Muda mfupi uliopita spika wa bunge, Anna Makinda amelazimika
kusitisha shughuli za bunge mwanzoni tu mwa hotuba ya kambi rasmi ya upinzani
iliyokuwa ikisomwa na waziri kivuli wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Joseph Mbilinyi aka Sugu.
Kauli kwenye hotuba hiyo iliyobabisha spika wa bunge asitishe
shughuli za leo hadi jioni ilisema,
“Tanzania imegeuka chini ya usimamizi wa wizara ya serikali
hii ya CCM kuwa taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa, kuwangoa kucha na
meno, kuwatoboa macho, kuwamwagia tindikali na hata kuwaua.”
SEHEMU YA HOTUBA HIYO:
MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O. MBILINYI (MB)
KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI
NA MICHEZO KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo
la mwaka 2013)
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Dira ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni
“kuwa na taifa lililohabarishwa vizuri, lina vijana wenye uwezo na malezi bora,
linathamini utamaduni wake na linakuwa mahiri katika michezo ifikapo mwaka
2025.” Aidha, ‘dhamira’ ya wizara hii ni ‘kuendeleza utambulisho wa taifa kwa
kuwezesha upatikanaji mzuri wa habari, kuwawezesha vijana kiuchumi na kukuza
utamaduni na michezo kwa umma kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.’
Mheshimiwa Spika,
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali hii ya
CCM imeshindwa kutekeleza dira na dhamira iliyotajwa katika maandiko ya kisera
ya Wizara. Badala yake, chini ya usimamizi wa Wizara hii, Tanzania imegeuka
kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya matendo ya watawala.
Tanzania imegeuka kuwa taifa linalofungia magazeti
yanayofichua ufisadi, uchafu na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa
viongozi, watendaji na watumishi wa Serikali hii ya CCM. Tanzania imegeuka,
chini ya usimamizi wa Wizara na Serikali hii ya CCM, kuwa taifa linaloteka
nyara wanahabari, kuwatesa kwa kuwang’oa kucha na meno, kuwatoboa macho,
kuwamwagia tindikali na hata kuwaua.
Tanzania sio nchi inayoandaa vijana wake tena. Haiwapi tena
elimu bora wala kuwapatia maarifa, uwezo na malezi bora; ni nchi isiyowawezesha
wala kuwathamini vijana wake; ni nchi inayoruhusu vijana wake kunyonywa na
kutoendelezwa; na ni taifa ambalo limeachia utamaduni utambulisho wake kama
taifa kupotea kabisa. Aidha, katika fani ya michezo ya aina zote, Tanzania
imeporomoka kutoka taifa lililokuwa linaheshimika kimataifa katika miaka ya
sabini na kuwa alichokiita rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ‘kichwa cha
mwendawazimu’ ambacho kila kinyozi anajifunzia kunyolea!
2. UHURU WA UHARIRI NA USALAMA WA WANAHABARI
Mheshimiwa Spika,
Kwa masikitiko makubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inalitaarifu Bunge lako tukufu kwamba sasa Tanzania imeingia rasmi katika
orodha ya fedheha (The List of Shame) ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni
taaluma ya hatari kwa wale wote wanaoitumia kama sehemu ya wajibu wao kwa taifa
na kama ajira yao.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kulinda Waandishi wa
Habari Ulimwenguni (the Committee to Protect Journalists - CPJ) iliyotolewa
mwaka huu 2013, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CPJ mwaka 1992, Tanzania
imeingizwa kwenye orodha ya nchi 20 ambazo ni hatari kwa waandishi wa habari
kufanya kazi zao kutokana na hatari ya kuuwawa kwa mwaka 2012 (20 Deadliest
Countries in 2012). Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ilishikilia nafasi ya 7
ulimwenguni kati ya nchi 20 zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha ya waandishi wa
habari.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, tishio kubwa kwa waandishi wa
habari duniani ni kuuwawa kwa kutekwa na kuteswa na/au kutishiwa maisha. Aidha,
Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni washiriki wakubwa wa mauaji
ya waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa takwimu za CPJ, kati ya waandishi waliouwawa
mwaka 2012, karibu ya 20% waliuwawa ama na maafisa wa serikali au na majeshi
yake. Karibu idadi hiyo hiyo ya waandishi wa habari waliuawa kwa sababu ya
kufuatilia taarifa za kiuchunguzi na za hatari. Taarifa hiyo inaonyesha kwamba
hadi kufikia Aprili 2013, waandishi wa habari wapatao 30 tayari wamekwishauawa
ulimwenguni wakati wakitimiza wajibu wao; wakati mwaka 2012 waandishi wa habari
103 waliuwawa ulimwenguni kote.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya CPJ inaungwa mkono na ushahidi wa matukio mengi
yanayodhihirisha kwamba maisha ya waandishi wa habari wa Tanzania yako hatarini
kutokana na vitendo na vitisho kutoka kwa Serikali na watendaji wake ambao
hawataki kusikia ukweli dhidi yao ukianikwa hadharani. Kudhihirisha kauli hii
tunaomba kumnukuu mwanahabari mahiri na mmoja wa wahanga wa vita dhidi ya
wanahabari na uhuru wa habari hapa nchini, Mzee Ndimara Tegambwage:
“Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi wa jiji la Mwanza,
walikusanywa na wenye uwezo kufanya maandamano makubwa kwa walichoita ‘kupinga
mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo’ na kudai kwamba alikuwa Mkenya na
‘siyo raia wa Tanzania.’ Desemba 2009, mwandishi Frederick Katulanda wa Mwanza,
alivamiwa nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza sauti na kudai kuwa ana nyaraka
za akaunti za benki za Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Walikuwa na mapanga.
Walikuwa wakichagizana kwa kusema, “Kata kichwa! Kata kichwa!” Waliondoka na mafaili.
Walimwachia kilema mguuni na makovu mikononi.
“Mwezi Septemba, 2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu,
katika eneo la Nyambiti, Jimbo la Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza,
mwandishi Frederick Katulanda alivamiwa na kupigwa na watu wapatao 15 waliojiita
“Green Guard” - wa “chama cha kijani.” Katika “kumshughulikia,” Katulanda
anasema, walikuwa wakionyesha kuwa na ujuzi mkubwa wa judo na karate huku
wakidai kuwa anawaandika ‘vibaya’ Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mwaka 2011 mwandishi Richard Massatu alikutwa amekufa katika
eneo la Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari viliripoti kuwa macho yake
yalikuwa yametobolewa na kuwekwa gundi aina ya super glue; mguu wa kushoto na
mbavu vilikuwa vimevunjika. Vyombo vya habari viliripoti kuwa Massatu aliyekuwa
mmiliki na mhariri mkuu wa gazeti la Kasi Mpya (sauti ya umma), alionekana mara
ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa na maofisa wa polisi na usalama katika baa
iitwayo Cross Park katika eneo la Igoma.
“Tarehe 3 Januari, maiti ya mwandishi Issa Ngumba iliokotwa
katika pori la mlima Kajuruheta, kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko katika
mkoa wa Kigoma.Ngumba alikuwa mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Tangu mwezi
uliopita Machi, mwandishi wa habari Erick Kabendera anayeishi Dar es Salaam,
anaishi kwa wasiwasi. Wazazi wake waishio Bukoba, wamehojiwa na ‘ofisa usalama’
kwa kile kilichoitwa ‘uhalali wa uraia wao.’
“Kuuwawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha
Luninga cha ITV, John Lubungo ambaye alikuwa mfuatiliaji mahiri wa habari
zinazohusu wafanyabiashara au biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo
inadaiwa kufanywa na watu wakubwa nchini, wakiwemo vigogo serikalini.
Kuna orodha ndefu ya waandishi wa habari waliotishwa na
wanaoendelea kutishwa; waliopigwa na polisi na askari magereza (Ukonga, Dar es
Salaama) kwa tuhuma mbalimbali; waliotishiwa maisha kwa simu na hata kwa
kufuatiliwa na watu wasiowafahamu.”
Kwa sababu ya uadilifu na kutopenda kujikweza, Mzee
Tegambwage hakutaja shambulio la tindikali na mapanga dhidi yake na mwandishi
mwenzake Saed Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi, ambalo baadae lilifungiwa na
Serikali hii ya CCM.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya
Katiba na Sheria ya tarehe 3 Mei mwaka huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilielezea kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa tishio kwa
maisha ya waandishi wa habari na kwa uhuru wa habari katika nchi yetu.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirejeaRipoti ya Timu Maalum
ya Uchunguzi Iliyoteuliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa Mwandishi
wa Habari Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya
Mufindi, Mkoani Iringa, iliyotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), taasisi mbili huru zinazojihusisha na
masuala ya habari Tanzania.
Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao
“... yanadhihirisha bila wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi waliwavurumisha
waandishi waliotoka Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za CHADEMA
katika kijiji cha Nyololo.
Zaidi ya hapo, Daudi
Mwangosi mwenyewe aliuawa akiwa mikononi mwa polisi huku wakisimamiwa moja kwa
moja na Kamanda (wa Polisi wa Mkoa wa Iringa SACP Michael) Kamuhanda.” Ripoti
hiyo inaelezea jinsi Marehemu Mwangosi alivyouawa: “Alipoangalia nyuma, Daudi
Mwangosi aliona kikundi cha polisi wakimpiga mwandishi mkuu wa gazeti la
Nipashe wa Iringa, Godfrey Mushi.... Wakati mwandishi Godfrey Mushi akiwa bado
anapigwa na polisi, marehemu Mwangosi aliwakimbilia akiwaomba waache kumdhuru
zaidi Mushi kwa kuwa alikuwa mwandishi tu.
Polisi hawakumsikiliza. Badala yake wakamburuta mwandishi
huyo ambaye tayari alikuwa amepoteza fahamu na kumweka kwenye gari lao na
wakamgeukia Daudi Mwangosi mwenyewe, wakampiga kwa nguvu mpaka akapoteza
fahamu.”
Hata amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga Mwampamba
kuwataka askari polisi waache kumpiga marehemu Mwangosi haikusikilizwa na
askari hao. Ili kujiokoa, marehemu Mwangosi alimkumbatia OCS Mwampamba na
“baadaye kumwangukia miguuni mwake kuepuka kipigo zaidi.”
Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, “picha za mgando zinaonyesha
polisi mmoja akipiga bomu la machozi tumboni mwa marehemu Mwangosi kwa karibu
kabisa.” Bomu hilo liliusambaratisha mwili wa marehemu Mwangosi aliyekufa papo
hapo. Kwa sababu marehemu Mwangosi alikuwa chini ya miguu ya OCS Mwampamba, “naye
pia alijeruhiwa vibaya.”
Mheshimiwa Spika,
Sio MCT/TEF pekee zilizofanya uchunguzi wa mauaji ya Marehemu
Mwangosi. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo ilitoa Taarifa ya Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea Kifo
cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo, iliyobaini
kwamba Marehemu Mwangosi “... alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye ...
alipigwa bomu na kufa papo hapo.” Aidha, kwa mujibu wa Taarifa hiyo, “...
Tume imejiridhisha kuwa tukio la lililopelekea kifo cha Daudi
Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi
ya utawala bora.” Taarifa ya Tume inafafanua kuwa, “...
Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki ... ya
kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele ya sheria na haki ya
kukusanyika na kutoa maoni.”
Mheshimiwa Spika,
Inaendelea..
Spika amesitisha bunge hilo ili kupata muda wa kuipitia
hotuba hiyo kuondoa kauli za uchochezi.


0 comments:
Post a Comment