Bila kutarajiwa, Mkapa ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya tatu,
alisikika akiwaita wapinzani kuwa ni ‘wapumbavu’ na ‘malofa’. Sababu ya
Mkapa kusema yote hayo ilikuwa ni kupinga kile anachodai kuwa ni
kitendo cha wapinzani kudai kuwa wanataka kuwakomboa Watanzania wakati
kazi hiyo ilishafanywa kitambo na vyama vya kupigania uhuru.
Sisi tunaamini kuwa maneno yaliyotumiwa na Mkapa ni matokeo ya
kuteleza kwa ulimi. Hatuamini hata kidogo kuwa aliyatumia kwa usahihi.
Hili linatokana na ukweli kuwa wapo watu kadhaa waliokwazika baada ya
kusikia kauli hiyo ya Mkapa kwenye mkutano uliokuwa ukifuatiliwa pia na
mamilioni ya Watanzania kupitia matangazo ya moja kwa moja ya
televisheni. Hakika, ijapokuwa Mkapa alikuwa akishangiliwa na maelfu ya
wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano huo, bado ukweli unabaki kuwa
kauli yake dhidi ya wapinzani iliwaacha wengi midomo wazi. Kamwe
haikutarajiwa kwamba kiongozi huyo mstaafu angefikia hatua ya kutamka
maneno hayo yanayochukuliwa na wengi kuwa ni sehemu ya matusi
yanayopaswa kuzuiwa na mamlaka zinazosimamia uchaguzi mkuu.
Kwakweli,‘mpumbavu’ siyo neno zuri kulitamka dhidi ya wengine.
Halifai kutumiwa kwa namna aliyoitumia Mzee Mkapa. Miongoni mwa maana
zake, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la Tatu
lililotolewa mwaka 2013 na Taasisi ya Ukuzaji Kiswahili (TUKI) na kisha
kuchapishwa na Chuo Kikuu cha Oxford, ni pamoja na ‘juha’, ‘fala’ na
‘zuzu’. Yote haya siyo maneno mazuri yanayofaa kutumiwa kwa namna
aliyoitumia Mkapa kwani yana muelekeo dhahiri wa kukiuka kanuni
inayozuia kauli za kashfa na matusi kwenye mikutano ya kampeni.
Sisi tunapinga matumizi ya maneno ya namna hii kwa sababu kadhaa,mojawapo ikiwa ni ukweli kwamba Mzee Mkapa ni kiigizo cha wengi. Wapo
vijana wanaojaribu kumuiga kila afanyalo kwa kuamini kuwa siku moja
watatimiza ndoto ya kufikia alipo yeye. Hii maana yake ni kwamba
wanaweza pia kuiga maneno hayo wakati wakiwazungumzia watu
wanaotofautiana nao kwa hoja, mtazamo na itikadi. Hatari nyingine ni
ukweli kuwa kauli hii ya Mkapa yaweza kutoa fursa kwa wanasiasa wengine
kufuata mwenendo huo katika kampeni zinazoendelea kuelekea uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba 25. Hili linapaswa kuepukwa.
Kadhalika, ikumbukwe kuwa mtu aliye kwenye nyumba ya vioo hapaswi
kuanzisha ugomvi wa kurushiana mawe kwani anaweza kujiweka katika hatari
ya kupata madhara makubwa pindi wale anaowashambulia watakapojibu
mapigo. Wapinzani wa CCM wasipokuwa na subira wanaweza kujibu mapigo
katika kampeni zao kwa kutoa kauli zinazoumiza zaidi ya zile za Mkapa,
na hapo watakaoathirika ni wananchi ambao huenda wasipate tena wasaa wa
kusikiliza kwa kina sera na ilani za vyama kabla ya kufanya uamuzi siku
ya kupiga kura.
Sisi tunaamini kuwa Mzee Mkapa ameteleza. Tunawasihi wanasiasa
wengine wawe wavumilivu na kuhakikisha kuwa nao hawatelezi kwa namna
iliyoshuhudiwa juzi kwenye viwanja vya Jangwani. Tuzingatie.


0 comments:
Post a Comment