Image
Image

Balozi Seif aitaka polisi jamii kupunguza uhalifu nchini




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba mamlaka yaliyomo ndani ya kamati za Polisi Jamii katika maeneo mbali mbali nchini yanaweza kusaidia kupunguza maovu endapo zitapata ushirikiano mzuri kutoka kwa kila mwana jamii.
Alisema wananchi wanapaswa kuzitumia kamati hizo kwa kutoa taarifa za maovu wanayoyashuhudia katika maeneo yao bila ya kuogopa ili kudumisha hali ya amani na utulivu.
Balozi Seif alisema hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo jipya la ofisi ya Polisi Jamii ya Shehia ya Chambani Jimbo la chambani Wilaya ya Mkoani ambalo linajengwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe pamoja na michango ya washirika wa maendeleo.
Alisema wahalifu wamo ndani ya jamii na suala la ubakaji kwa sasa linaonekana kutishia amani ya jamii mambo ambayo kama hakukuwa na nguvu za pamoja kati ya Wananchi, viongozi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi katika kukabiliana na vitendo hivyo hatma ya watoto itakuwa mashakani.
“ Wananchi wahakikishe kwamba amani na utulivu wa maeneo na Taifa zima inadumu kwa kuvitumia vikundi vya polisi Jamii na ulinzi shirikishi kwenye maeneo wanayoishi “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba kuporomoka kwa maadili ndio sababu kubwa inayochangia kesi za ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia unaowakumba zaidi wanawake na watoto wadogo.
Alisema wananchi na jamii nzima wakati wote ingependa kuona inaendelea kuishi kwa amani, utulivu na upendo bila ya bughudha yoyote ambapo inaweza kudhibitiwa kwa nguvu za pamoja.
Balosi Seif aliwapongeza wananchi wa Shehia ya Chambani kwa uwamuzi wao wa kuanzisha kikundi cha polisi jamii na ulinzi shirikishi jambo ambalo kupitia kamati yao limesaidia kupunguza wimbi la maovu na matatizo yanayoleta kero jamii.
Katika kuunga mkono nguvu za wanancnhi hao wa shehia ya Chambani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameahidi kuchangia mifuko mia moja ya saruji, matofali ya kumalizia linta pamnoja na matari 50 ya kuezekea.
Ahadi hiyo ilikwenda sambamba na zile zilizotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mh. Faida Moh’d shilingi Laki 500,000/-, Mwakilishi wa Viti Maalum Mh. Shadia Mohd Suleiman Shilingi Laki 500,000/- pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid Shilingi Laki 400,000/-.
Mapema akisoma Risala ya wana Kikundi hicho cha Polisi Jamii cha Shehia ya Chambani Ofisa Polisi Jamii wa Jimbo la Chambani Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Salma Twaha alisema Polisi jamii ni mikakati ya njia stahiki ya kulinda amani ya Nchi katika misingi ya kutekeleza wajibu kwa hiari.
Kamanda Salma Twaha alisema Polisi Jamii ndani ya Jimbo hilo iliyoanzishwa na kuundwa kwa Kamati ya Uongozi wa Kikundi hicho mwaka 2011 imefanikiwa kwa kiasi kikubwa malengo iliyojipangia.
Alisema hadi sasa tayari Kamati ya Ulinzi wa Jamii ya shehia ya Chambani imeshapokea na kusikiliza kesi 240 ambazo zote zimeshatolewa maamuzi yenye kuleta faraja ndani ya shehia hiyo.
Alifahamisha kwamba Wananchi kupitia uongozi wa kamati yao ya ulinzi wa jamii imekuwa ikisimamia pia masuala ya maadili kwa watoto wao sambamba na kupambana na matukio ya vitendo vya wizi.
Akigusia suala la ujenzi wa kituo cha polisi Jamii cha Shehia ya Chambani Kamanda Salma Twaha alisema jengo hilo lililofikia hatua ya linta linatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi Milioni Mia 105,185,500/- hadi litakapomalizika.
Akimkaribisha Balozi Seif Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid amewahimiza wnanachi hasa vijana wa Jimbo hilo kujikusanya pamoja katika vikundi vya ushirikia ili kupata nguvu za kujiajiri na kupunguza ukali wa maisha.
Mh. Mwanajuma alisema matatizo mengi hasa vitendo vinavyofanywa na vijana waliowengi vinatokana na ukoksefu wa kazi za kufanya jambo ambalo huwasababishia kujiingiza katika matendo maovu.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliweka jiwe la msingi la jengo jipya ya skuli ya msingi ya Ngomeni akiendelea na ziara yake ndani ya Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumza na wananchi, walimu na wanafunzi wa Skuli ya Ngomeni Balozi Seif ameipongeza jamii ya Kijiji hicho kwa uwamuzi wao wa kuwaondoshea usumbufu wa kufuata elimu masafa marefu watoto wao.
Balozi Seif alisema azi iliyofanywa na wazazi wa Kijiji cha Ngomani ya ujenzi wa wa jengo hilo ni wa jisariri na unafaa kuigwa na wananchi wengine ambao maeneo yao bado hayajawa na skuli.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibarinaendelea kutafakari ule mpango uliowekwa kwa wazee kuchangia huduma za skuli baada ya kazi hiyo kufanywa na Serikali tokea mwaka 1964 ambapo kwa sasa ililazimika kupata kuungwa mkono na wazazi wa watoto nchini.
Balozi Seif alihahamisha kwamba uwezo wa Serikali kuu ukiruhusu tena jukumu hilo litaendelea kubebwa na Serikali kama Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Karume alivyotangaza kwamba watoto wote wa Visiwa hivi watapata elimu bila ya malipo.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wananchi wa Kijiji cha Ngomeni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaeleza wananchi hao kwamba Serikali itajitahidi kutatua kero zinazowakabili wananchi hatua kwa hatua kadri hali itakavyoruhusu.
Alisema malengo na sera za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar toke ilipoasisiwa mara baada ya Mapinduzi ya Januari mwaka 1964 ni kuwaondoshea kero wananachi wake na kustawisha maisha yao.
Balozi Seif alisema juhudi zitafanywa katika kuona wananchi hao wanapata huduma za maji safi na salama sambamba na uimarishaji wa miundo mbinu ya bara bara iendayo kijijini huko.
Aliwataka wananchi hao kujizatiti katika kuanza ujenzi wa kituo cha afya na yeye atakuwa tayari kuongeza nguvu za ujenzi baada ya wananchi hao kuanza kwa hatua ya msingi.
Mapema Balozi Seif na msafara wake alipata wasaa wa kukagua mradi wa vitalu vya Serikali vya miche nya mikarafuu unaosimamiwa na kuendeshwa na Wizara ya Kilimo na Mali asili kiliopo Chanjaani Mwatoro Wilaya ya Chake Chake.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Nd. Afan Othman Maalim alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uoteshaji wa miche ya mikarafuu umeongezeka kutokana na kasi ya wakulima wa zao hilo kuhamasiska kutokana na kupanda kwa bei ya zao hilo katika soko la Dunia.
Nd. Afan alisema licha ya wizara ya Kilimo kujiwekea malengo ya kuotesha miche ya mikarafuu milioni moja kila lakini inaonekana wazi kwamba mahitaji halisi ya miche hiyo kwa wakulima bado haijafikiwa.
Hata hivyo katika kwenda na ufanisi wa mradi huo maafisa wa Kilimo hulazimika kufanya utafiti katika mashamba ya wakulima wanaoomba miche hiyo ambayo hutolewa bure na baadaye kuwapatia ushauri mzuri wa kitaalamu ili kwenda sambamba na mafanikio ya mpango huo.
Balozi Seif alionyesha kuridhika kwake na hatua iliyochukuliwa na Wizara ya Kilimo katika kulifufua zao la Mikarafuu hapa Zanzibar ambalo lilififia katika miaka ya karibuni baada ya kuporomoka kwa bei yake.
Aliushauri uongozi wa Wizara hiyo ufanye jitihada na uchunguzi wa kufufua tena mradi wa upandaji upya wa minazi ambayo ni bidhaa inayokubalika vyema katika masoko ya kimataifa hasa katika sekta ya utalii.

Othman Khamis Ame 

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment