ELIMU ni mafunzo anayopewa mtu kutoka kwa mwalimu au mkufunzi kupitia
njia ya mfumo rasmi au mfumo usio rasmi lengo likiwa ni kutoa maarifa
kwa mwanafunzi.
Maarifa yanayotelewa kwa mtu mmoja au kikundi cha watu humsaidia mwanafunzi kufika mahala, ambapo hajawahi kufika kimaendeleo.
Aidha, elimu huweza kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali za maisha hususan kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa mujibu wa matunda ya elimu watu husema elimu ni sauti ya wasio
kuwa na sauti kwa sababu kupitia elimu mtu anaweza kujikomboa kutoka
kwenye ujinga na maradhi.
Japokuwa elimu inaweza kumtoa mtu mahala ambapo hajafika na pia
kumfanya mtu kuwa wa kwanza katika jambo lolote hata kama historia yake
ilikuwa mbaya, bado mazingira mazuri yanahitajika ili kumsaidia
mwanafunzi kuelewa kile anachojifunza darasani.
Pamoja na mazingira kuwa mazuri jamii inapaswa kushirikiana kwa hali
na mali ili kuhakikisha watoto wanaohitimu darasa la saba wanaelewa
kusoma na kuandika.
Hivi karibuni Taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayojihusisha na
masuala ya utafiti Twaweza, inasema utafiti umebaini asilimia 20 ya
wanafunzi wanaohitimu darasa la 7 hawawezi kusoma hadithi za kiswahili
na kiingereza za kitabu cha darasa la tatu.
Mtafiti wa taasisi hiyo, Elvis Term anasema utafiti uliofanyika
kuangalia watoto wanaohitimu darasa la saba kama wana uwezo wa kusoma na
kuandika uliobeba jina la “je watoto wetu wanajifunza?
Uliofanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja 2013 hadi 2014 na kutoa ripoti tatu, ambapo hii ikiwa ni ripoti ya nne.
Wanafunzi waliopimwa katika utafiti huo walikuwa ni 100,000 wenye
umri wa kuanzia miaka 7-16 uliohusisha wilaya 131 katika mikoa 25
nchini.
Utafiti huo umebaini asilimia 45 tu ya watoto waliopo darasa la tatu
wana uwezo wa kusoma kitabu cha darasa la pili wakati asilimia 55
hawawezi kusoma.
Utafiti huo pia umebaini wanafunzi wawili kati ya 10 pekee ambao sawa
na asilimia 19 ndio wanaoweza kusoma hadithi ya kiingereza ya kitabu
cha darasa la pili.
“Wanafunzi wa darasa la tatu wanaoweza kusoma kiswahili cha darasa la
pili ni kati ya wanafunzi wanne hadi watano ambao ni sawa na asilimia
80,” anasema Term.
Pia, utafiti huo umebaini watoto watatu kati ya 10 ndio wana uwezo wa
kufanya hisabati rahisi za kuzindisha za kitabu cha darasa la pili
ambao ni sawa na asilimia 29 tu ya watoto wanaosoma darasa la tatu.
Anasema akiwa kama mtafiti, utafiti huo unaashiria hali mbaya ya
maendeleo ya elimu duni nchini hali inayomsukuma kutoa mwito kwa jamii
kuzingatia umakini wa suala la elimu kwa watoto.
“Kwa kuzingatia ripoti ya utafiti huu ni dhahiri
matokeoyanathibitisha maendeleo duni ya sekta ya elimu nchini japo
kumekuwepo na juhudi mbalimbali za kuinua kiwango cha elimu nchini,”
anasema.
Pia, anasema tofauti za kijiografia nchini zinaonekana kuwa sababu kubwa zinazoendelea kuathiri uwezo wa watoto kujifunza.
Kutokana na ripoti ya utafiti huo watoto wenye umri wa miaka 7 hadi
16 wanatofauti ya ufaulu wa takribani asilimia 20 kati ya maeneo ya
vijijini na mjini.
Asilimia 67 ya watoto wa mjini wana uwezo wa kusoma hadithi ya
kiswahili ya kitabu cha darasa la pili ikilinganishwa na asilimia 46 tu
ya watoto wa vijijini.
Term anasema asilimia 44 ya watoto wa mjini wanaweza kusoma hadithi
ya kiingereza kitabu cha darasa la pili ikilinganishwa na asilimia 26 ya
watoto wa vijijini.
Anasema tofauti ya kijiografia bado inaonekana kuleta tofauti kubwa
kati ya watoto wa mjini na vijijini na hali hiyo inahusisha baadhi ya
wazazi waliopo maeneo ya vijijini kutofuatilia kile watoto
wanachojifunza.
Aidha, anasema katika wilaya 5 ambazo zimefanya vizuri kwenye utafiti
huo zote ni za mjini, ambapo asilimia ya watoto wenye miaka 9-13 ambao
walifaulu majaribio ya masomo yote matatu, somo la hisabati, kiswahili
na kingereza ni wilaya za mjini.
Mbali na hilo, utafiti huo pia umebaini kuwa kuna tofauti kubwa ya
kusoma na kuhesabu kati ya watoto wanaotoka katika familia tajiri na
masikini.
Pia, anatoa mwito kwa jamii kwamba lazima iwajibike kuhakikisha watoto wanaohitimu darasa la saba wanaweza kusoma na kuandika.
Anasema ni vyema wazazi wachukue jukumu lao la kushirikiana na walimu
kufuatilia maendeleo ya mtoto ili kuwajengea watoto msingi imara wa
masomo.
Kimsingi ni kwamba wazazi wanapaswa kuelewa urithi wa mtoto ni elimu
na elimu bora hujengwa kwa misingi imara ambayo ni pamoja na kufuatilia
maendeleo ya mtoto shuleni ili kumjengea uwezo wa uelewa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment