Image
Image

EXCLUSIVEL: UFAHAMU UGONJWA WA KISONONO KWA UNDANI KUPITIA KIPENGELE MAHUSUSI CHA AFYA NA MAISHA NA VILE VILE KUPITIA CITY FM RADIO 91.7 UTAPATA KUFAHAMU MENGI.


Hujambo mpenzi msomaji wa makala haya karibu Ujumuike  nami katika makala haya ya Afya na maisha.

Leo nitazungumzia magonjwa ya kisonono na mambo mengine kwa kuelezea matibabu ya ugonjwa huo, karibuni.

Kabla ya kueleza tiba ya ugonjwa wa kisonono ni muhimu kufahamu kuwa, wanawake wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ugonjwa huu kwa asilimia 60 hadi 80, huku wanaume wakiwa katika hatari ya kupata ugonjwa huo kwa asilimia 20.

Hii ni katika hali ambayo, kama tulivyoashiria huko nyuma dalili za ugonjwa huo huwa hazijitokezi kwa uwazi kwa wanawake ikilinganishwa na wanaume na pia ugonjwa huu una madhara zaidi kwa wanawake kwani hata huweza kuwaletea madhara watoto wao wachanga pale wanapojifungua.

Hayo yote yanaonyesha umuhimu wa kutibiwa ugonjwa huo mapema hasa kwa wanawake.

Kisonono ni ugonjwa wa zinaa unaowapata watu wengi na Shirika la Afya Duniani WHO linakadiria kuwa watu milioni 106 duniani huambukizwa ugonjwa huo kila mwaka.
Lakini je, tiba ya ugonjwa wa kisonono ni ipi? Tiba ya gono inahusishwa na tiba ya ugonjwa wa chlamydia kwani mara nyingi magonjwa haya mawili ya zinaa huambatana pamoja.

Matibabu ya kisonono pia hutegemea umri wa mgonjwa na kama ni mwanamke, ni mjamzito au la, Kwa bahati mbaya kuhusiana na matibabu ya ugonjwa huo kumeripotiwa ongezeko la kutosikia dawa vijidudu na hivyo baadhi ya dawa zilizokuwa zikitumika huko nyuma hivi sasa zimekuwa hazina tena athari na hivyo hazitumiki tena.

Kisonono ambacho sio sugu kilicho kwenye shingo ya kizazi (cervix), urethra na puru, hutibiwa kwa dawa za cephalosporin, ambapo mgonjwa hupewa dozi moja ya dawa hizo pamoja na dawa aina ya macrolide kwa mfano azithromycin, na za jamii ya penicillin kwa mfano doxycyclin kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa chlamydia.

Mara nyingi kwa wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka 18 na wanawake wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa sindano.

Mgonjwa hutakiwa kufuata ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa hizo kwani dawa nyingi huwa na madhara kwa wajawazito kwa mfano doxycyclin.

Kwa kawaida ushauri nasaha hutolewa kwa washirika wote wawili wa ngono, na ni vizuri wote wawili watibiwe hata kama mmoja wao hatakuwa na dalili za ugonjwa huu.

Mara nyingi madaktari huwapatia wale wanaosumbuliwa na kisonono dozi pia kwa ajili ya wapenzi wao hata bila ya kupimwa.
&&&&&
Baada ya kufahamu namna ya kutibu gono, sasa tuangalie madhara ya ugonjwa huo.

1.   Moja ya madhara anayoweza kupata mtu kutokana na ugonjwa wa kisonono ni, mwanamke kutoweza kuzaa yaani kuwa mgumba au mimba kutoweza kutunga.

Tunaelezwa kuwa magonjwa ya zinaa ya chlamydia na gono yana mchango katika kusababisha wanawake kutozaa kwani magonjwa hayo kwa asilimia 10 hadi 15 huweza kusababisha uvimbe katika fupanyonga au Pelvic Inflammatory Disease (PID) na hasa kwa kuwa wanawake wengi wenye kisonono huwa hawaonyeshi dalili.

Ugonjwa wa PID husababisha makovu katika mirija ya uzazi hali ambayo husababisha kushika mimba kuwa kugumu na matatizo wakati wa ujauzito. PID ni ugonjwa unaopaswa kutibiwa haraka.

Kwa upande wa wanaume ugonjwa wa kisonono pia huweza kuwafanya wanaume wasipate watoto kwani huwasababishia uvimbe katika sehemu ya mbele ya korodani ambako mbegu za kiume hutengenezwa,   Uvimbe huo usipotibiwa husababisha utasa.

Ugonjwa wa gono pia huweza kuathiri moyo, ubongo, ngozi na kadhalika kwa hivyo ni hatari sana kwa mtu yoyote na unahitaji kutibiwa mapema. 

Pia ugonjwa huo huleta madhara au uvimbe kwenye maungio ya viungo, ambapo vimelea vinavyosababisha kisonono huweza kusambaa kwenye damu na kuleta maambukizo kwenye sehemu nyinginezo mwilini.

Maambukizo hayo huleta homa, vipele, vidonda kwenye ngozi, maumivu ya viungo na uvimbe. 

Vilevile wanawake ambao ni wajawazito na wameambukizwa gono wako kwenye hatari ya mimba kutoka au kuzaa mapema kabla mimba haijatimiza umri wake (preterm labor). 

Kwa wale wanaoambukizwa gono kipindi cha kukaribia kujifungua, wanaweza kuwaambukiza watoto wao na hivyo watoto kupata ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis), kuwa vipofu, homa ya mapafu (pneumonia) na ugonjwa wa mifupa (septic arthritis).
&&&&&

Bila shaka baada ya kusikia hayo tuliyoyaeleza kuhusu ugonjwa wa kisonono, unajiuliza tunawezaje kujikinga na ugonjwa huo. 

Mpenzi msomaji unaweza kujikinga na gonjwa hili la zinaa kwa njia zifuatazo. 

Kwanza kabisa ni kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha na uasherati. 

Kuchukua tahadhari na kuzungumzia juu ya ugonjwa huo na dalili zake ili kuweza kufahamu kuwa mshirika wako wa ngono ana ugonjwa huo au la, na iwapo anao hatua inayofuata ni kutibiwa na kupata ushauri wa daktari. 

Njia nyingine ya kujikinga ni kuepuka kufanya ngono na mtu aliyeambukizwa gono. 

Vilevile kutumia mipira ya kiume wakati wa kujamiiana, na wanawake wajawazito wanapaswa kuhakikisha kuwa wanahudhuria kliniki mapema ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa tiba muafaka iwapo watagundulika kuwa na ugonjwa wa gono au ugonjwa mwingine wowote.

Wanawake wajawazito wanashauriwa kujifungua hospitalini ili kama mtoto ameathirika na gono apate matibabu ya haraka baada ya kuzaliwa ili kuepusha kuwa kipofu.
&&&&&

Tunahitimisha makala hii kwa  taarifa inayotujuza kuwa aina mpya ya kisonono imesambaa duniani. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, aina mpya ya vimelea vya ugonjwa wa gono ambavyo vinahimili dawa zinazotumika duniani kutibu ugonjwa huu vimegunduliwa. 

Taarifa iliyotolewa na WHO inasisitiza hatari ya kuwa sugu ugonjwa huo unaowaathiri mamilioni ya watu duniani. 

Shirika la Afya Duniani limetoa wito kwa serikali na madaktari kuongeza ufuatiliaji wa aina hii ya kisonono kutokana na ugonjwa huo kuwa na madhara mengi kama ugumba, matatizo wakati wa ujauzito na hata vifo vya kina mama wajawazito. 

Dakta Manjula Lusti-Narasimhan, mmoja wa wanasayansi wa Shirika la Afya Duniani katika kitengo cha magonjwa ya zinaa amesema kuwa, aina hii mpya ya vimelea vya kisonono inaonyesha usugu dhihi ya dawa zote za antibiotiki tunazotumia kuviangamiza, zikiwemo dawa jamii ya cephalosporin ambazo ni dawa za mwisho katika kutibu ugonjwa wa kisonono. 

Dakta Manjula Lusti-Narasimhan ametahadharisha kwamba, katika miaka michache ijayo, aina hii mpya ya kisonono huenda ikawa sugu kwa dawa zote ambazo zinapatikana kwa sasa na kwamba ugonjwa sugu wa kisonono sio tatizo la bara la Ulaya au Afrika pekee bali ni tatizo la dunia nzima. 

Kwa mara ya kwanza, vimelea sugu vya ugonjwa wa kisonono dhidi ya dawa za cephalosporin viliripotiwa katika nchi ya Japan, ikifuatiwa na Uingereza, Hongkong na Norway. 

Wanasayansi wanaamini kuwa, matumizi holela ya dawa aina ya antibiotiki pamoja na uwezo wa vimelea vya ugonjwa huo  hubadilika na kuzoea mazingira mapya ndio chanzo kikuu cha kuwa sugu kisonono na hivyo muda si mrefu ugonjwa huu unaweza kuwa janga kubwa dunia kama hatua za haraka hazitachukuliwa. 

Kuna uwezekano wa vimelea hivi sugu vya kisonono kusambaa kwa haraka duniani bila kugundulika kutokana na nchi nyingi kutokuwa na ufuatiliaji na utunzaji kumbukumbu mzuri wa wagonjwa wake. 

WHO imezitaka nchi zote kuongeza ufuatiliaji wa wagonjwa wake pamoja na kudhibiti matumizi holela ya dawa za antibiotiki mpaka pale taarifa kamili za ugonjwa huu zitakapojulikana.

Msomaji wa makala Haya kumbuka kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha na ngono zembe na uasherati ni suala linasisitizwa sana sio tu katika kujikinga na kisosono bali na magonjwa mengine ya zinaa au STD.

Kwani kwa kawaida kama hujapimwa huwa vigumu kutambua iwapo wewe au mwenzako ameathirika au la, na kama una michibuko au umekatika kwenye ngozi unaweza kupata maambikizo ya magonjwa hayo. 

Ushauri wa Bure Njia pekee na nzuri ni kuacha ngono zembe au uasherati hivyo tunapaswa kufahamu kuwa mtu aliyepata gono mara moja anaweza kupata tena. Tunaishia hapa kwa leo, tudumu katika kheri na kwaherini.

MTAALAMU WA MAGONJWA HAYA NI  SADICK FACK, PAMOJA MITANDAO MBALI MBALI ILIYOSAPOTI KWA HILI.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment