Image
Image

Maandalizi uchaguzi mkuu yakamilika kwa asilimia 50.

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema taratibu za maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu zimekamilika kwa zaidi ya asilimia 50.
Akizungumza Dar es Salaam jana na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema licha ya kukamilikia kwa kiasi hicho bado kuna changamoto ndogo ndogo.
“Changamoto ni ndogo ndogo na si kama tulivyotegemea kutokana na kuwepo kwa ushindani mkubwa kwenye vyama vinavyoshiriki uchaguzi mwaka huu,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema baadhi ya changamoto ambayo NEC ilikuwa ikipata ni pamoja na uwepo wa rufani nyingi za pingamizi kutoka kwa wagombea mbalimbali hususan wa udiwani na ubunge.
Alisema tume ilipokea pingamizi 56 na kati ya hizo, 55 zimesikilizwa na kutatuliwa na pingamizi moja iliachwa kutokana na kufikishwa bila kufuata vigezo.
Pamoja na changamoto zilizopo alisema hadi kufikia sasa wanaendelea kukamilisha hatua mbalimbali ikiwemo ya kuainisha mikoa, jimbo, wilaya, kata na vituo pamoja na kupeleka majina yote ya wagombea wa nafasi ya udiwani na ubunge ili kuandaa karatasi za kupigia kura.
Vifaa
Alisema uandaaji wa karatasi za kupigia kura za wagombea wa urais zipo katika hatua ya mwisho kukamilika na kwamba wapigakura wataziona. Kailima alisema tayari wamepokea vifaa bilioni 72 na kwamba vitaanza kuwasilishwa kwenye vituo husika.
“Maandalizi yanaendelea vizuri tu na tayari tunaanza kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa ngazi ya jimbo, kata na waratibu wa uchaguzi ngazi ya mkoa,” alisema.
Kamati
Mkurugenzi huyo alisema kutokana na migongano, uvunjifu wa sheria na maadili hadi kufikia sasa kamati tatu zipo ili kushughulikia uvunjifu wa maadili ngazi ya Taifa, na kwamba zitakuwa na mjumbe mmoja mmoja kutoka kila chama kilichosimamisha mgombea urais.
Kamati nyingine ni ya jimbo, na wajumbe wake watafanya uamuzi ambapo watakuwa mmoja mmoja kutoka kila chama kilichosimamisha mgombea ubunge na katika ngazi ya kata mjumbe atatoka kwa kila chama kitakachosimamisha mgombea udiwani.
Alifafanua kuwa kamati hizo zitafanya uamuzi pale chama, mgombea, tume au serikali itakapopeleka taarifa ya kutofuatwa kwa maadili.
“Hadi kufikia sasa tume tayari imepokea kesi mbili, lakini sitazitja kwani wahusika wenyewe walisema wasitajwe na tayari zimeamuliwa,” alisema.
Uhakiki
Kwa upande wa uhakiki wa daftari la awali la mpigakura, alisema hadi sasa takriban nusu ya wapiga kura wamehakiki taarifa zao. Alisema utaratibu huo unaondoa tatizo la watu waliojiandikisha bila kuwa na sifa stahiki.
Kuhusu idadi ya Watanzania waliojiandikisha, alisema tume itaweka wazi baada ya kukamilika kwani hadi sasa wanaendelea kupokea taarifa za wapigakura kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Jimbo la Lushoto
Akizungumzia kuhusu mgombea ubunge wa Jimbo la Lushoto Mkoa wa Tanga kupitia Chadema aliyefariki dunia, Mohamed Mtoi, Mkurugenzi huyo alisema hakutakuwa na uchaguzi katika jimbo hilo hadi chama hicho kitakapomsimamisha mgombea mwingine.
“Taratibu za uchaguzi zimesimamishwa hadi chama hicho kitakaposimamisha mgombea mwingine kwani hadi sasa tumetoa muda wa siku 30 ili kiweze kukamilisha utaratibu na utatumika maeneo yote yaliyopoteza mgombea na uchaguzi wake utafanyika baada ya uchaguzi mkuu,” alisema.
Kutangaza matokeo
Katika hatua nyingine, NEC imesisitiza kuwa itatangaza matokeo ya mgombea atakayeshinda na kwamba hakuna atakayeibiwa kura.
Pia, imeitaka jamii kuondoa hofu ya uchaguzi mkuu ujao kwani utakuwa huru na haki kwa sababu kutakuwa na wakala kwa kila ngazi ya mgombea.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa hapa nchini, Makamu Mwenyekiti NEC, Hamid Hamid alisema tume ipo huru katika kutoa matokeo ya mgombea wa chama chochote atakayeshinda uchaguzi mkuu ujao bila kuyabadilisha.
Hamid alisema kutokana na hofu, vyama husika vimeweka mawakala katika kila ngazi ya mgombea kwa maana ya nafasi ya diwani, mbunge hadi rais na kwamba watashuhudia taratibu zote hadi kubandikwa kwa matokeo.
“Tume tupo tayari kutangaza mshindi wa aina yeyote na kwa sababu ukitangaza asiyeshinda mashine zote zitatuumbua kwa sababu fomu zikijazwa zitaonesha nafasi ya kila mgombea, ambapo nafasi ya rais itatumwa kwa njia ya kompyuta hadi makao makuu,” alisema.
Hamid alisema mara baada ya kubandika matokeo hayo taarifa sahihi itatolewa kwa kila kituo ikiwa na idadi ya mshindi huku wadau wakiwa wanajua na kisha kupelekwa tume.
Alisema hadi sasa mchakato wa uhakiki wa majina waliojiandikisha kupiga kura umemalizika na kwamba kila aliyejiandikisha ana wajibu wa kupiga kura ifikapo siku ya uchaguzi.
Kuhusu kampeni za kashfa kwa vyama vya siasa, Makamu Mwenyekiti huyo alisema sheria zipo vyama vya siasa vinatakiwa kushtaki kituo cha polisi pale wanapoona au kusikia kashfa dhidi yao huku akibainisha taratibu za kimaadili zipo zitafuatwa baina ya vyama hivyo.
Akijibu swali kuhusu vyombo vya habari vya serikali kutoa fursa sawa kwa wagombea kupitia vyama vyao, alisema ni wajibu wa serikali kutoa nafasi sawa huku akivitaka vyama vitakavyonyimwa nafasi hiyo kutoa taarifa katika tume hiyo.
Hamid alisema Katiba ya nchi haina dini, hivyo tume ina jukumu la kukemea pale ambapo vyama vitakuwa vinakiuka katiba kwa kuhubiri udini kwa jamii zao na si kusubiri hadi yatokee. Hivyo aliwataka wananchi kujitokeza kupiga kura ifikapo Oktoba 25, mwaka huu kwa kuzingatia amani iliyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema mkutano huo wa viongozi wa dini una nafasi kubwa katika kusaidia uchaguzi uwe huru na amani kwani umekutanisha makundi yote ya watu ambao jamii inawasikiliza.
Alisema viongozi wa dini wana nafasi ya kutunza amani kabla na baada ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuliombea taifa au kuhamasisha taifa huku viongozi wa kisiasa wakiwa na jukumu la kujenga taifa.
“Ufafanuzi umetolewa kwa viongozi wa dini na kisiasa katika kuwaelezea wafuasi wao au kuwafafanulia na wao wenyewe kuacha maneno ya kuropokaropoka maneno ya aina hiyo itasaidia kuona mioyo ya wafuasi wao kuwa haki inatendeka,” alisema.
Alisema jamii isiwe na dhana ya kuhisi Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kutoa nafasi ya upendeleo kwa mgombea urais, hivyo katiba na miiko hairuhusu mwanya wa kuingiliwa kwa tume ya uchaguzi kwani zinajitegemea.
Naibu Waziri huyo aliwataka watu kujikita katika kunadi sera na kushawishi wapigakura na si kufanya njama za kuharibu amani ya nchi ikiwa ni pamoja na kujitokeza kwa wingi kupiga kura na wasihofie kuibiwa kura kwani mawakala wanatosha.
Makamu Mwenyekiti Chama cha NCCR-Mageuzi Zanzibar, Ambar Hamis alisema Serikali imejipanga kutoa elimu kwa jamii kupitia vyama vyao na viongozi wa dini ili kuimarisha amani nchini.
Alisema kutokana na mkutano huo anaamini kuwa hautazaa matunda kwani ni sawa na mkutano uliofanyika katika Bunge la Katiba kwa kuwa wadau wakuu hawapo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment