Image
Image

Hatari inayowanyemelea wabeba mizigo,iko hapa.

UPO msemo wa wahenga usemao; ‘Kazi ni kazi ili mradi mkono uende kinywani’ lakini kazi zingine zinahatarisha maisha ya watu wengi. Wengi wamejikuta wakiathirika kwa kujua ama kutojua lakini yote haya yanachangiwa na tatizo la ukosefu wa ajira, changamoto ambayo imewafanya vijana wengi kubuni kazi mbalimbali za kujipatia kipato ili kuweza kuendesha maisha yao.
Wapo ambao wamejipatia ajira kwenye masoko mbalimbali nchini, achilia mbali ile ya kuuza bidhaa tofauti tofauti wapo pia ambao wanajishughulisha na ubebaji wa mizigo.
Hali ilivyo
Gazeti hili lilitembelea katika soko la Tandale lililoko Wilaya ya Kinondoni na kukutana na Masha Athuman ambaye anafanya kazi ya kubeba mizigo kwa miaka 15 sasa.
Ni saa tatu asubuhi tayari ameanza kushusha mizigo toka kwenye moja ya magari yaliyokuwa yameegeshwa sokoni hapo kuipeleka katika maghala akishirikiana na wenzake.
“Niliamua kuifanya kazi hii baada ya kufeli kidato cha pili na kushindwa kuendelea na masomo. Mzee wangu hakuwa na uwezo wa kuniendeleza kimasomo na hakuwa na fedha za kunipa angalau za kuanzia biashara,” anasema.
Anasema kutokana na hali hiyo aliona kuliko akaibe mali za watu ni heri aungane na vijana wenzake sokoni hapo kufanya kazi hiyo.
“Niliamua kutumia nguvu nilizojaliwa na Mwenyezi Mungu kubeba mizigo ili nipate ridhiki yangu.
“Ingawa napata fedha za kuendesha maisha yangu lakini suala la uzito wa mizigo tunayobeba ni changamoto kubwa, mara nyingi tunapata maumivu ya viungo hasa mgongo.
“Yaani ukimaliza kubeba mzigo, halafu ukae chini au ulale unahisi kama vile mgongo si wa kwako tena maana maumivu huwa ni makali mno, lazima umeze dawa ya kuyatuliza,” anasema.
Wanabeba zaidi ya kilo 100
Anasema licha ya kuwapo kwa maelekezo ya kuwataka wakulima kuhakikisha mizigo inakuwa na ujazo wa kilogramu 90 lakini wapo ambao wameendelea kukaidi amri hiyo.
“Mizigo inaletwa ikiwa na ujazo wa kilo 120 hadi 130, wengi  hapa uzito wetu ni kilo kati ya 60 hadi 80, kazi ni ngumu, kubwa na ujira tunaopata ni mdogo,” anasema Athumani.
Anasema kwa kawaida huwa wanalipwa ujira wao kwa kuhesabiwa kiasi cha tani wanazoshusha toka kwenye gari husika.
“Bei ya sasa hivi ni Sh 6000 kwa tani moja na wakati mwingine huwa inapanda hadi Sh 7000 kutegemeana na msimu, kiasi hiki ni kidogo, kama unavyotuona hapa tupo zaidi ya 10 na gari tunaloshusha lina tani 30.
“Tukimaliza kazi na kugawana ujira mara nyingi  mtu mmoja hupata Sh 17,000, ni fedha kidogo mno tunapata ukilinganisha na kazi tunayofanya,” anasema.
Sheria ya Vipimo
Sheria ya Vipimo namba 340 ya mwaka 2012 imeainisha kuhusu ujazo wa mazao ya kilimo kati ya kilo 90 hadi 100.
Wakala wa vipimo (WMA) umeelekeza kuwa mazao kama maharage, mbaazi, kunde, mahindi, ngano na mtama yanatakiwa yafungwe katika magunia ya ujazo wa kilo 90 wakati mchele, chumvi, sukari, vitunguu, viazi mbatata na vitamu vinatakiwa viwe katika ujazo wa kilo 100.
Wengi hupata TB
Anasema hiyo ni kutokana na lile vumbi linalokuwa katika mizigo na kwamba hupatwa pia na maumivu ya viungo hasa mgongo na wakati mwingine kuvunjika miguu.
“Binafsi nilishawahi kuanguka, nikavunjika mguu, nilisikitika mno, nilitumia zaidi ya Sh 200,000 kujitibia hadi nikapona na kurejea kazini.
Anasema alirejea kazini kwa sababu hana namna nyingine ya kujipatia kipato zaidi ya kazi hiyo.
“Ni kweli miongoni mwetu wengine hatujasoma lakini tunahitaji kupata fedha za matumizi kama wanadamu. Tunaiomba serikali itusikilize kilio chetu, suala la ujazo wa mizigo inayokuja sokoni lisimamiwe ipasavyo kuokoa afya zetu,” anasema.
 Kisa cha Yusuph
Yusuph Ally naye alikuwa akibeba mizigo sokoni hapo tangu mwaka 1994 lakini kwa sasa ameacha baada ya kuvunjika kiuno.
“Nakumbuka ilikuwa ni miaka mitano tangu nilipoanza kazi hii, siku moja nilianguka na gunia, nilikwenda Hospitali ya Tandale ambako nilipewa dawa za kutuliza maumivu, nilimeza kwa siku tatu na baadae nikarejea kazini,” anasema.
Anasema kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele alianza kuona uvimbe mgongoni katika njia ya uti wa mgongo.
“Uvimbe ule ulizidi kukua kila siku, nikaanza kuhisi maumivu makali ya mgongo, ilifika mahali sikuweza kunyanyua tena mzigo nikawa nafanya kazi ya kuwatwisha wenzangu.
“Maumivu yakazidi kuwa makali nikaelekezwa kwa daktari mmoja huko Kibaha mkoani Pwani ambaye ni mtaalamu wa mifupa, akanipiga picha ya mionzi lakini hakuona tatizo, akanipa dawa zilizonigharimu Sh 50,000 lakini hazikunisaidia,” anasema.
Anasema kwa kuwa aliendelea kupata maamivu alilazimika kutumia dawa za kutuliva maumivu aina ya ‘dicloper na diclofenac’ kwa muda mrefu ili apate nafuu.
“Lakini hali ilizidi kuwa mbaya nikaamua kuacha kubeba mizigo mikubwa, nilipata kibarua kwa wakala wa kuuza soda lakini nililazimika kubeba makasha ya kuwekea soda.
“Sasa unajua ‘kreti’ ikiwa na soda inakuwa na uzito pia, hali hiyo ilinizidishia maumivu na ilifika wakati nikapatwa na ganzi mwili mzima. Nilishindwa hadi kutembea na kuna wakati nilikuwa naanguka na kuna siku nilishindwa kabisa kuamka kitandani.
“Ikabidi nitume mtu kwa bosi wangu akaja nyumbani kunichukua na guta (baiskeli ya miguu mitatu) hadi ofisini kwake, ambako nilikwenda kumuonyesha mahala ambako nilihifadhi fedha zake kisha akanirudisha nyumbani,” anasimulia.
Anasema aliendelea kukaa nyumbani na hali yake ilizidi kuwa mbaya hivyo akalazimika kuwajulisha wenzake.
“Wale niliokuwa nabeba nao mizigo walikuja nyumbani wakanichukua hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),” anasema.
Anasema wakati huo hakuweza tena kutembea alikuwa anabebwa kama mtoto mdogo.
“Nikahamishiwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) wakanipiga X-rays na kubaini uti wa mgongo ulikuwa umevunjika.
“Waliniambia natakiwa kuwa na koti la plastiki ambalo nililipia Sh 150,000 na nilihangaika zaidi ya mwezi kupata fedha hizo,” anasema.
Anasema masharti mengine aliyopewa na daktari ni kutakiwa kulala chini na alipoenda kliniki alitakiwa kuwa na Sh 160,000 za kununulia dawa.
“Kuna dawa fulani baadae walinipa zinafanana na zile za TB, zilikuwa bei ghali kidogo lakini ndizo zilizonisaidia hadi leo hii unaona ni mzima,” anasema.
Anasema kwa sasa ameamua kuachana na shughuli hizo za kubeba mizigo ili kulinda afya yake.
“Wakati ule mzigo ulikuwa unakuja na kilo 200 na kuendelea, nilikuwa napata Sh 10,000 hadi 20,000 kwa siku. Mwanzoni ni ngumu kuzoea uzito huu lakini unaanza kuzoea na kuona ni kitu cha kawaida, nilikuwa na uwezo wa kukimbia na kilo hizo kuelekea ghalani
“Nilitumia zaidi ya Sh 800,000 kujitibu maradhi yale, Namshukuru Mungu nimepona siku hizi nafanya biashara ya kuuza kanzu,” anasema.
Kisa cha Kassim
Juma Kassim ni kijana anayebeba mizigo katika Kituo cha Mbezi Mwisho, kazi ambayo ameanza kuifanya tangu Oktoba 2004 hadi sasa.
“Naifanya kwa sababu inanisaidia kupata fedha ya kula na kulipa pango, mimi ni mwenyeji wa Dodoma nilikuja Dar es Salaam kutafuta maisha, nilizaliwa bila ulemavu lakini sasa ni mlemavu.
“Si rahisi mtu kunitambua pindi anaponiangalia lakini mkono wangu wa kushoto umepinda kidogo, hali hiyo ilinipata baada ya kuanguka nikiwa na gunia kichwani na kuudondokea mkono huu (anamwonyesha mwandishi),” anasema.
Daktari
Abdalah Makala ni Daktari Bingwa na Mkuu wa Kitengo cha Mazoezi katika Idara ya Huduma za Utengamao (Fiziotherapia), iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Anasema katika kitengo hicho huwa wanapokea wagonjwa kati ya 200 hadi 250 kwa siku ambapo zaidi ya asilimia 60 ni wale wanaosumbuliwa na maumivu ya mgongo.
“Watu wanaobeba mizigo mizito hujiweka katika hatari ya kupata maumivu ya mgongo, katika idara yetu kundi hili ndilo kubwa kuliko wengine,” anasema.
Anasema asilimia 25 huwa ni watoto walio chini ya miaka mitano ambao wamezaliwa na matatizo ya mtindio wa ubongo, asilimia 10 ni wale wenye kiharusi na asilimia tano wanasumbuliwa na matatizo mbalimbali yanayotokana na umri mkubwa.
“Huwa tunatumia mashine za umeme za kuvuta mgongo, kusisimua misuli na neva za fahamu katika kumtibu mgonjwa husika. Lakini pia tunatumia mikono yetu, chupa maalumu ya maji ya moto (hot pack) pamoja na barafu.
“Barafu ni zuri zaidi, hutuliza maumivu ndani ya saa 72, huongeza kasi ya mzunguko wa damu mwilini na kupunguza uvimbe katika sehemu husika,” anasema.
Historia ya kitengo hicho
Anasema idara hiyo ilianzishwa kati ya mwaka 1950 na 1960 ikiwa chini ya Idara ya Mifupa.
“Baadae ikatengana na kujitegemea na kuwa Idara ya Fiziotherapia na kisha kuungana na Idara nyingine ya Tiba ya Mikono. Kutokana na muungano huo ikabidi ibadilishwe jina na kuwa Idara ya Huduma za Utengamano (Re-habitation),” anasema.
Daktari huyo anasema kazi kubwa ya idara hiyo ni kupunguza uwezekano wa watu kupata ulemavu.
“Gharama za matibabu hutofautiana kulingana na tatizo husika, wagonjwa wetu wengi wanalipa kwa bima, lengo la kitengo hiki ni kusaidia watu wasipatwe na ulemavu,” anasema Dk. Makala.
Anasema kitengo hicho pia huwahudumia wanawake ambao matumbo yao hayajafunga baada kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua.
“Wanapojifungua misuli husinyaa na baada ya kushonwa wakati wa upasuaji kama hakushonwa vizuri lazima apate maumivu, sasa sisi tunao uwezo wa kumrejesha katika hali ya kawaida kwa mazoezi, nawasihi wananchi waje tutawatibia,” anasema.
Wagonjwa wanaosumbuliwa na maumivu ya mgongo ni zaidi ya asilimia 60, asilimia 25 ni watoto wenye mtindio wa ubongo, asilimia 10 ni wale wenye kiharusi na asilimia tano husumbuliwa na maradhi ya utu uzima.
“Kwa hiyo tumekuwa tukiwapa matibabu na elimu, mfano watu wanaonyanyua vitu vizito mara nyingi hupatwa na matatizo ya mgongo hivyo huwa tunawapa elimu hii jinsi gani wanapaswa kunyanyua mzigo ili wasipate madhara na tunawaelekeza namna ya kusogeza mzigo mzito,” anasema.
Anasema kundi lingine ambalo wamekuwa wakilifikia kuwapa elimu ni mafundi, wanawake na watu wanaotumia muda mwingi kukaa ofisini.
“Kwa hawa wa ofisini huwa tunawaelekeza njia bora za kufuata wakiwa wanatumia kompyuta zao wasipatwe na matatizo,” anasema.
Wagonjwa
Amanda Ndege ni mama wa watoto mapacha, Zuri na Tenzi wenye umri wa mwaka mmoja na nusu ambao alijifungua Aprili 23 mwaka huu, ni miongoni wa wanaohudhuria kliniki katika kitengo hicho.
“Tenzi ukuaji wake upo vizuri lakini hali imekuwa tofauti kwa Zuri, tangu mimba yangu ikiwa na wiki 17 madaktari walibaini ana tatizo la kichwa kikubwa,” anasema Ndege.
Anasema alilea mimba yake hiyo hadi alipojifungua na kwamba Zuri alianzishiwa tiba mapema akiwa na umri wa siku saba.
“Awali tulikuwa tukitibiwa Hospitali ya Ami, tukahamia MOI kwa matibabu zaidi,” anasema.
Anasema Zuri alipofikisha umri wa miezi mitano ndipo alianzishiwa rasmi tiba hiyo ya mazoezi.
“Nilimleta hapa MNH akaanza kupata matibabu, mwanangu amepitia mapito mengi ndiyo maana tulimpa jina la Zuri kwa sababu hatukutarajia kumpata, namshukuru Mungu matibabu haya yamemsaidia kwa kiasi kikubwa kwani maendeleo yake kwa ujumla ni mazuri.
“Sasa hivi ukimuita anasikia, anaweza kugeuka kukuangalia na ameanza kukaa kwa kutegemea mikono yake. Awali hakuyaweza yote haya, hakika mazoezi ni dawa, nawashukuru madaktari kwa kumsaidia,” anasema.
Naye Neema Mwalasa (48) ambaye ni mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni miongoni mwa wagonjwa wanaopata matibabu katika kitengo hicho.
“Ilikuwa mwaka 2003 nilipoteleza na kuanguka bafuni, nikaanza kusikia maumivu ya mgongo taratibu baadae yakawa makali ilipofika mwaka jana,” anasema Neema.
Anasema alipoona yanazidi ndipo aliamua kwenda katika hospitali ya Rejence ambako alifanyiwa vipimo na baadae kuhamia Lugalo kisha MOI ili kupata matibabu zaidi.
“Pale MOI nilishauriwa kuwa pamoja na kupata dawa za matibabu na vipimo ni vema nipate pia mazoezi ndipo nikaja Muhimbili na kupokelewa na Dk. Quresh Karimjee na nimeanza kupata nafuu,” anasema.
Siku ya Fiziotherapia Duniani
Dk. Makala anasema Septemba 8, kila mwaka huwa ni Siku ya Fiziotherapia Duniani, mwaka huu maadhimisho hayo yamepewa kaulimbiu isemayo ‘Kuongeza Umri wa Kuishi’.
“Huwa tunatumia maadhimisho haya kutoa elimu kwa jamii ili waepuke kujiweka katika hatari ya kupata maradhi mbalimbali, hasa kwa kufanya mazoezi ambayo husaidia kuepuka maradhi mengi yasiyokuwa ya kuambukiza. Kuanzia mwakani MNH tutakuwa tunayaadhimisha kwa kufanya shughuli mbalimbali,” anasema.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment