 kwa taarifa na kumbukumbu zenu. Endapo
kuna taarifa ambayo siyo sahihi mnaombwa kuwasiliana na ofisi ya msajili
wa vyama ya siasa mapema iwezekanavyo ili irekebishwe," ilisema barua
hiyo.
Barua hiyo imevitaja vyama 22 ambayo vina usajili wa kudumu na chama
cha mwisho kusajiliwa ni Alliance for Change and Transparency
(ACT-Wazalendo) ambacho viongozi wake ni Anna Mghwira ambaye ni
Mwenyekiti na Katibu Mkuu ni Juma Sanani.
Chama hicho kilipata usajili Mei 5, 2014. Vyama vingine ni Chama Cha
Mapinduzi ambacho Mwenyekiti wake ni John Magufuli na Katibu Mkuu ni
Abdulrahman Kinana. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Mwenyekiti wake ni Freeman Mbowe na Katibu Mkuu ni Dk Vincent Mashinji.
Chama kingine ni Union for Multiparty Democracy (UMD) ambacho
Mwenyekiti wake ni Kamana Masoud na Katibu Mkuu ni Moshi Kigundula.
Chama cha National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi)
Mwenyekiti wake ni James Mbatia na nafasi ya katibu iko wazi.
Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD) bado
kinaonesha kuwani marehemu Oscar Makaidi na Katibu wake ni Tozy
Matwanga, United Peoples’ Democratic Party (UPDP) Mwenyekiti ni Fahmi
Dovutwa na Katibu Mkuu ni Hamadi Ibrahim, National Reconstruction
Alliance (NRA) Mwenyekiti ni Marsheed Humudi na Katibu Mkuu ni Simai
Abdullah.
Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA) kwa mujibu wa orodha hiyo
Mwenyekiti ni James Mapalala, Katibu Mkuu ni Mwaka Mgimwa, Chama cha
Democratic Party (DP) nafasi ya Mwenyekiti iko wazi na Katibu Mkuu ni
Georgia Mtikila. Chama hicho kilikuwa kinaongozwa na Mchungaji
Christopher Mtikila ambaye alifariki kwa ajali ya gari.
African Progressive Party of Tanzania (APPT-Maendeleo) kinaongozwa na
Mwenyekiti wake wa siku nyingi Peter Mziray, Katibu Mkuu ni Nziamwe
Samwel, Jahazi Asilia kinaongozwa na Kassim Bakari Ali na Katibu Mkuu ni
Mtumweni Jabir Seif, Sauti ya Umma (SAU) Mwenyekiti ni Paul Kyara na
Katibu Mkuu ni Ali Kaniki.
Tanzania Farmers Party (AFP) kinaongozwa na Said Soud Said na Katibu
Mkuu ni Rashid Ligania Rai, Chama cha Kijamii (CCK) Mwenyekiti wake ni
mwanahabari wa siku nyingi Constantine Akitanda na Katibu Mkuu ni
Renatus Muabhi, Alliance for Democratic Change (ADC) Mwenyekiti ni Hamad
Rashid Mohamed na Katibu Mkuu ni Doyo Hassan Doyo wakati Chama cha
Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kinaongozwa na Hashim Rungwe na Katibu Mkuu
ni Ali Omar Juma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment