WAKATI kasi ya uhakiki wa watumishi hewa ikiendelea, imebainika
baadhi ya taasisi za Serikali ikiwamo Jeshi la Polisi halijawalipa
mishahara askari wake wapya walioajiriwa Juni, 2016 kwa kipindi cha
miezi minne sasa.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata Dar es Salaam jana na
kuthibitishwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Mambo yaNdani ya Nchi, Christina Mwangosi, zinasema askari
wapya hawajalipwa mishahara kutokana na maandalizi ya mfumo mpya wa
malipo.
“Unajua kuna taratibu za malipo zinaendelea kufanyiwa kazi, hivi sasa
majina yao yanaingizwa kwenye mfumo wa malipo kutokana na uhakiki
unaondelea.
“Kuna baadhi yao hawajalipwa, lakini wizara inaendelea kuwaingiza
katika mfumo huo, tunaamini watalipwa pindi taratibu zote
zitakapokamilika,” alisema Christina.
Wakizungumza na gazeti hili, kwa sharti la kutotaja majina yao
gazetini, askari hao walisema wamekuwa wakiishi maisha magumu kutokana
Juni hadi sasa.
“Tangu tumehitimu mafunzo hatujawahi kulipwa mishahara yetu, tunaishi katika mazingira magumu.
“Hatuna fedha za kujikimu, kila mmoja wetu ana majukumu yake ambayo
anapaswa kuyatimiza kupitia malipo ya mshahara…tunaomba
tuangaliwe,”alisema mmoja wa askari huyo.
Lakini askari mmoja kutoka Idara ya Uhamiaji makao makuu, alisema
baada ya kumaliza mafunzo waliajiriwa, lakini nao hawajawahi kulipwa.
“Tulipotoka depo tulipewa likizo ya mwezi mmoja kusubiri kuingizwa
katika mfumo wa malipo, tuliporudi tumeendelea kufanya kazi bila kulipwa
mishahara jambo linalotufanya tuishi kwa shida,” alisema.
Alisema hawaelewi kwanini suala hilo linachukua muda mrefu kumalizika.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja
Jenerali Projest Rwegasira kuzungumzia suala hilo, alisema baada ya
askari hao kumaliza mafunzo majina yao yalipelekwa Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kuingizwa kwenye mfumo wa
malipo.
“Walivyotoka mafunzoni tuliwapokea na kupeleka majina yao Utumishi
kama bado hawajaanza kulipwa nakuomba waulizeni Utumishi ndiyo wenye
majibu sahihi,” alisema Meja jenerali Rwegasira.
Alipoulizwa Serikali kusitisha ajira mpya, Meja Jenerali Rwegasira alisema ajira za askari huanza pale wanapoingia mafunzoni.
“Unajua ajira za jeshi, si sawa na za raia wa kawaida kwa kuwa
wanapoanza mafunzo huingia moja kwa moja kazini, ndiyo sababu tumepeleka
majina yao huko,”alisema.
Alisema baada ya Serikali kusitisha ajira mpya,hata wao wamelazimika kusimamisha udahili wa askari wapya katika vyuo vyao.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alipoulizwa suala
hilo, alimtaka mwandishi awasiliane na Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean
Ndumbaro.
Juhudi za kumtafuta Dk. Ndumbaro, hazikufanikiwa kwa sababu yake ya kiganjani muda wote haikuwa hewani.
AGIZO
Juni 19, mwaka huu, Dk. Ndumbaro aliliambia gazeti hili kuwa Serikali
imesitisha ajira zote kama njia ya kukabiliana na wimbi la watumishi
hewa.
Alisema hakuna nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa Serikali na
wakala zake pamoja na utoaji wa vibali wa likizo ya bila malipo.
Alisema lengo kubwa ni kupitia upya muundo wa Serikali na taasisi zake.
Alisema utekelezaji wa mkakati huo, utakwenda sambamba na kusitisha
kwa muda utoaji wa vibali vya ajira zote mbadala pamoja na uidhinishaji
wa ajira hizo zilizopo Sekreterieti ya Ajira katika utumishi wa umma na
kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi.
“Ni kweli tumesitisha kwa muda ili kupitia mfumo wa Serikali na hata
kuangalia ulipaji wa mishahara kama upo katika malipo stahiki.
“…na hili litakwenda sambamba na hata kusitishwa malipo ya mishahara
yanayotokana na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi. Tukimaliza kazi hii
ndipo tunaweza kuanza kutoa ajira za Serikali,” alisema Dk. Ndumbaro.
Alisema muundo mpya wa utumishi wa Serikali unakwenda sambamba na
uhakiki wa malipo ya mishahara, hivyo ni lazima ijulikane ni nani
anayelipwa kuliko ilivyo sasa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment