SIKU
moja baada ya gazeti la Nipashe kufichua namna kina mama wanavyotozwa
wastani wa Sh. 300,000 kwa ajili ya huduma ya uzazi katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili,
Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii, Ummy Mwalimu, ameitaka bodi ya hospitali
hiyo kueleza sababu za kuwalipisha kinyume na sera ya taifa ya afya. Jana
katika toleo la Nipashe lilichapisha habari iliyokuwa ikieleza namna
wanawake wajawazito wanavyotozwa fedha kwa ajili ya kujifungua. Akizungumza
na Nipashe jana kwa njia ya simu, Mwalimu alisema baada ya kusikia
taarifa hiyo, ameutafuta uongozi wa bodi ya hospitali hiyo kwa ajili ya
kutaka maelezo na sababu za kutoza fedha hizo. Alisema
utaratibu unaotumiwa na hospitali hiyo ni kinyume cha Sera ya Taifa ya
Afya ya mwaka 2007 inayosisitiza kuwa kina mama wajawazito ni lazima
wapate huduma hizo bure. Mwalimu
alisema suala hilo wamekuwa wakilisisitiza kila mara na wataendelea
kulisisitiza, ili kila hospitali ya umma itoe huduma bure kwa wanawake
walio kundi la msamaha. “Nimeongea
na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, nimemweleza
nataka kupata taarifa ya sababu za kutoza wanawake fedha kwa ajili ya
kujifungua kinyume cha sera ya afya ya uzazi ya mwaka 2007 na mwenyewe
ameniahidi atakaa na uongozi wa hospitali ili kunipa taarifa hiyo,”
alisema Mwalimu. “Bodi imeniahidi itakaa na uongozi wa hospitali ili kujadili kwa pamoja na kunipatia majibu ya hoja hii mara moja.” Alipoulizwa
kama serikali imepeleka fedha za kutosha katika hospitali za serikali
ili kusaidia utoaji wa huduma hizo bure, Waziri Mwalimu alisema
wanapeleka fedha kwa ajili ya huduma. Alisema mishahara ya wauguzi na madaktari inatoka serikalini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa makundi hayo maalumu.
“Kabla hujamalizia swali lako, naomba nikueleze kuwa madaktari
tunawalipa mishahara kwa fedha za serikali na dawa zinanunuliwa na
kusambazwa katika hospitali za serikali," alisema. "Lakini
pia serikali inahakikisha dawa zinapatikana katika hospitali zote za
serikali inakuwaje sasa hospitali inawatoza wanawake hizo fedha?” Pia alieleza serikali inapeleka fedha za kutoa huduma na uendeshaji wa hospitali za umma ili madaktari wawahudumie wananchi.
Alisema gharama wanazotozwa wagonjwa wa kundi la msamaha zinakuwa hazina
tofauti sana na zile za hospitali binafsi hali ambayo inampa wasiwasi. “Kama
wanatoza fedha hizo kwa ajili ya kutoa huduma kwa makundi maalumu na
siyo kwa wagonjwa wa private, inamaana fedha wanazopata ni nyingi ingawa
wamejitetea ni kwa ajili ya kuboresha huduma katika hospitali hiyo.” KUCHANGIA HUDUMA
Wakati wanawake waliojifungua katika hospitali hiyo wakilalamikia
kutozwa wastani wa Sh. 300,000, juzi Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya
Umma na Huduma kwa wateja wa Muhimbili, Aminieli Aligaesha alithibitisha
wanawake wanaokwenda kujifungua hospitalini hapo wanatozwa fedha hizo
kwa ajili ya kuchangia huduma. Kiasi alichokitaja ni Sh. 125,000 kwa wanawake wanaojifungua kawaida na Sh. 250,000 kwa wanawake wanaojifungua kwa upasuaji. Aidha,
Aligaesha alisema hospitali hiyo inatoza kundi hilo lililo nje ya
malipo kwa kuwa haina fedha za kutosha kutoa huduma. Alisema hawajapokea
fedha kutoka serikalini kwa miezi tisa. Wakati
serikali ikiendelea na kampeni yake ya kutoa huduma ya afya bure kwa
ajili ya makundi maalumu ya msamaha wakiwa kina mama wajawazito, wazee,
watoto chini ya miaka mitano na watu wenye maambukizi ya Ukimwi, mwaka
wa fedha wa 2016/17 serikali imetenga Sh. bilioni 251 kwa ajili ya sekta
hiyo. Kufikia
robo ya mwaka wa fedha katika utekelezaji wake, zimeshatolewa Sh.
bilioni 20 pekee badala ya bilioni 62.5 katika kipindi hicho iwapo fedha
hizo zingetolewa kwa uwiano sawa wa vipindi vinne vya mwaka. Hata hivyo utaratibu wa utoaji fedha si lazima kufuata mgawanyo sawa. Kwa
mujibu wa taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango, serikali inatoa Sh.
bilioni 68 kila mwaka kwa ajili ya mishahara ya watumishi 3,121 wa
Hospitali ya Muhimbili yenye makusanyo ya Sh. bilioni 4 kwa mwezi. Mishahara hiyo inagawanywa kwa madaktari bingwa 238, madaktari wa kawaida 173 na wauguzi 1,699. Kwa
mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wastani wa kipato cha
Mtanzania ni Sh. milioni 1.9 kwa mwaka sawa na kila mwezi Sh. 159,910. Gharama
hizo hazilingani au kuendana na gharama za huduma ya uzazi wanazotozwa
kina mama wanaopata huduma ya kujifungua katika Hospitali ya Muhimbili.
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 comments:
Post a Comment