Image
Image

Rais Kikwete,Nkurunzinza wazindua treni za mizigo kwenda Burundi, Uganda na DR Congo.


Rais  wa jamhuri ya muungano wa Tanzania  Jakaya Kikwete na mwenzake Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi wamezindua safari za treni tatu za mizigo ‘block train’ kutoka Dar es Salaam kwenda Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Uzinduzi wa treni hizo zenye mabehewa 15 hadi 20 ulifanyika jana jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuzindua mkutano wa marais wanachama wa nchi zinazounda ukanda wa kati.
Marais waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili ni Rais Yoweri Museven wa Uganda, Rais wa Kenya aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Amina Mohamed, Rais wa DRC aliwakilishwa na Waziri wa Usafirishaji, Justine Kanumba huku Rais wa Rwanda, akiwakilishwa na Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo, James Musoni.
Akizindua treni hizo, Rais Kikwete alisema, “kuanzia sasa zitakuwa zikibeba mizigo ya nchi moja pekee yake kwa wakati mmoja, kama ni mizigo ya Burundi itakuwa Burundi tu vivyo hivyo kwa DRC na Uganda, kinyume na ilivyokuwa awali.
“Awali safari za treni za mizigo zilikuwa zikichukua wiki mbili kufikisha mizigo kwenye nchi husika, lakini sasa itakuwa inachukua siku mbili pekee,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake Rais Nkurunziza alisema Tanzania imefanya jambo la maana kuisaidia nchi yake ambayo ipo mbali na bahari. “Safari hizo zitasaidia kusafirisha mizigo mingi na kwa njia ya kwa haraka.”
Vikwazo vya usafirishaji
Awali akifungua mkutano wa Ukanda wa Kati wa Kibiashara jijini hapa, Rais Kikwete alisema Tanzania imeshapiga hatua kubwa katika kuhakikisha inaondoa vikwazo vyote vya usafirishaji mizigo kwenda nchi jirani, ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vizuizi barabarani.
“Tumeamua kupunguza vizuizi vya polisi barabarani kutoka 15 hadi vitatu na vituo vya mizani kutoka 10 hadi vitatu vitakavyojengwa vigwaza mkoani Pwani, Manyoni (Singida) na Nyakahura (Kagera),” alisema Rais Kikwete.
Alisema ni jukumu la nchi kuonyesha kuwajibika katika mradi huo kwa kuwa sehemu kubwa ya mradi ipo nchini, hivyo ni vyema kuhakikisha nchi jirani zinasafirisha mizigo yao kutoka bandari ya Dar es Salaam bila tatizo.
“Kama ambavyo nimesema inatuwezesha kukuza biashara za ndani na kimataifa na kukuza uchumi.”
Katika mradi huo, kilomita 2,707 za reli hiyo zipo Tanzania, barabara ni kilomita 2,406, pia bandari kubwa tatu za Dar es Salaam, Kigoma na Mwanza zipo Tanzania.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment