Image
Image

DK KIGWANGALLAH KUWATAJA MABOSI WA AKINA MASOGANGE KATIKA KIKAO CHA BUNGE, NI SAKATA LA USAFIRISHAJI NA UINGIZAJI WA DAWA ZA KULEVYA NCHINI.



VITA dhidi ya usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia katika viwanja vya ndege nchini iliyoanzishwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, imemvuta Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamis Kigwangallah, ambaye ameahidi kutaja majina wauzaji wa dawa hizo ili kuisadia serikali kuchukua maamuzi magumu.

Dk. Kigwangala aliliambia NIPASHE jana kwa njia ya simu kuwa hadi sasa amepokea majina saba ya vinara wanaojihusisha na biashara hiyo na kwamba anaendelea kupokea ushahidi ukiwamo wa picha za watu hao wanawauzia kina nani na wanakaa wapi.

Mbunge huyo amesambaza taarifa kupitia mitandao ya jamii ikiwamo Facebook akiwataka wananchi wenye taarifa za wauza unga kuwasiliana naye na kumpa ushahidi ili awataje bungeni katika mkutano wa 11 wa Bunge unaoanza kesho.


Alisema zoezi la kupokea majina hayo na ushahidi linakwenda vizuri na kwamba mwitikio umekuwa mkubwa kutoka kwa wananchi na kusisitiza kwamba lazima awataje wahusika kwa majina.

Aliongeza kuwa ameandika barua kwa Spika wa Bunge kuomba fursa ya kutoa maelezo bungeni kama mbunge na kwamba atampelekea barua nyingine ili apatiwe nafasi ya kusimama na kutaja majina hayo.

“Mimi siogopi kitu, nikipata ushahidi wa kina nitataja majina ya watu wote waliotajwa na wananchi wanaoniletea ushahidi na katika hili moja ya jina ni la kinara anayetajwa tajwa sana,” alisema Dk. Kigwangallah.

Aliwataka wananchi wenye taarifa zinazojitosheleza kumtumia ili azifanyie kazi kabla ya kuwataja bungeni.

Alisema shinikizo la wanasiasa linaweza kusaidia kuiamsha serikali kupitia Jeshi la Polisi kuanza kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.

MTAMBO MPYA WAFUNGWA JNIA
Kufuatia malalamiko kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Umegeuzwa uchochoro wa kupitishia dawa hizo kwenda nje, Serikali imefunga mtambo mpya ya kisasa utakazokuwa na uwezo wa kutambua zitakazoingizwa au kupitishwa kutoka ndani na nje nchi.

Dk. Mwakyembe jana alifika katika uwanja huo kukagua mtambo huo wa Rapscan 600 series na kuelezwa na viongozi kuwa umetoka Uingereza na kufungwa kwenye uwanja huo kuanzia wiki iliyopita.

Dk. Mwakyembe akizungumza na NIPASHE katika uwanja huo baada ya kumaliza kukagua mtambo huo, alisema lengo la serikali kuongeza mtambo mwingine ili  kukomesha kabisa tatizo la watu wasiokuwa waaminifu kupitishia dawa hizo katika uwanja huo na kuliletea aibu Taifa.

Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa upande wake nayo imefunga mitambo yake kwa  lengo la kukabiliana na dawa hizo na kwamba kutoka na ushirikiano uliopo katika ya vyombo vya usalama ni wazi kuwa itakuwa vigumu kwa mtu kuzipitisha JNIA.

Kwa upande wake Meneja Usalama wa JNIA, Clemence Jingu, alimweleza Dk. Mwakyembe kuwa mtambo huo umefungwa kitaalamu na kwamba hatua iliyobaki ni kufungwa kifaa kijulikanacho kama Soft narc scan.

Jingu alisema katika uwanja huo wameanzisha huduma ya kukagua mizigo ya abiria wanaoingia nchini kutoka nchi mbalimbali nyakati za usiku  ambayo awali haikuwapo .

Agosti 16, mwaka huu Dk. Mwakyembe aliwataja maofisa usalama wanne wanaodaiwa kuhusika katika njama za kusafirishwa dawa za kulevya na kuigiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kuwafuka kazi na kufunguliwa mashtaka.

Alichukua hatua hiyo kufuatia kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 kukamatwa Julai 5, mwaka huu nchini Afrika Kusini zikitokea Tanzania, kupitia JNIA.

Maofisa usalama hao ni Yusufu Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana.

Pia aliliagiza Jeshi la Polisi kumuondoa mara moja katika uwanja huo, askari wake, Ernest na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwenye njama za kupitisha mabegi sita ya dawa hizo yaliyokamatwa Afrika Kusini.

Pia alisema polisi inapaswa kumsaka Nassoro Said Mangunga aliyevikwepa vyombo vya dola Afrika Kusini na kutoroka na mabegi matatu ya dawa hizo.

Alisema mbeba mizigo katika uwanja huo, Zahoro Mohamed Seleman, anapaswa kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ili kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka ya jinai.

Dk. Mwakyembe pia aliiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu siku ya tukio, kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wakati mwafaka kukagua mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya.

Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 wamekamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.

Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini na kuharibu taswira ya nchi na kusababisha wenzao wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.

Wiki moja baada ya tukio la wasichana hao kukamatwa, Watanzania wengine wawili walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa hizo aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hong Kong. 

CHANZO: NIPASHE



Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment