MCHAKATO wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umefikia
tamati huku wananchi wakishuhudia viongozi wenye majina makubwa
wakiambulia patupu na vurugu za kila aina zikiibuka.
Katika mchakato huo wa upigaji kura tulisikia malalamiko mengi. Kwa
mfano, wilayani Tarime mkoani Mara upigaji kura ulisimama baada ya kura
za ndiyo kukamatwa na sehemu nyingine tuhuma za rushwa zilikuwa nyingi.
Hali hiyo imeufanya mchakato huo kugubikwa na utata mwingi kwani
ilionekana dhahiri kwamba siku hizi utajiri unaweza kununua siasa au
siasa ikanunua utajiri. Kwa mazingira hayo mfumo wetu wa kupata viongozi
una tatizo kubwa.
Ni tatizo kwa sababu kama mchakato ndani ya chama kimoja unakuwa
umezungukwa na mazingira yasiyoruhusu dhana ya utawala bora kufanya kazi
maana yake ni kwamba wasio na fedha marafuku kupata uongozi.
Hii maana yake taifa linakosa viongozi wazuri na wenye uchungu wa
kutumikia nchi kwa vile mkono mtupu haulambwi. Si hivyo tu, bali
tunaitemea mate dhana nzima ya demokrasia ambayo haiamini katika kupata
viongozi kwa fedha.
Kwa maana kuwa kiongozi bora ni yule anayetokana na ridhaa ya watu na
si kama inavyoonekana katika mchakato huo kwani umeacha majeraha kwa
wengi.
Ni kwa sababu hiyo tunajiuliza kama rushwa ilipewa kiti cha mbele ili
kupofusha wapiga kura, itakuwaje uchaguzi mkuu ujao? Je, wasaka nafasi
za uongozi watabeba fedha za kununua uongozi kwa magari au viroba?
Tunasema hivi kwa sababu ile dhana ya kukataa viongozi wanaonunua
uongozi inafumbiwa macho kwa sababu ya taratibu tunazoambiwa zipo ndani
ya chama. Hii maana yake tunageuza rushwa suala la mapatano badala ya
kuwajibishana.
Kwa mfumo huo chaguzi zetu zitaendelea kuzua maswali yasiyokwisha kwa
sababu tu ya kufunika kombe ili mwana haramu apite. Lakini pia, rushwa
inapozidi hasa kwenye kutafuta uongozi hufikia hatua ya kusababisha
vurugu.
Ni matarajio yetu katika uchaguzi mkuu ujao rabsha na rafu
zilizojitokeza na kuudhalilisha mchakato huo hautajirudia kama kweli
tunataka ufanyike kwa uhuru na haki, vinginevyo kicheko kinaweza
kusababisha vilio.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment