CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa kimemfungia mwamuzi Rashid
Farahani Webu kuchezesha mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi sita
kutokana na kitendo chake cha kushindwa kuzitafsiri kanuni zinazohusika
na uchezeshwaji wa mchezo huo.
Kwa mujibu wa barua ya chama hicho iliyotolewa jana kwa vyombo vya
habari, mwamuzi huyo alifanya kitendo hicho wakati wa mchezo wa Ligi Kuu
ya Zanzibar Kanda ya Unguja kati ya Miembeni na Jang’ombe Boys baada ya
kutoa maamuzi yaliyokinzana na kuandika ripoti isiyosahihi.
Barua hiyo ambayo imetiwa saini na Makamu wa Rais wa ZFA Unguja, Mzee
Zam Ali inaeleza kwamba uamuzi huo umetokana na kifungu cha 25(d) cha
kuendeshea mpira wa miguu Zanzibar.
“ZFA inakufungia kuchezesha mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi sita
kwa kushindwa kuzitafsiri vyema kanuni zinazohusika na uchezeshwaji wa
mchezo huo, kitendo ambacho kilikufanya kutoa maamuzi yasiyoshihi,
“ilisema sehemu ya barua hiyo.
Sambamba na kufungiwa mwamuzi huyo pia alitakiwa kwa kipindi chote
hicho cha kutumikia adhabu yake kuhudhuria masomo yanayoandaliwa na
Kamati ya Waamuzi, ili aweze kupata uelewa mzuri.
Katika hatua nyingine wachezaji wanne wa timu ya Kimbunga wamefungiwa
kucheza mpira ndani na nje ya Zanzibar kuanzia tarehe ya barua hiyo
hadi mwisho wa msimu wa ligi 2017/2018 kutokana na kitendo cha kufanya
vurugu na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya uanamichezo.
Wachezaji hao ni Haji Nahoda Haji, Shomari Waziri Ali, Juma Simai
Shukuru na Idrissa Simai Pandu ambao bila ya uhalali wowote wanadaiwa
kumpiga mwamuzi Ramadhan Kessy aliyechezesha kati yao na timu ya KMKM
kwenye Uwanja wa Fuoni, ambao ulivunjika katika dakika ya 26.
Adhabu hiyo kwa wachezaji hao imetolewa chini ya vifungu vya 26c(ii)
na 26c(iii) vya kuendesha na kuchezesha soka katika Ligi Kuu ya Zanzibar
2016/2014.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment