Image
Image

Dk. Bilal aongoza mamia ya watanzania kuuaga mwili wa KOMBANI.

MAKAMU wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal jana aliongoza mamia ya Watanzania waliojitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Mwili wa Kombani uliagwa katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam huku idadi kubwa ya watu wakiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, viongozi wa vyama vya siasa na wabunge wakihudhuria.
Jeneza lenye mwili wa marehemu liliwasili katika viwanja hivyo majira ya saa 5:00 asubuhi, likiwa limebebwa na askari wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliokuwa wamevalia suti nadhifu huku wakisindikizwa na Mawaziri na Manaibu Mawaziri hadi kwenye jukwaa.
Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama alisema, serikali imepata pigo kubwa kutokana na kifo cha Kombani kwani alikuwa ni kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya taifa kupitia wajibu wake na majukumu aliyopewa na serikali.
Alisema pengo aliloacha Kombani haliwezi kuzibika kirahisi kwani mchango wake ulikuwa ukihitajika kwa ajili ya kuendeleza harakati za kuleta maendeleo ya taifa. “Alijitahidi kuwapigania wananchi wa jimbo lake, hakuna ubishi alifanya kazi kubwa kwa wananchi wa jimbo lake.
Amefanya mageuzi makubwa katika sekta ya utumishi na atakumbukwa daima,” alisema Mhagama. Awali akizungumza, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema, Kombani aliwasaidia kuunda muundo mpya wa utumishi wa Bunge ambapo alisema, Agosti 16, mwaka huu walipitia muundo huo kwa mara ya mwisho ambapo Kombani alishiriki.
Alisema wakiwa katika kikao hicho Kombani alitoka nje na baada ya muda alipewa taarifa kuwa anajisikia vibaya. “...Kwa kuwa nilikuwa Mwenyekiti wa kile kikao nikapewa taarifa kuwa Waziri anajisikia vibaya nikawa nimeshangaa kwa sababu tulikuwa naye yuko vizuri, nikawa nimetoka kwenda kumuona,” alisema.
Alisema wakati wakiwa hapo Katibu wa Bunge alimwambia kuwa Waziri anataka apelekwe kwa daktari wake ambapo alipelekwa kwa daktari huyo katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni. Aliwataka waliohudhuria tukio hilo kuchukulia kifo cha Kombani kama somo la kutenda mema kama ilivyokuwa kwa Waziri huyo.
Akitoa salamu za uliokuwa Umoja wa Wabunge Wanawake, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angellah Kairuki alisema, bado mchango wa waziri huyo ulikuwa ukihitaji kwani alikuwa ni mshauri mzuri katika mambo mbalimbali ya umoja huo pamoja na Bunge kwa ujumla.
Alisema umoja huo ulipokea kifo chake kwa mshtuko mkubwa kwani hawakutegemea kama wangempoteza mapema kiasi hicho na hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi ambapo pia alikuwa anatetea jimbo lake la Ulanga Mashariki.
Mwili huo jana ulisafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko ambapo kwa mujibu wa ratiba ya maziko, leo mwili huo unatarajiwa kuwasili katika uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya sala kabla ya kwenda kuhifadhiwa katika nyumba yake ya milele.
Katika sala hiyo itakayofanyika uwanjani hapo, inatarajiwa kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Rais Dk Bilal, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Bunge Makinda na viongozi mbalimbali.
Kombani alifariki Septemba 24, mwaka huu katika Hospitali ya Apollo nchini India na anatarajiwa kuzikwa shambani kwake, Lukobe, nje kidogo ya mji wa Morogoro.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment