KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Sirro
amesema jeshi hilo limemkamata mtuhumiwa ‘Scopion’ aliyehusika katika
matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha eneo la Buguruni jijini humo.
Sirro alitoa kauli hiyo jana Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar es
Salaam wakati wa mkutano wa kujadili usalama katika eneo hilo
ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Alisema
mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina maarufu kama Scopion alikamatwa
baada ya polisi kupewa taarifa za matukio ambayo ameyafanya ikiwemo la
kumchoma kisu, kumtoa macho na kumsababishia upofu, Said Ally.
"Nimesikia wananchi wanalalamika hapa kuwa tumeshindwa kumkamata
Scopion, ni nani kwa Jeshi la Polisi asikamatwe, tayari tumemkamata na
sheria itachukua mkondo wake, hakuna mtu anayeweza kushindana na jeshi,"
alisema.
Aidha Sirro alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo na kuhojiwa
aliutaja mtandao wake wote na tayari wameukamata, hivyo amewataka wakazi
wa eneo hilo kutokuwa na hofu kwani mtuhumiwa huyo hayupo tena katika
eneo hilo.
"Najua suala hili bado lipo mahakamani hatuwezi kulizungumzia sana,
bahati nzuri alipokamatwa alieleza aliyoeleza na tukafanikiwa kuukamata
mtandao wote, hivyo hakuna haja ya kuwa na uwoga eneo hili lipo salama,"
alisema.
Kabla ya kauli hiyo ya Sirro, wananchi wamelalamikia askari wa eneo
hilo ambao walishindwa kuchukua hatua kwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa
akifahamika muda mrefu. Sadiki Mgaya ambaye alishuhudia tukio la
kuchomwa kisu na kutolewa macho kwa Said Ally, alisema mtuhumiwa huyo
alisema kuwa amekuja kwa ajili ya kulipa kisasi kwa wakabaji baada ya
yeye kukabwa.
Alisema baada ya kufanya tukio hilo, askari walifika katika eneo hilo
na mtuhumiwa huyo akiwa hapo na wananchi waliwaonesha askari lakini
hawakuchukua hatua zozote badala yake waliwataka wananchi wamkamate.
Aidha wananchi hao pia wamemlalamikia Mkuu wa Kituo cha Polisi
Mnyamani na kudai kuwa amekuwa akipelekewa taarifa za uhalifu ikiwemo za
vibaka lakini mtu anapokamatwa akifika kituoni hapo anatoa rushwa na
kuruhusiwa kuondoka.
Lakini akiondoka askari wengine wanatumwa tena kumkamata. Kauli hizo
za wananchi zikamfanya Sirro kutoa kauli ambapo alisema askari na
maofisa wote ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao watachukuliwa hatua
ikiwemo kufikishwa mahakamani pamoja na kufukuzwa kazi.
"Najua wapo askari na maofisa wa ovyo ambao hawajui kutimiza wajibu
wao, lakini nikuahidi Mkuu wa Mkoa tutawachukulia hatua, nimesikia hapa
wananchi wanalalamika askari wanachukua rushwa, tutachunguza
tukijiridhisha basi ni lazima tuchukue hatua," aliongeza.
Aidha Sirro alisema watafanya doria kubwa katika eneo hilo ili
kuwakamata wote wanaohusika na matukio ya kihalifu kwani wamebaini
katika eneo hilo bado kuna uporaji mdogo mdogo.
"Tutarudi hapa tunaomba ushirikiano wenu bila ninyi kutuambia
hatuwezi kujua, nawaomba wazazi muwakanye watoto wenu ambao wanahusika
na matukio hayo kwani tutakapoanza msako huo wasije wakalalamika,
uhalifu haulipi na mwisho wa siku utamkosa mtoto wako," alisisitiza.
Kwa upande wake Makonda aliwataka wananchi hao kujitolea kufanya
ulinzi shirikishi na kuwataka wananchi kuchangia ulinzi huo ili vijana
hao wahusike kufanya ulinzi na kulifanya eneo hilo libaki na amani.
"Tuna wajibu wa kufanya ulinzi shirikishi wananchi mtoe michango,
hapa Sirro amesema mapungufu yaliyopo kwenye vituo yanafanyiwa kazi,
niwaase tu mjiepushe na matukio ya kuhalifu kwani wale watakaokamatwa
sheria itachukua mkondo wake," alisema Makonda.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment