SAKATA la Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL), kugeuziwa kibao kwa kutakiwa kurejesha zaidi ya Dola za
Marekani milioni 100 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 216.2 kwa Shirika la
Umeme nchini (Tanesco), limezidi kuchukua sura mpya baada uongozi wa
kampuni hiyo kuibuka.
Kuibuka kwa viongozi hao kumekuja siku chache baada ya Wakili wa
Tanesco, kueleza hatua watakazochukua kuhusu uamuzi huo baadaya Mahakama
ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID), uliotolewa Septemba
12 mwaka huu unaoitaka Tanesco kuilipa Standard Chartered ya Hong Kong
(SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu
Mwenyekiti ambaye pia ni Mwanasheria wa Kampuni wa IPTL, Joseph
Makandege alisema hawatambui madai ya Benki ya Standard Chartered ya
Hong Kong (SCB-HK) kama mdai na wala hawana haki kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na hali hiyo alisema inaungana na Shirika la Umeme nchini
(Tanesco) kukata rufaa katika Mahakama ya ICSID kwani hukumu iliyotolewa
ina mapungufu mengi ya kisheria.
Licha ya uamuzi huo Makandege alisema IPTL haikulipwa kwa kutumia
viwango vya zamani bali walilipwa kutokana na umeme waliouuza kwa
Tanesco na si vinginevyo.
Alisema watu wasifanye makosa kuilipa benki hiyo kwani inachotaka
kufanya ni kitendo cha utapeli kwa msukumo wa kampuni za mabeberu.
“Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong hawastahili kulipwa fedha
na Watanzania kwani hawastahili kwa mujibu wa sheria nasi kama IPTL/PAP
hatuwatambui na hawana haki ya kutuzungumzia. Na ndiyo maana wameamua
kukimbia mahakama zetu za ndani na kukimbili nje, hawa wana msukumo wa
mabeberu wenye nia ovu.
“Kwa uamuzi huu wenye utata uliotolewa na ICSID ni wazi Standard
Chartered walikuwa na nia ovu, ninasema hivyo kwa sababu tangu Septemba
5, mwaka 2013 suala hili liliamuriwa vizuri chini ya Jaji Utamwa (John)
na IPTL ikashinda kesi na kutwaa uongozi.
“Na hili si la kwanza kwani Aprili 3, 2014 tulifungua shauri namba
60 chini ya Jaji Dk. Fauz Twalib la kuitaka Mahakama itamke kwamba
benki ya Standard Chartered Hong Kong si wadeni wetu, tena awali
waliibuka na hoja kwamba hawasikilizwi na Mahakama zetu za ndani kwa
wakati ambapo shauri hilo lilipangiwa kusikilizwa mfululizo.
“Lakini pia dai letu lingine tuliomba Mahakama Kuu itupe nafuu ya
Standard kutulipa gharama kama fidia ya Dola za Marekani bilioni 3.240
ambapo hata tuzo waliopewa na ICSID eti wanataka walipwe Dola za
Marekani milioni 148 na kama wakitulipa fedha zetu hata madai yao
yaingia humo nab ado kuna fedha nyingine inabidi watupatiwe sisi,”
alisema Makandege
Wakili huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa
IPTL/PAP, Harbindar Singh Sethi mwenye makazi yake hapa nchini na Afrika
Kusini, alisema licha ya mahakama kutoa uamuzi wataendelea kusimamia
uamuzi huo wa kutomtambua mtu anayeitwa Martha Renju wala Benki ya
Standard Chartered ya Hong Kong.
“Sisi msimamo wetu kama IPTL/PAP tunasema hadharani kwamba
hatuitambua Benki ya Standard Chartered ambao hawa kila wakati wamekuwa
wakikimbia mahakama zetu za ndani na kukimbilia nje na hata hukumu hii
ya tuzo ina viashiria vya mabeberu.
“Tuzo husika waliyopewa ni dhahiri Standard Chartered ni batili kwa
mujibu wa sheria. Wao ni kina nani hadi wakafungie kesi kwa niaba yetu.
Hii ni kesi ya ngedere imepelekwa kwa nyani,” alisema
Kutolewa fedha za Escrow
Akizungumzia mchakato wa kutolewa fedha katika akaunti ya Tegeta
Escrow, Makandege alisema mchakato wa kutolewa kwa fedha hizo ulikuwa wa
kihalali kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisema Julai 5, mwaka 2006, Serikali na IPTL waliingia mkataba wa
Escrow ambao ulipelekea kutolewa kwa fedha hizo kwenye akaunti hiyo
iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) bila kuwahusisha
Benki ya Standard Chartered.
“Oktoba 8, 2010 IPTL na Tanesco kwa kuzingatia kipengele cha 10 cha
mkataba huo ambayo kinaeleza kuwa endapo kuna mgogoro baina ya pande
hizo mbili wahusika watakutana na kujadiliana na hatua ya kuafikiana
itahesabika kuisha kwa mgogoro.
“Hata ripoti mbalimbali ikiwemo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) hakuna sehemu yoyote inayoeleza kuwa zile fedha ni za
umma. Hata ICSID imetoa hukumu na kusema si fedha za Serikali lakini
wanakiri zilitolewa kihalali ingawa hawakupewa Standard na kama
kungelikuwa na mgogoro fedha zile singetolewa,” alisema
Kunyang’anywa mitambo
Alipoulizwa kuwa hatua ya suala hili kugubikwa na utata na
utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge la 10 likiwemo la wao
kunyang’anywa mtambo, Makandege alisema wanajua kuna watu hivi sasa
wanahaingika wakitaka kuona suala hilo linafanyika.
Pamoja na hali hiyo alisema kuwa mitambo bado ni mali yao kwa mujibu
wa sheria na hakuna hatua itakayowafanya wafanikiwe watu hao ambao
hakuwataja.
“Tunajua kuna watu hivi sasa wanataka kuona suala hili likitekelezwa
ikiwemo IPTL kunyang’anywa mtambo, ninawaambia hakuna jambo kama hilo,
nasi kila wakati tumekuwa wazi ikiwemo kulaani maazimio ya Bunge ambayo
ni wazi yalikuwa na lengo la kukimbiza wawekezaji wazawa. Suala hili
hata Rais mstaafu (Jakaya Kikwete) aliliweka wazi kwa nini lianze sasa
baada ya mjadala wake kufungwa,” alisema.
Kauli ya Mwanasheria Tanesco
Wiki ilipita Wakili wa Tanesco, Richard Rweyongeza alisema
walichokuwa wanabishania mahakamani si Tanesco kulipa bali walikuwa
wanabishania italipa kiasi gani na analipwa nani.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akizungumza na MTANZANIA ambapo
alichambua hoja mbalimbali ikiwemo uamuzi wa ICSID kuhusu tuzo waliyoipa
Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.
“ Kabla hatujaingia katika kutetea kesi hiyo, mwaka 2014 mahakama
hiyo ilisema inayo madaraka na ikaamuru Tanesco kuilipa SCB-HK.
“Sisi tuliingia kutetea baada ya uamuzi huo Mei, 2014 tukaomba hesabu
zifanyike upya kwa malekezo yaliyotolewa na mahakama hiyo ili kujua
deni halisi, hesabu zilipofanyika kwa mtaji wa mwekezaji walichukua
mkopo wakahesabu kuwa ni mtaji, hatua hiyo ilikataliwa na mahakama.
“Kabla ya hesabu kufanyika ndipo ikaingia suala la akaunti ya Tegeta
Escrow, fedha zilipochukuliwa katika akaunti hiyo, SCB-HK wakabadilika
wakasema hakuna haja ya kufanya hesabu upya kwa sababu Tanesco
wamekubali viwango hivyo ndio sababu waliwalipa IPTL.
“Tulibishania hoja hiyo ya kulipa kwa viwango vya zamani ikaamuliwa
hesabu zifanyike upya, mahakama ilikubali hesabu zifanyike kwa kutumia
mkopo wa wana hisa.
“Baada ya kuamuru hivyo deni likashuka kutoka walichokuwa wakidai
Dola za Marekani milioni 369 hadi kuamuliwa kulipa Dola za Marekani
milioni 148,”anasema Wakili Rweyongeza.
Alisema IPTL walilipwa Dola za Marekani milioni 246 kwa kutumia
viwango vya zamani na kwamba uamuzi uliotolewa unaanza kutumika katika
kipindi chote ambacho Tanesco ilikuwa inadaiwa mpaka mwaka 2015.
“Kutokana na hesabu hizo gharama ilikuwa chini, IPTL ililipwa zaidi
hivyo inatakiwa kurejesha Dola za Marekani zaidi ya milioni 100 kwa
Tanesco,”alisema.
Rweyongeza alisema walipendekeza SCB-HK wadai fedha zao kwa IPTL
lakini mahakama hiyo ilikataa na kuamuru Tanesco ndio walipe hivyo kwa
mtazamo wa kawaida IPTL inatakiwa kurejesha fedha kwa shirika hilo.
Katika kuhitimisha mahakama hiyo ilisema pande zote mbili
zinazopingana zilishinda katika maeneo muhimu waliyokuwa wakibishania
lakini zilipoteza katika hoja zingine.
Baada ya kumaliza kusikiliza kesi hiyo mahakama iliamuru pande hizo
mbili kulipa gharama za usuluhishi na zingine kwa viwango sawa.
Malipo hayo na anayelipwa katika mabano ni Dola za Marekani
254,775.02 (Profesa MC Rae), Dola 171,278.36 (Profesa Douglas) na Dola
370,126.76 kwa ajili ya Profesa Stem.
Gharama zingine zilizokadiriwa moja kwa moja ni Dola za Marekani
157,336.26 na gharama za utawala wa mahakama hiyo Dola za Marekani
180,000 ambapo jumla ya gharama zote wanazotakiwa kulipa Tanesco na
SCB-HK ni Dola za Marekani 1,133,516.42.
Fedha hizo zilitolewa na kwenda kwa Kampuni ya Pan Africa Power
Solutions Tanzania Limited (PAP) kwenda kwa mmiliki wake, Harbindar
Singh Sethi mwenye makazi yake hapa nchini na Afrika Kusini.
Katika kesi hiyo Tanesco ilikuwa inawakilishwa na mawakili wa kampuni za R.K Rweyongeza & Advocates na Crax Law Partners.
Chanzo cha Escrow
Mwanzoni mwa miaka ya 1990 nchi ilikuwa na upungufu wa umeme
kutokana na upungufu wa maji kwenye mabwawa, ambapo 1994 serikali ilitoa
kazi ya uwekezaji kwa IPTL iliyokuwa ikimilikiwa na VIP ya Tanzania
iliyokuwa na asilimia 30 na Mechmar ya Malaysia yenye asilimia 70.
Kutokana na hali hiyo Tanesco na IPTL walisainiana mkataba wa miaka
20, hata hivyo uzalishaji haukuanza mara moja kutokana na mgogoro
ulioibuka baina yao (Tanesco na IPTL) .
Mwaka 2002 IPTL ilianza kuzalisha umeme na mkataba ukaanza
kuhasabiwa hapo, lakini kutokana na mgogoro ikafunguliwa akaunti ya
Escrow na mwaka 2004 Tanesco ilifungua shauri kupinga tozo la Capacity
Charge
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment