MSAJILI
wa Hazina nchini, Lawrence Mafuru amesema benki nchini zinashindwa
kueleza ukweli juu ya kuyumba kwao na kwamba madai ya kuwa hali zao ni
mbaya kutokana na agizo la serikali la kutaka fedha zake zitunzwe Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), hazina ukweli.
Mafuru amesema taarifa ambazo
serikali wanazo ni kwamba benki hizo zaidi ya 50 zimekopesha fedha
nyingi kwa watu mbalimbali, lakini marejesho ya madeni hayo yamekwama
kiasi cha kusababisha benki hizo ziwe katika hali hiyo.
Akizungumza
jana Dar es Salaam, Msajili wa Hazina licha ya kukiri kuwa mzunguko wa
fedha umepungua kutokana na Tanzania kuchagua kwamba fedha inazozipata
zitumike katika miradi ya maendeleo badala ya matumizi ya kawaida, benki
zinazolalamika zimeshindwa kurejesha fedha ilizokopesha watu na taasisi
mbalimbali.
Akizungumzia taarifa zinazoenezwa kwamba benki zimekosa
fedha za kujiendesha, Mafuru alisema taarifa walizozipata ni kwamba
Septemba mwaka huu, benki hizo zaidi ya 50 nchini zimekopesha zaidi ya
Sh trilioni 16.3 kwa watu mbalimbali.
Hata hivyo, alisema kati ya
fedha hizo, Sh trilioni 1.43 zimekopeshwa bila ya kurudishwa katika
benki husika na kwamba benki hizo zinashindwa kueleza ukweli uliopo
badala yake wanalalamika kwamba hatua ya serikali kuamua fedha zake
zitunzwe BoT badala ya katika benki za kibiashara, ndio sababu ya hali
yao (benki) mbaya.
Kwa mujibu wa Mafuru, serikali imeamua kuchukua
uamuzi huo wa kuzitoa fedha zake kutoka katika benki mbalimbali za
kibiashara nchini kwa ajili ya kuwezesha serikali kujua mapato
wanayopata kutoka katika taasisi zake.
Msajili wa Hazina amesema
zaidi ya Sh bilioni 515 zimeingizwa BoT baada ya uamuzi huo wa Serikali
ya Awamu ya Tano ambao ulitangazwa na Rais John Magufuli baada ya
kushika madaraka mwaka mmoja sasa. Mafuru alikiri kuwa ni kweli kwamba
mzunguko wa fedha umekuwa mdogo na kueleza kuwa chanzo chake si kwamba
benki zimekosa fedha kwa ajili ya kujiendesha.
Alifafanua kuwa awali
watu wengi walitegemea safari na posho ambazo baada ya chenji kubaki,
walikuwa wakitumia bila ya malengo, lakini sio kwamba mzunguko huo wa
fedha unawaathiri watu wote.
“Tumeona tusitegemee wahisani badala
yake tujiwekeze katika miradi mikubwa ya maendeleo ambayo kwa sasa
haitaonekana, lakini baadaye itasaidia kuondoa nafasi iliyopo sasa,’’
alisema Mafuru.
“Tayari shilingi bilioni 515 zimeingizwa BoT na mpaka
Septemba mwaka huu fedha hizo zilikuwa kwenye akaunti hiyo. BoT ni
sehemu ya mfumo wa benki, kwani itakuwa inafanya kazi ya kukopesha kama
zilivyo benki nyingine,” alifafanua Mafuru ambaye ofisi yake inasimamia
mashirika na taasisi za umma.
Alifafanua kuwa ofisi yake ambayo ina
jukumu la kusimamia mapato na matumizi, awali walikuwa wanapata shida
kupata taarifa za mapato na matumizi katika benki hizo zilizopo kila
kona nchini na kwamba baada ya BoT kuchukua dhamana hiyo, imewasaidia,
kwani wanaandika barua na kupatiwa taarifa hizo kwa muda mfupi.
Alisema
serikali inategemea mapato yake kutoka katika makundi matatu ambayo ni
Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na kupitia mashirika na taasisi
mbalimbali.
Alisisitiza kuwa itasaidia kujua mashirika hayo zaidi ya
260 namna wanavyotumia fedha zake katika miradi mbalimbali na kwamba
suala la kuchukua fedha bila ya kuzitumia lisiwepo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment