TOFAUTI na watu wengi wanavyofikiria kuwa lishe ni
kula na kushiba, tafsiri sahihi ya lishe bora ni hali ya mwili kupokea chakula
chenye virutubisho vyote muhimu kwa ajili ya kuujenga, kuukinga na kuupa joto
ili kuuwezesha kufanya kazi vizuri.
Katika semina iliyoendeshwa na Jukwa la Lishe
Tanzania (PANITA) kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari mjini Morogoro
mwishoni mwa wiki, iligundulika kwamba mtu anaweza akala kila siku na kushiba,
lakini akawa hapati kile ambacho mwili wake unahitaji na hivyo akawa na tatizo
la lishe, na kuwa rahisi kuandamwa na magonjwa.
Kwa wengi, imekuwa ikichukuliwa kwamba utapiamlo ni
mwili kupungukiwa na protini na wanga, lakini ukweli ni kwamba ni pamoja na
kupungukiwa vitamini muhimu mwilini na madini. Siku hizi utapiamlo unachukuliwa
pia kama hali ya kula chakula kingi kuliko mwili, unavyohitaji na hivyo mtu
kuwa na uzito uliozidi.
Magonjwa kama upungufu wa damu, goita, kushindwa
kuona vizuri na kuzaa watoto wenye migongo wazi na vichwa vikubwa ni matokeo ya
upungufu (utapiamlo) wa madini kama ya joto na baadhi ya vitamini.
Hata hivyo, tatizo kubwa liko kwa watoto wanaopata
upungufu wa vitamini, madini na virutubisho vyote muhimu ndani ya siku 1,000
tangu mimba zao zitungwe. Hao hupata udumavu, ambayo ni hali ya akili zao
kutokua hadi kufikia kiwango kinachotakiwa.
Madhara ya hali hiyo ni watoto kuwa rahisi
kuambukizwa maradhi, uwezo wao wa darasani kuwa hafifu na hata wakishakuwa watu
wazima, wanakuwa na uwezo hafifu wa kufanya maamuzi ya busara.
Katika muktadha huo, familia na hata serikali
hulazimika kuwatibu watu wanaougua mara kwa mara kutokana na miili yao
kutohimili magonjwa, familia pia hushindwa kuzalisha kutokana na muda mwingi
kumhudumia mgonjwa. Halikadhalika, mtu mwenye utapiamlo, hawezi kuzalisha
ipasavyo kulinganisha na mweye lishe bora.
Takwimu zinaonesha kwamba Tanzania ni ya tatu kwa
kuwa na watoto weye udumavu Afrika, ikiwa nyuma ya Ethiopia na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa takwimu hizo, asilimia 42 ya watoto
nchini umri wa miaka mitano, wanakabiliwa na udumavu nchini, kiwango ambacho
PANITA wanasema ni kikubwa sana. Ili kuondokana na hali hii inashauriwa
kuwekeza katika lishe, kuanzia ngazi ya familia hadi serikali yenyewe.
Taarifa ya kimataifa kuhusu hali ya lishe duniani ya
mwaka jana 2015, inaonesha kwamba unapowekeza Sh 2,183, tarajia kupata Sh
34,928 kutokana na uwekezaji huo.
Takwimu zinaonesha pia kwamba kama elimu ya lishe
itasambaa, gharama za chakula kwa ajili ya kujenga afya bora ya mtu, hususan
watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, si kubwa na vyakula hitajika
vinapatikana kila mahala. Yaani si lazima uwe tajiri kula lishe bora.
Inakadiriwa kwamba haizidi Sh 600 kwa siku kwa ajili
ya kumlisha mtoto mmoja lishe bora. Wataalamu wanasema yai moja la kuku wa
kienyeji mara moja kwa wiki, kikombe kimoja cha maziwa na kula matunda na mboga
za majani mara kwa mara, inatosha kuboresha afya zetu. Hivyo, hatuna budi
tuwekeze katika lishe kwa maendeleo yetu.
0 comments:
Post a Comment