Hujambo mpenzi msomaji wa makala haya karibu Ujumuike nami katika makala haya
ya Afya na maisha.
Leo nitazungumzia magonjwa ya kisonono na
mambo mengine kwa kuelezea matibabu ya ugonjwa huo, karibuni.
Kabla ya kueleza tiba ya ugonjwa wa
kisonono ni muhimu kufahamu kuwa, wanawake wana uwezekano mkubwa zaidi wa
kupata ugonjwa huu kwa asilimia 60 hadi 80, huku wanaume wakiwa katika hatari
ya kupata ugonjwa huo kwa asilimia 20.
Hii ni katika hali ambayo, kama
tulivyoashiria huko nyuma dalili za ugonjwa huo huwa hazijitokezi kwa uwazi kwa
wanawake ikilinganishwa na wanaume na pia ugonjwa huu una madhara zaidi kwa
wanawake kwani hata huweza kuwaletea madhara watoto wao wachanga pale
wanapojifungua.
Hayo yote yanaonyesha umuhimu wa
kutibiwa ugonjwa huo mapema hasa kwa wanawake.
Kisonono ni ugonjwa wa zinaa
unaowapata watu wengi na Shirika la Afya Duniani WHO linakadiria kuwa watu
milioni 106 duniani huambukizwa ugonjwa huo kila mwaka.
Lakini je, tiba ya ugonjwa wa
kisonono ni ipi? Tiba ya gono inahusishwa na tiba ya ugonjwa wa chlamydia kwani
mara nyingi magonjwa haya mawili ya zinaa huambatana pamoja.
Matibabu ya kisonono pia hutegemea
umri wa mgonjwa na kama ni mwanamke, ni mjamzito au la, Kwa bahati mbaya
kuhusiana na matibabu ya ugonjwa huo kumeripotiwa ongezeko la kutosikia dawa
vijidudu na hivyo baadhi ya dawa zilizokuwa zikitumika huko nyuma hivi sasa
zimekuwa hazina tena athari na hivyo hazitumiki tena.
Kisonono ambacho sio sugu kilicho
kwenye shingo ya kizazi (cervix), urethra na puru, hutibiwa kwa dawa za
cephalosporin, ambapo mgonjwa hupewa dozi moja ya dawa hizo pamoja na dawa aina
ya macrolide kwa mfano azithromycin, na za jamii ya penicillin kwa mfano doxycyclin
kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa chlamydia.
Mara nyingi kwa wagonjwa walio na
umri wa chini ya miaka 18 na wanawake wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa
sindano.
Mgonjwa hutakiwa kufuata ushauri wa
daktari kabla ya kutumia dawa hizo kwani dawa nyingi huwa na madhara kwa
wajawazito kwa mfano doxycyclin.
Kwa kawaida ushauri nasaha hutolewa
kwa washirika wote wawili wa ngono, na ni vizuri wote wawili watibiwe hata kama
mmoja wao hatakuwa na dalili za ugonjwa huu.
Mara nyingi madaktari huwapatia wale
wanaosumbuliwa na kisonono dozi pia kwa ajili ya wapenzi wao hata bila ya
kupimwa.
&&&&&
Baada ya kufahamu namna ya kutibu
gono, sasa tuangalie madhara ya ugonjwa huo.
1. Moja ya madhara anayoweza kupata mtu kutokana na ugonjwa wa kisonono ni,
mwanamke kutoweza kuzaa yaani kuwa mgumba au mimba kutoweza kutunga.
Tunaelezwa kuwa magonjwa ya zinaa ya
chlamydia na gono yana mchango katika kusababisha wanawake kutozaa kwani
magonjwa hayo kwa asilimia 10 hadi 15 huweza kusababisha uvimbe katika
fupanyonga au Pelvic Inflammatory Disease (PID) na hasa kwa kuwa wanawake wengi
wenye kisonono huwa hawaonyeshi dalili.
Ugonjwa wa PID husababisha makovu
katika mirija ya uzazi hali ambayo husababisha kushika mimba kuwa kugumu na
matatizo wakati wa ujauzito. PID ni ugonjwa unaopaswa kutibiwa haraka.
Kwa upande wa wanaume ugonjwa wa kisonono pia huweza
kuwafanya wanaume wasipate watoto kwani huwasababishia uvimbe katika sehemu ya
mbele ya korodani ambako mbegu za kiume hutengenezwa, Uvimbe huo
usipotibiwa husababisha utasa.
Ugonjwa wa gono pia huweza kuathiri
moyo, ubongo, ngozi na kadhalika kwa hivyo ni hatari sana kwa mtu yoyote na
unahitaji kutibiwa mapema.
Pia ugonjwa huo huleta madhara au uvimbe kwenye
maungio ya viungo, ambapo vimelea vinavyosababisha kisonono huweza kusambaa kwenye
damu na kuleta maambukizo kwenye sehemu nyinginezo mwilini.
Maambukizo hayo
huleta homa, vipele, vidonda kwenye ngozi, maumivu ya viungo na uvimbe.
Vilevile wanawake ambao ni wajawazito na wameambukizwa gono wako kwenye hatari
ya mimba kutoka au kuzaa mapema kabla mimba haijatimiza umri wake (preterm
labor).
Kwa wale wanaoambukizwa gono kipindi cha kukaribia kujifungua, wanaweza
kuwaambukiza watoto wao na hivyo watoto kupata ugonjwa wa uti wa mgongo
(meningitis), kuwa vipofu, homa ya mapafu (pneumonia) na ugonjwa wa mifupa
(septic arthritis).
&&&&&
Bila shaka baada ya kusikia hayo
tuliyoyaeleza kuhusu ugonjwa wa kisonono, unajiuliza tunawezaje kujikinga na
ugonjwa huo.
Mpenzi msomaji unaweza kujikinga na gonjwa hili la zinaa kwa
njia zifuatazo.
Kwanza kabisa ni kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha na
uasherati.
Kuchukua tahadhari na kuzungumzia juu ya ugonjwa huo na dalili zake ili
kuweza kufahamu kuwa mshirika wako wa ngono ana ugonjwa huo au la, na iwapo
anao hatua inayofuata ni kutibiwa na kupata ushauri wa daktari.
Njia nyingine
ya kujikinga ni kuepuka kufanya ngono na mtu aliyeambukizwa gono.
Vilevile
kutumia mipira ya kiume wakati wa kujamiiana, na wanawake wajawazito wanapaswa
kuhakikisha kuwa wanahudhuria kliniki mapema ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa
tiba muafaka iwapo watagundulika kuwa na ugonjwa wa gono au ugonjwa mwingine
wowote.
Wanawake wajawazito wanashauriwa kujifungua hospitalini ili kama mtoto
ameathirika na gono apate matibabu ya haraka baada ya kuzaliwa ili kuepusha
kuwa kipofu.
&&&&&
Tunahitimisha makala hii kwa taarifa inayotujuza kuwa aina mpya ya kisonono imesambaa duniani.
Kwa mujibu wa
taarifa hiyo, aina mpya ya vimelea vya ugonjwa wa gono ambavyo vinahimili dawa
zinazotumika duniani kutibu ugonjwa huu vimegunduliwa.
Taarifa iliyotolewa
na WHO inasisitiza hatari ya kuwa sugu ugonjwa huo unaowaathiri mamilioni ya
watu duniani.
Shirika la Afya Duniani limetoa wito kwa serikali na madaktari
kuongeza ufuatiliaji wa aina hii ya kisonono kutokana na ugonjwa
huo kuwa na madhara mengi kama ugumba, matatizo wakati wa ujauzito na hata
vifo vya kina mama wajawazito.
Dakta Manjula Lusti-Narasimhan, mmoja wa wanasayansi wa Shirika la Afya Duniani katika kitengo cha magonjwa ya zinaa
amesema kuwa, aina hii mpya ya vimelea vya kisonono inaonyesha usugu dhihi
ya dawa zote za antibiotiki tunazotumia kuviangamiza, zikiwemo dawa jamii ya
cephalosporin ambazo ni dawa za mwisho katika kutibu ugonjwa wa kisonono.
Dakta
Manjula Lusti-Narasimhan ametahadharisha kwamba, katika miaka michache
ijayo, aina hii mpya ya kisonono huenda ikawa sugu kwa dawa zote ambazo
zinapatikana kwa sasa na kwamba ugonjwa sugu wa kisonono sio tatizo la
bara la Ulaya au Afrika pekee bali ni tatizo la dunia nzima.
Kwa mara ya
kwanza, vimelea sugu vya ugonjwa wa kisonono dhidi ya dawa za
cephalosporin viliripotiwa katika nchi ya Japan, ikifuatiwa na Uingereza,
Hongkong na Norway.
Wanasayansi wanaamini kuwa, matumizi holela ya dawa aina ya
antibiotiki pamoja na uwezo wa vimelea vya ugonjwa huo hubadilika na
kuzoea mazingira mapya ndio chanzo kikuu cha kuwa sugu kisonono na hivyo muda
si mrefu ugonjwa huu unaweza kuwa janga kubwa dunia kama hatua za haraka
hazitachukuliwa.
Kuna uwezekano wa vimelea hivi sugu vya kisonono kusambaa
kwa haraka duniani bila kugundulika kutokana na nchi nyingi kutokuwa na
ufuatiliaji na utunzaji kumbukumbu mzuri wa wagonjwa wake.
WHO imezitaka nchi
zote kuongeza ufuatiliaji wa wagonjwa wake pamoja na kudhibiti matumizi holela
ya dawa za antibiotiki mpaka pale taarifa kamili za ugonjwa huu
zitakapojulikana.
Msomaji wa makala Haya kumbuka
kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha na ngono zembe na uasherati ni
suala linasisitizwa sana sio tu katika kujikinga na kisosono bali na magonjwa
mengine ya zinaa au STD.
Kwani kwa kawaida kama hujapimwa huwa vigumu kutambua
iwapo wewe au mwenzako ameathirika au la, na kama una michibuko au umekatika
kwenye ngozi unaweza kupata maambikizo ya magonjwa hayo.
Ushauri wa Bure Njia pekee na nzuri ni
kuacha ngono zembe au uasherati hivyo tunapaswa kufahamu kuwa mtu aliyepata gono
mara moja anaweza kupata tena. Tunaishia hapa kwa leo, tudumu katika kheri na
kwaherini.
MTAALAMU WA MAGONJWA HAYA NI SADICK FACK, PAMOJA MITANDAO MBALI MBALI ILIYOSAPOTI KWA HILI.
0 comments:
Post a Comment