Image
Image

Utoaji mikopo vyuo vikuu uwajali watoto wa maskini



TAARIFA kwamba robo tatu ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini walioomba mikopo kwa ajili ya mwaka huu wa fedha watakosa fursa hiyo zinaibua wasiwasi kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wengi wasio na uwezo kiuchumi kupata fursa ya kuanza au kuendelea na masomo.
Serikali inasema kuwa imetoa zaidi ya Sh. bilioni 80 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini, lakini Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB),inasema kuwa haitakuwa na uwezo wa kuwapatia mikopo wanafunzi wote walioomba.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema kwamba kati ya wanafunzi 88,000 wa mwaka wa kwanza walioomba mikopo hiyo, ni 21,500 pekee ndio wamekidhi vigezo.
Kutokana na takwimu hizo, ni dhahiri kwamba wazazi na walezi wa wanafunzi 66,500 watalazimika kugharimia wenyewe elimu ya juu kwa watoto wao.
Ingawa mpaka sasa HESLB imetoa majina ya wanafunzi 3,966 ambao ni wanufaika wa kwanza wa mkopo kwa mwaka huu wa masomo, mwaka wa masomo uliopita, bodi ilitoa Sh. bilioni 459 kwa wanafunzi 122,486, kati yao 53,618 wakiwa wa mwaka wa kwanza na 68,916 waliokuwa wakiendelea na masomo.
Fedha hizo zilitolewa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa awamu zaidi ya nne. Awamu ya kwanza ilikuwa na wanafunzi 12,282 huku ya pili ikiwa na wanufaika 28,554.
Badru alisema wanafunzi watakaopata mikopo hiyo ni wale waliokidhi vigezo vipya vya mikopo vilivyotangazwa na serikali wiki iliyopita. Alisema wameanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea tangu Jumanne iliyopita.
Alisema HESLB inatoa mikopo hiyo kulingana na kalenda za vyuo husika na kwamba kwa Jumanne walitoa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuongeza kuwa hadi juzi vyuo vilivyokuwa vimepokea fedha ni 33.
Pamoja na kwamba HESLB inasema kuwa imebadili utaratibu wa utoaji wa mikopo kuanzia mwaka huu wa fedha kwa kuzingatia vipaumbele, bado tunaona kwamba upo umuhimu mkubwa wa kuwapatia mikopo wanafunzi wote waliodahiliwa baada ya kukidhi vigezo.
Hata kama HESLB haina fedha za kutosha kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wote, lakini upo umuhimu mkubwa kwa serikali kuliangalia hili kwa jicho la huruma ili watoto wa maskini wasio na uwezo waendelee na masomo ya elimu ya juu.
Haitakuwa busara kwa mwanafunzi ambaye alishadahiliwa miaka iliyopita na kukopeshwa halafu mwaka huu anyimwe mkopo kwa maelezo ya kubadilishwa kwa vigezo.
Kuwapatia mikopo wachache na kuwaacha wengi kutaathiri lengo la kuanzishwa kwa HESLB ambalo lilikuwa ni kuwawezesha watoto wa maskini kupata elimu ya juu.
Tunashauri kwamba bodi iweke utaratibu mzuri wa kuwafuatilia na kuwabaini baada ya kujiridhisha waombaji ambao wazazi au walezi wao wana uwezo wa kiuchumi wa kuwasomesha.
Uamuzi mwingine utakaofanyika bila kuzingatia uwezo wa waombaji unaweza kusababisha malalamiko mengi na kuathiri utoaji wa elimu ya juu kwa Watanzania wote.
Tunasisitiza kwamba serikali iliangalie suala hili kwa jicho la pili na jambo la msingi ni kuiwezesha HESLB kwa bajeti ya kutosha sambamba na fedha za bodi hiyo kusimamiwa vizuri tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Uwezo wa HESLB kuendelea kukopesha waombaji wote wenye sifa za kudahiliwa upo kwa kuwa kuna taarifa njema kuwa watu wengi waliokopa miaka ya nyuma wameanza kuzirejesha fedha hizo, katika kipindi ambacho makusanyo ya kodi za serikali yameongezeka.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment