MAABARA
ya kupima sampuli za ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kwa kutumia panya buku
wa Mradi wa Apopo ulio chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine
(SUA), imezinduliwa jijini Dar es Salaam, huku ikielezwa kuwa panya
mmoja ana uwezo wa kupima sampuli 100 ndani ya dakika 20.
Uzinduzi wa
maabara hiyo ulifanywa jana na Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za
Afya wa Wizara ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Dk Mohamed Mohamed kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo na
uzinduzi ulioshuhudiwa na wadau mbalimbali pamoja na wananchi.
Akielezea
mradi huo wa kupima vimelea vya kifua kikuu kwa kutumia panya
waliofunzwa, Meneja Mradi, Dk Georgies Mgode alisema panya hao wana
uwezo wa kubaini harufu ya vimelea vya ugonjwa huo ndani ya sekunde.
Aidha,
alisema kwa dakika 20 panya anaweza kupima sampuli 100 wakati sampuli
kama hizo zingepimwa kawaida kwenye maabara zinazotumia hadubini kwa
siku nne, hivyo majibu hadi yafike kwa mgonjwa yanaweza kuchukua siku
saba ili hali kwa kutumia panya mgonjwa ndani ya siku moja anapata
majibu na kuanza tiba.
“Ni kweli hawa panya wana faida kubwa kwenye
ugunduzi wa vimelea vya ugonjwa wa TB, kwa sababu wana uwezo ndani ya
sekunde wakabaini maambukizi ya kwa mgonjwa wakati mtu wa maabara
anatumia zaidi ya siku moja kupata majibu,” alisema Dk Mgode.
Alisema
kwa kuzinduliwa kwa maabara hiyo itakayokuwa na panya buku 10 jijini
Dar es Salaam ni hatua ya mafanikio ya harakati za vita dhidi ya ugonjwa
huo hasa kwa kuwa jiji hilo ndilo linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya
watu, kuliko maeneo mengine na pia ni moja la miji yenye idadi kubwa ya
wagonjwa wa kikua kikuu.
Akielezea jinsi panya hao wanavyofanya
kazi, Dk Mgode alisema katika mradi wa Apopo panya hao walifanyiwa
utafiti na wakagundulika kuwa na vinasaba vingi kuliko mnyama mwingine
na ubongo wao una uwezo mkubwa wa kubaini vitu wakifundishwa.
Alisema
kutokana na nchi kuwa miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi ya juu ya
ugonjwa huo, kutumia njia ya hadubini kwenye maabara pekee hakutoshi
katika kupambana na ugonjwa huo, na kuwa njia hiyo inatoa uhakika wa
sampuli kwa asilimia 20 hadi 60 huko asilimia 40 hawagunduliki na hivyo
kuendelea kuambukiza wengine.
Alisema kwa kutumia panya buku, wana
uwezo wa kutambua harufu ya vimelea vya kifua kikuu, tofauti na vipimo
vya kawaida vinavyotumika hospitalini ambavyo ni lazima vimelea vya
ugonjwa huo vionekane kwenye darubini, jambo ambalo wakati mwingine ni
vigumu kubaini vimelea hivyo iwapo mgonjwa hakuonesha dalili yoyote ya
ugonjwa.
Alisema katika mradi huo, maabara nyingine ya panya buku iko
Morogoro ambayo hutumika kupima sampuli mbalimbali kutoka hospitali 28
nchini ambazo hupeleka sampuli za wagonjwa na tangu mradi huo uanze kazi
mwaka 2008 zaidi ya sampuli 380,000 zimeshapimwa kutoka hospitali
mbalimbali nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua maabara hiyo, Dk
Mohamed alisema hiyo ni hatua kubwa ya kuokoa maisha ya watu na kuzuia
maambukizi ya ugonjwa huo ambao changamoto kubwa ilikuwa kwenye upimaji
kubaini vimelea wa ugonjwa huo.
“Hii ni hatua kubwa tunapongeza
juhudi hizo za kuunga mkono serikali harakati za kupambana na ugonjwa wa
TB, kwa sababu wakati mwingine hadi kuugundua ugonjwa ilikuwa vipimo
kama kuotesha sampuli vifanywe na majibu yalichukua hata wiki sita, sasa
utaona jinsi ugonjwa ulivyokuwa ukienea”, alisema Dk Mohamed.
Kwa
upande wake, Mwakilishi kutoka Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Kifua Kikuu
na Ukoma (NTLP), Dk Allan Tarimo alisema Tanzania ni moja ya nchi zenye
maambukizi ya juu ya ugonjwa wa kifua kikuu na katika takwimu barani
Afrika inashika nafasi ya nne huku kimataifa ikiwa nafasi ya sita.
Dk
Tarimo alisema pamoja na kuwa ugonjwa huo unatibika mgonjwa anapowahi
kupata tiba, lakini hadi sasa ni kati ya wagonjwa 165,000 wanaogundulika
kwa mwaka, wanaopata tiba ni chini ya wagonjwa 62,000.
Alisema kwa
mujibu wa muongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa siku moja
mtaalamu wa maabara anatakiwa kupima wagonjwa 20 tu wa kifua kikuu, ila
kwa kutumia panya hao, kwa dakika 20 wanaweza kupima sampuli 100, na
hiyo inakuwa mkombozi kwa kupunguza tatizo hilo, kama sio kuliondoa.
Kwa
upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Magonjwa ya
Mifugo (TVLA), Dk Furaha Mramba alisema mradi huo na maabara hiyo
itakuwa mkombozi kutokomeza ugonjwa huo nchini.
TVLA wametoa eneo
lililojengwa maabara hiyo jijini Dar es Salaam ili kusaidia kupambana na
ugonjwa huo na kwamba watafiti wa mradi huo wa Apopo wanafanya kazi na
watafiti kutoka TVLA.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment