Na ARODIA PETER-DAR ES SALAAM
NI ujambazi wa kutisha. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kuibuka
na wizi unaofanywa na majambazi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hatua hiyo inatokana na majambazi hao kuibuka na mbinu mpya kila
kukicha katika matukio mbalimbali ambayo sasa yamekuwa yakishika kasi.
Mbali na mbinu ya kutumia pikipiki, majambazi hayo pia huvamia
vibanda vya kutoa huduma za fedha, kuiba magari na hata wakati mwingine
kuua.
Katika hali iliyovuta hisia za watu wengi, juzi usiku majambazi
yalifunga mtaa kwa saa mbili na kupora fedha kwa watoa huduma ya fedha
kwa njia ya simu katika eneo la Tabata jijini Dar es Salaam.
Mbali na maduka, watu wengine waliokuwa nje nao pia waliporwa simu na
fedha. Hata hivyo thamani ya fedha na vitu vilivyoporwa havikujulikana
mara moja.
Tukio hilo lililoshtua wakazi wengi wa mitaa ya Kimanga na Kisukuru
wilayani Ilala, Dar es Salaam, ni la pili kutokea ndani ya kipindi cha
mwezi mmoja.
Awali mwezi uliopita, majambazi wenye silaha walimuua kwa risasi
askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na baadaye kumpora fedha
Sh milioni tano, nje ya geti la nyumbani kwake Mtaa wa Kimanga, saa tano
asubuhi.
Tukio la juzi lilitokea katika moja ya maduka yaliyoko pembezoni mwa
kituo cha daladala cha Jiandae kilichopo Tabata Kimanga, ambako
majambazi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya wanne yaliingia dukani na
kuwaamuru wafanyakazi kutoa fedha zote za mauzo ya siku, huku
wakiwatishia kwa mapanga na bastola.
Mmoja wa wafanyakazi wa kike katika maduka hayo alipoteza fahamu baada ya tukio hilo na alikimbizwa hospitali kwa matibabu.
Licha ya idadi kubwa ya watu katika eneo hilo lenye biashara
mbalimbali wakati wa jioni, majambazi hao hawakujali, walifanya uporaji
huo na baadaye kutokomea kwa kutumia pikipiki aina ya Boxer.
Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia MTANZANIA jana kuwa kwa muda wa
dakika tano hakuna gari iliyoruhusiwa kwenda au kutoka Kimanga.
“Majambazi waliwaamuru wenye magari kutokukatiza eneo hilo, huku waenda kwa miguu wakiamriwa kuondoka haraka.
“Katika hali ya kawaida ni vigumu kuamini kama majambazi wanaweza
kuvamia na kupora vitu katika maduka matatu kwa mpigo halafu wakatoweka
bila kukamatwa,” alisema shuhuda huyo aliyekataa kutajwa jina.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga, Manase Mjema, alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, alisema majambazi hao yalikuwa yamejiandaa na
yalitumia silaha kubwa.
“Awali kabla ya kufyatua risasi yaliwaamuru wafanyakazi wa maduka
yanayofanya biashara kupitia miamala ya simu kutoa fedha zote za mauzo,
vijana walikuwa ngangari kidogo, hivyo majambazi waliamua kupiga risasi
tatu hewani ndipo waliamua kutoa fedha walizokuwa nazo,” alisema.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alikiri kuwapo kwa ulinzi hafifu katika
mtaa wake, huku pia akishauri Jeshi la Polisi kuimarisha doria mitaani
kwa kuongeza askari wasiokuwa na sare ili wasitambulike kwa urahisi.
“Nikiri kwamba ulinzi wetu wa mtaa wakati wa usiku bado ni mdogo,
tunaomba polisi nao waangalie mbinu mbadala za kukabiliana na uhalifu,
na hasa ujambazi huu wa kutumia silaha za moto. Eneo la Tabata hivi sasa
limekumbwa na matukio mengi ya ujambazi, kwa hiyo lazima mbinu nazo
zibadilike,” alisema Mjema ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kimanga
(Chadema).
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya,
alikiri kupokea taarifa za ujambazi na tayari askari wake wameanza
uchunguzi ili kuwabaini wahalifu hao.
“Nitoe ombi na nisisitize wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa
Jeshi la Polisi ili kutokomeza vitendo vyote vya uhalifu. Viongozi wote
wa mitaa watupatie taarifa za watu wanaowatilia shaka, nasi tutazifanyia
kazi,” alisema Kamanda Mkondya.
Katika siku za hivi karibu kumeibuka matukio ya ujambazi katika
maeneo mbalimbali nchini huku wakiibua mbinu mpya za kufanikisha wizi
huo.
Kutokana na hali hiyo majambazi hao wamekuwa wakitumia pikipiki kwa
ajili ya kutekeleza uvamizi kwenye matukio hayo na hata wakati mwingine
kuua watu na kujeruhi.
Katika mfululizo wa matukio ya ujambazi jijini Dar es Salaam, Agosti
23, mwaka huu, askari wanne wa Jeshi la Polisi waliuawa baada ya
majambazi kuvamia Tawi la Benki ya CRDB lililopo Mbande, wilayani
Temeke.
Majambazi hao wanaokadiriwa kufikia 14, wakati askari hao
wakibadilishana lindo, waliibuka ghafla na kuanza kurusha risasi na
askari mmoja aliyekuwa lindo alifanikiwa kukimbia.
Kutokana na foleni katika barabara nyingi za Dar es Salaam pamoja na
miundombinu ya makazi yasiyokuwa rasmi, matukio mengi ya ujambazi
yanayoripotiwa ni ya kutumia pikipiki, hivyo kuwapa wakati mgumu polisi
ambao mara nyingi wanatumia magari ya doria.
Mapema mwaka huu Rais Dk. John Magufuli aliliagiza Jeshi la Polisi
kutumia mbinu za kisasa katika kukabiliana na uhalifu na kuifanya nchi
kuwa sehemu salama nyakati zote.
Dk Magufuli alionesha kushangazwa na askari wa Jeshi la Polisi
kunyang’anywa silaha yake na majambazi na wakati mwingine kuuliwa na
majambazi, akihoji uwezo wa majambazi kiasi cha kuwatesa polisi kiasi
hicho.
Rais alikuwa akizindua Mpango wa kuboresha usalama wa jamii na mali
zao, ambao una dhamira ya kupunguza uhalifu ambapo ameliagiza jeshi hilo
kuwahi kushughulikia majambazi kabla ya wenyewe kushughulikiwa na
majambazi hayo.
Pamoja na hali hiyo Jeshi la Polisi lilitangaza mikakati mbalimbali
ikiwamo ukaguzi maalumu wa bodaboda na kufunga kamera za CCTV katika
miji mikuu ili kufuatilia matukio mbalimbali.
Majambazi hao ambao kwa muda sasa wamekuwa wakiibuka na mbinu mpya
ikiwamo ya kutumia bodaboda kuvamia benki na wanaotoka benki na kuwapora
fedha.
Licha ya polisi kuweka ulinzi maalumu na waendesha bodaboda
watakaoonekana kupakia kitu chochote na kukiweka mbele (katika tenki la
mafuta) au kiti cha nyuma, ikiwemo kusimamishwa na kupekuliwa lakini
bado mbinu hiyo imekuwa ikifeli na watu wakijikuta wakidhurika.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara
ya wananchi kuvamiwa na kuporwa fedha, ikiwa ni muda mfupi baada ya
kuzichukua benki huku wafanyakazi wa benki wakidaiwa kuhusika kutoa
taarifa za wateja.
Mara zote majambazi hutumia bodaboda kufanikisha uhalifu huo, huku
wakiwa na silaha ambazo huzitumia kutishia, kujeruhi na wakati mwingine
kuua.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment