WATAFITI wawili na dereva mmoja wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha
Selian (SARI) jijini Arusha wameuawa na kisha miili yao kuchomwa moto
katika kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino katika mkoa wa Dodoma
wakati wakifanya utafiti wa udongo, baada ya kuhisiwa kuwa ni wanyonya
damu.
Waliouawa wametajwa kuwa ni Nicas Magazine aliyekuwa dereva wa gari
aina ya Toyota Hilux Double Cabin lenye namba za usajili STJ 9570 mali
ya Selian pamoja na watafiti wawili ambao ni Teddy Lumanga na Jaffari
Mafuru.
Polisi mkoani Dodoma inawashikilia wanakijiji 30 wa kijiji cha Iringa
Mvumi kuhusu mauaji hayo, huku Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana
akitoa amri ya kuwasimamisha kazi Ofisa Utumishi wa Wilaya hiyo na
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.
Mauaji hayo yalitokea juzi katika kijiji cha Iringa Mvumi, tarafa ya
Makang’wa wilayani Chamwino baada ya watu hao waliokuwamo katika gari
hilo kuvamiwa na wanakijiji wa Iringa Mvumi na kuwakatakata kwa mapanga
pamoja na silaha za jadi kisha kuwachoma moto hadi kufa. Inadaiwa chanzo
cha tukio hilo ni Cecilia Chimanga (34) kupiga yowe kijijini
kuwafahamisha kwamba ameona watu anaohisi ni wanyonya damu (mumiani).
Baada ya taarifa hizo kufika kijijini ndipo Mchungaji wa madhehebu ya
Kanisa la Christian Family, Patrick Mgonela (46) alikitangazia kijiji
kupitia kipaza sauti cha kanisani kuwa wamevamiwa na wanyonya damu ndipo
wanakijiji wakaenda kuchoma gari, kuwaua na kuwachoma moto.
Baada ya tukio hilo, msako ulifanyika kwa kujumuisha askari wa
kawaida na makachero na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na maofisa
wengine wa Polisi. Akizungumza na gazeti hili jana Kaimu Ofisa Tarafa ya
Makang’wa, George Mzuri alisema watafiti hao pamoja na dereva walifika
kijijini hapo kufanya shughuli zao, lakini hata hivyo hawakupitia
ofisini.
“Tunasikia walifika kijijini kwa ajili ya shughuli zao, lakini
hawakutoa taarifa kwenye Serikali ya Kijiji wakawa wanatafuta njia ya
kutokea wakafika mahali wakakuta akinamama wanaopika chumvi kwa njia ya
asili,” alidai Mzuri.
Alisema waliamua kumwita mmoja wa wanawake hao ili wamuulize njia,
lakini mama yule alikuwa akiogopa kwa kudhani kuwa walikuwa ni wanyonya
damu.
“Mara yule mama akaanza kupiga kelele, karibu na hapo walipokuwa kuna
kanisa ambalo likatumika kutangaza watu waelekee mbugani kuna wanyonya
damu,” alisema na baada ya wananchi hao kufika eneo la tukio walianza
kuwashambulia watu hao na kisha kuwaua na kuwachoma moto.
Alisema juhudi za kuwaokoa watu hao zilishindikana kutokana na wingi
wa watu. Akizungumza katika eneo la tukio, Rugimbana alisema wote
waliohusika na mauaji hayo watachukuliwa hatua za kisheria, wakati
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema mpaka sasa
watu 30 wanashikiliwa na Polisi wakiwemo wanaume 21 na wanawake tisa.
Jijini Arusha, Mratibu wa Utafiti wa Kituo cha Selian, Charles
Lyamchai alisema, “ni huzuni kwetu sisi wafanyakazi wa Kituo cha Utafiti
cha Selian Arusha mara baada ya kusikia vifo vya wafanyakazi wenzetu
waliochomwa moto jana (juzi) wakiwa wanaendelea kufanya utafiti wa
udongo huko mkoani Dodoma.
“Ukweli taarifa hizi zimetuumiza sana kwani wenzetu walikuwa
wakifanya utafiti kwenye vijiji mbalimbali ili kujua aina za udongo
unaofaa kwa ajili ya kilimo.”
Kwa mujibu wa Lyamchai, taarifa hizo zimewashtua wafanyakazi wa kituo
hicho kwani wenzao walikuwa kazini wakitekeleza majukumu yao ya kazi.
Alisema wiki mbili zilizopita wenzao walikuwa wakiendelea na kazi ya
kukusanya sampuli za udongo kwenye maeneo mbalimbali, lakini walipofika
kijiji hicho cha Iringa Mvumi wakiendelea na shughuli, ghafla walitokea
watu wasiojulikana na kuanza kupiga mayowe kisha kuanza kuchoma moto
gari la serikali pamoja na watumishi hao watatu.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Nicas Magazine ambaye alikuwa ni
dereva wa gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin yenye namba za usajili
STJ 9570 mali ya Selian, pamoja na watafiti wawili ambao ni Teddy
Lumanga pamoja na Jaffari Mafuru.
“Tumeumia na tukio hili, lakini ndio hivyo yameshatokea na baadhi ya
wenzetu wameshaondoka kwenda mkoani Dodoma ili kujua tunaanzia wapi na
kupanga taratibu za maziko, lakini tumeshtushwa na tukio hili kwa kweli
tumeumia sana,” alisema mratibu huyo wa Utafiti wa Selian.
Aliongeza kuwa kazi wanazofanya watafiti ni ngumu sasa hawajui kabla
ya kukutwa na mauti hayo wenzao walikumbana na nini. Imeandikwa na Sifa
Lubasi, Dodoma na Veronica Mheta, Arusha
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment