Image
Image

Rais Dkt. Magufuli apokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi wa nchi mbalimbali ikulu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 10 Oktoba, 2016 amepokea hati za utambulisho za mabalozi wanne wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Balozi wa
Jamhuri ya Sudan hapa nchini Mhe. Mahjoub Ahmed Abd Allah Sharfi, Balozi wa  Jamhuri ya Slovakia hapa nchini Mhe. Frantisek Dlhopolcek, Balozi wa Ukraine hapa nchini Mhe. Yevheni Tsymbaliuk na Balozi wa Jamhuri ya Ghana Mhe. Kwame Asamoah Tenkorang.

Rais Magufuli amezungumza na Mabalozi hao kwa nyakati tofauti baada ya kupokea hati zao za utambulisho, ambapo wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo kwa kujikita zaidi katika biashara na uwekezaji.

"Mhe. Balozi najua nchi yenu ya Sudan ina utajiri wa mafuta na imefanikiwa kujenga uchumi wake kupitia mafuta, sisi pia hapa nchini tumebaini uwepo wa mafuta na gesi asilia katika maadhi ya maeneo, ningependa uhusiano na ushirikiano wetu sasa ujielekeza katika kubadilishana uzoefu na ujuzi wa namna tunavyoweza kunufaika na mafuta na gesi"  amesema Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa Sudani hapa nchini Mhe. Mahjoub Ahmed Abd Allah Sharfi.
Dkt. Magufuli pia ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi za Sudan, Slovakia, Ukraine na Ghana kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo Mafuta na gesi, Kilimo, Uvuvi, Mbuga za wanyama, Madini na ufugaji.
"Hivi sasa Tanzania ipo katika mpango wa ujenzi wa viwanda na pia tunatekeleza mpango wa pili wa maendeleo, hivyo nakuomba Mhe. Balozi uwahamasishe wafanyabiashara na wawekezaji wa Ukraine waje wawekeze katika viwanda kwani soko la uhakika la bidhaa lipo" amesisitiza Dkt. Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa Ukraine hapa nchini Mhe. Yevheni Tsymbaliuk.
Aidha, Rais Magufuli amewasihi Mabalozi wa Slovakia, Ukraine na Ghana ambao makazi yao ya
Ubalozi yapo Mjini Nairobi nchini Kenya kuanzisha Ubalozi wao hapa nchini ili kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano katika masuala ya biashara na uwekezaji.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Oktoba, 2016.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment