Asilimia kubwa ya wakazi wa kijiji cha Chikunja, wilayani Masasi,
wameshawasili kwa Binti Palanga, wakinywa pombe aina ya gongo. Wengine wameketi
chini ya mkorosho wakinywa chibuku, na baadhi wapo katika kikundi
wakishirikiana kopo lililojaa pombe maarufu ya wanzuki.
Si
kijiji cha Chikunja pekee, haya ndiyo maisha ya wakazi wa maeneo mengi nchini
Tanzania ambao takwimu zinaonyesha wanakunywa zaidi pombe za kienyeji kuliko
wale wanywaji wa pombe nyingine zinazotengenezwa viwandani.
Pia,
takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, Tanzania ni miongoni
mwa nchi za Afrika zenye wanywaji wengi zaidi wa pombe ukilinganisha na nchi
nyingine.
Miongoni
mwa nchi 55 za Afrika zilizo chini ya uangalizi wa WHO, Tanzania inashika
nafasi ya tatu kwa kuwa na wanywaji wengi zaidi wa pombe baada ya Nigeria na
Uganda. Nchi nyingine zenye kiwango kikubwa cha wanywaji ni Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Kenya, Angola na Afrika Kusini.
Hata
hivyo takwimu hizo za WHO, licha ya kuonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa
nchi zenye wanywaji wengi wa pombe, takwimu hizo ziliweka wazi kuwa, asilimia
kubwa ya Watanzania hao, wanakunywa pombe za kienyeji au kwa jina jingine
'mataputapu'.
Kwa
mfano, katika wanywaji hao, asilimia 86 wanakunywa pombe za kienyeji kama
wanzuki, chibuku, rubisi, mbege, dadii, choya, moonshine, banana na gongo
wakati ni asilimia 10 tu wanaokunywa bia na asilimia moja wanakunywa mvinyo wa
viwandani, huku asilimia tatu wakinywa pombe nyingine kali zilizotengenezwa
viwandani.
Kwa
mchanganuo huo, wanaokunywa pombe za viwandani ni asilimia 14 tu ya wanywaji
wote.
Dk
Andrew Kitua wa Hospitali ya Hubert Kairuki anasema baadhi ya pombe
huchanganywa na vilevi vyenye hatari kiafya kwa mfano anasema, methanol,
ethanol au furfural inapozidi husababisha upofu na haitakiwi kunywewa na
binadamu.
Anasema,
kwa kawaida pombe za kienyeji hutengenezwa kwa kusindika nafaka, na nafaka hizo
zinapochachushwa hutengeneza vilevi(alcohol).
Anasema
hata hivyo kiwango cha 'alcohol' hicho kimetofautiana kulingana na aina ya
nafaka iliyotumika, kiwango cha joto kilichotumika kusindika na muda uliotumika
kuchachusha pombe hiyo.
Pamoja
na madhara ya vilevi, Mfamasia katika Hospitali ya Amana, Charles Lymo anasema,
tatizo lingine linalosababisha madhara kwa wanywaji wa pombe za kienyeji ni
aina ya unywaji na namna ya upikaji.
"Kuna
pombe zinachanganywa na hamira, hamira zenyewe hazina kipimo, huwezi kujua
hamira hiyo inaweza kuleta madhara makubwa kwenye mwili wa binadamu,"
anasema.
Anaongeza
na kusema kuwa aina ya unywaji wa pombe za kienyeji husababisha magonjwa ya
kuambukiza, kwa mfano, kopo moja la mbege huweza kutumiwa na watu zaidi ya kumi
au mrija mmoja waweza kutumika na watu wengi jambo ambalo linaweza kusababisha
maambukizi ya kifua kikuu.
"Lakini
pia, maji yanayotumika kutengeneza wakati mwingine yana vijidudu vya amoeba au
minyoo, wanywaji wengi hupata maradhi haya na kuharisha" anasema Mfamasia
Lymo.
Pia,
ripoti hiyo imeonyesha kuwa, bara la Afrika linaongoza kwa kuwa na wanywaji
sugu wa pombe duniani ambapo asilimia 25 kati yao ni wale wanaokunywa kupita
kiasi.
Utafiti
uliofanywa na Dk Joseph Saria na wenzake kuhusu kiwango cha pombe za kienyeji
na madhara yake kiafya nchini Tanzania, umeonyesha kuwa, pombe nyingi za
kienyeji zinachanganywa na kemikali ambazo zina madhara ya kiafya kwa wanywaji.
Kwa
mfano pombe kama choya, dadii, mnanasi, mbege, moonshine na gongo mchanganyo
wake huzalisha sumu kama Methanol, Butanol, Acetaldehyde na Furfural.
Katika
utafiti huo uliochapishwa Julai mwaka jana katika Jarida la Sayansi(TAJNAS)
imeelezwa kuwa unywaji wa pombe hizi za kienyeji unasababisha maradhi ya
saratani hasa ya koo na mdomo , ini, wakati pombe zenye kiwango kikubwa cha
furfural zinatajwa kuwa na sumu inayosababisha uvimbe katika ubongo, maradhi ya
ini na figo.
"Pombe
nyingi za kienyeji huchanganywa majumbani na pasipo kupimwa hivyo uwezekano wa
kuwa na sumu kali zenye madhara ni mkubwa," inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Pia
ripoti hiyo inaeleza kuwa Watanzania wengi hukimbilia pombe za kienyeji kwa
sababu ya unafuu wake wa bei, ukilinganisha na pombe zinazotengenezwa viwandani
ambazo ni ghali.
Lakini
pia, utafiti huo ulionyesha kuwa pombe za kienyeji hazitengenezwi vijijini
pekee, bali hutengenezwa kwa wingi katika vitongoji vya miji mikubwa kama Dar
es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza.
Ingawa
Tanzania kuna sheria ya ununuzi wa pombe ambapo pombe inaruhusiwa kuuzwa kwa
mtu mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, hata hivyo sheria hii haihusiki au
haitekelezwi huko vijijini ambako kuna wanywaji wengi zaidi na inasemekana kuwa
watoto wa miaka 10 ambao tayari wengi wao ni walevi wa pombe hizo za kienyeji.
Pia,
unywaji huo unashamiri zaidi vijijini kwa sababu sheria nyingi zinatekelezwa
mjini kwa mfano sheria ya kiwango cha pombe kwenye damu pindi mtu anapoendesha
gari ni asilimia 0.8 au umri wa wauzaji wa pombe katika vilabu. Lakini kwa
vijijini sheria hizo hazifuatiliwi.
WHO
inaeleza kuwa madhara ya pombe kiafya husababisha vifo vya watu milioni 2.5
kila mwaka, ambapo kati yao, vijana 320,000 wenye umri wa miaka kati ya 15 na
29 hupoteza maisha kwa magonjwa yanayosababishwa na unywaji wa pombe.
Pombe
inaelezwa kuwa ni sababu kuu ya tatu duniani kwa kusababisha maradhi na pia ni
chanzo cha matatizo mengi ya kijamii kama uvivu, mashambulizi, kutelekeza
familia na husababisha watu kufanya ngono zisizo salama.
0 comments:
Post a Comment