Image
Image

Hukumu ya kina Mramba,Yona hatima yao hii leo Kisutu.


Waziri wa zamani wa fedha,Basil Mramba(Kushoto) waziri wa zamani wa nishati na madini Daniel Yona(Katikati)na aliyekuwa katibu mkuu wa wizara ya Fedha,Grey Mgonja wakiwa ndani ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakati wakisubiri kuendelea kwa kesi yao ambapo wote wanatuhumiwa kwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Shilingi 11.7Bilioni wakati wa uongozi wao(Picha kwa hisani ya Maktaba Yetu).

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, leo inatarajia kutoa hukumu dhidi ya mawaziri waandamizi wa zamani,  Basil Mramba, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja wanaokabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS), Government Business Corporation kufanya ukaguzi wa madini ya dhahabu nchini.

Hukumu hiyo itasomwa mbele ya jopo la mahakimu watatu, wakiongozwa na Mwenyekiti, Jaji John Utamwa, Jaji Samu Rumanyika ambao walianza kusikiliza kesi hiyo kabla ya kuteuliwa kuwa majaji wakisaidiana na Hakimu, Saul Kinemela.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mahakama hiyo kusikiliza ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na wawashtakiwa.
Baada ya mahakama hiyo kusikiliza ushahidi huo, iliwaona washtakiwa hao wana kesi ya kujibu na kuwataka kujitetea kwa nyakati tofauti.

Baada ya kukamilisha utetezi wao na kuupitia mahakama leo inatarajia kutoa hukumu dhidi yao.

Kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, kosa la matumizi mabaya ya madaraka adhabu zake ni kulipa faini ya Sh. milioni 2 au kifungo cha kati ya mwaka mmoja au miaka mitatu jela baada ya mshtakiwa kupatikana na hatia.

Katika mashtaka hayo ilidaiwa kuwa washtakiwa wakiwa watumishi wa serikali, Oktoba 10, mwaka 2003 walikaidi ushauri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kuwataka wasitoe msamaha kwa Kampuni ya Alex Sterwart (Assayers) Government Business Corporation.

Novemba 25, mwaka 2008, washtakiwa hao, walifikishwa katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hezron Mwankenja na kusomewa mashitaka 13, likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka.
Kesi hiyo ilipangiwa jopo hilo na kuanza kuisikilizwa mapema mwaka 2009.

Katika shitaka la kwanza, ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Joseph Ole, kuwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri walitumia vibaya madaraka.

Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa kudhibiti madini ambapo kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation waliingia mkataba na kampuni tanzu kukagua uzalishaji wa madini ya dhahabu, kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mramba na Yona wanadaiwa kuwa Mei 28, mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma jijini Dar es Salaam, wakiitumikia serikali katika nafasi za uwaziri wa Fedha na Nishati na Madini, kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mikataba ya kuiongezea kampuni hiyo muda wa miaka miwili wa kuendelea kukagua madini kuanzia Juni 2005 hadi Juni 2007 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma. 

Ole aliendelea kudai kuwa, katika shitaka la tatu wote wawili wanadaiwa kuwa kati Machi na Mei mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao kwa kumualika Dk. Enrique Segura wa M/S Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation kuja kusaini mkataba wa nyongeza wa miaka miwili kabla timu ya majadiliano ya serikali haijaanza kulifanyia kazi suala hilo.

Katika shitaka la nne, kati ya Machi na Mei mwaka 2005, washitakiwa wanadaiwa kuwa walitumia nyadhifa zao vibaya kwa kukaidi kupeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali suala la kodi kama ilivyopendekezwa na Timu ya Serikali ya Majadiliano, jambo ambalo lilisababisha mkataba uongezeke kwa miaka miwili bila kupitishwa na timu ya majadiliano. 

Shitaka la tano, ilidaiwa kuwa Oktoba 10, mwaka 2003, Mramba akiwa Waziri wa Fedha, alidharau mapendekezo ya TRA ya kutotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Katika shitaka la sita, Mramba anadaiwa kati ya 18 na 19 Desemba mwaka 2003, akiwa Waziri wa fedha, alitoa kibali namba GN 423/2003 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume cha mapendekezo yaliyopendekezwa na TRA.

Shitaka la saba, anadaiwa kuwa Desemba 19, mwaka 2003  akiwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka vibaya kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Shitaka la nane, Oktoba 15, mwaka 2004 akiwa Waziri wa Fedha, alitoa kibali namba GN 497/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Shitaka la tisa, anadaiwa kuwa kati ya Oktoba 14 na 15, 2004, alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 498/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA. Shitaka la 10, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, mwaka 2005 alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 377/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Shtaka la 11, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, 2005, alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 378/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Shitaka la 12, Mramba na Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni 2003 na Mei 2005, wakiwa na nyadhifa hizo za uwaziri kwa makusudi na kutowajibika waliruhusu mkataba wa kuzuia kulipa kodi ili kuipendelea kampuni hiyo na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 11,752,350,148.00.

Katika shtaka la mwisho, Mramba anadaiwa kuwa kati ya 2003 na 2007, akiwa Waziri wa Fedha kwa makusudi alishindwa kuwa makini au kutotimiza wajibu wake kwa kusaini vibali vilivyotajwa katika mashtaka hayo, kuruhusu kampuni hiyo kutokulipa kodi na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa kwa nyakati tofauti walikana mashitaka yote na kupelekwa rumande katika Gereza la Keko baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Masharti hayo ni kujidhamini kwa kiasi cha Sh. bilioni 3.9 kila mmoja, kuwasilisha hati zai za kusafiria mahakamani na kutokutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam, bila kibali cha Mahakama hiyo.

Pia, walitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminiwa kwa kila mshitakiwa.

Hata hivyo, baada ya kutimiza masharti yao, waliachiwa kwa dhamana hadi leo, hukumu dhidi yao itakaposomwa.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment