Image
Image

Maalim Seif,Shein kukutana kwa mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, yataendelea kufanyika leo Ikulu Mjini Zanzibar.

Mazungumzo ya kikao hicho ambacho ni cha tatu,kitaongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.

Wajumbe wa kikao hicho ni Marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, Amani Abeid Karume, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Mazungumzo hayo yanasubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), kufuta matokeoi ya Uchaguzi Mkuu visiwani humu Oktoba 28, mwaka huuu na kuibua mgogoro mkubwa wa Kikatiba.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Nassor Ahmed Mazrui, alisema kuwa hadi sasa mazungumzo hayo bado siri kubwa hata viongozi wa ndani ya chama chake, hawafahamu kinachoendelea tangu viongozi hao wa kitaifa kuanza kukutana.

“Hadi sasa usiri umetawala, sielewi chochote kinachoendelea kama kurejewa kwa uchaguzi au Zec kuendelea kutangaza matokeo, lakini ninachofahamu kuwa kesho (leo), viongozi wakuu watakutana tena kwa mara ya nne Ikulu,” alisema Mazrui ambaye pia ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani humu.

Alisema inasikitisha mno vikao vyote vitatu vilivyofanyika pamoja na hicho kinachotarajiwa kufanyika leo, upande mmoja unawakilishwa na watu watano wakati upande mwingine ukiwa na uwakilishi wa Maalim Seif peke yake.

Alisema mashariti yaliyowekwa katika muongozo wa mazungumzo, ni magumu kwa kuwa hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kushiriki katika mazungumzo ya kutafuta muafaka wa uchaguzi wa Zanzibar zaidi ya Maalim Seif pekee.

Hali kadhalika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud, alithibitisha kufanyika kwa kikao hicho, lakini alisema hafahamu kinachoendelea pamoja na bosi wake kuwa mshiriki wa mazungumzo hayo.

“Yawezekana wewe ndugu mwandishi unafahamu zaidi, lakini na mimi pia nimesikia kuwa viongozi wetu watakutana, bahati mbaya sifahamu kinachoendelea,” alisema Waziri Aboud.

Maamuzi ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar, yamesababisha Baraza la Wawakilishi kukosa uwakilishi wa wananchi kinyume na Kifungu cha 90(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, Baraza la Wawakilishi linatakiwa kuitishwa mkutano wake wa kwanza tangu kuvunjwa Agosti 13, mwaka huu ndani ya siku 90.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, alisema ataendelea kushika wadhifa huo pamoja na Naibu wake bila ya kuwa na wajumbe katika chombo hicho cha kutunga sheria Zanzibar.

Mjadala mkubwa umekuwa ukiendelea katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar kuhusu tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi huku CUF wakiendelea kupinga lakini CCM wanaunga mkono uamuzi wa Zec.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment