Image
Image

Magufuli asema anataka Tanzania yenye viwanda asisitiza hatakubali kuwepo kwa urasimu kwa watu wanaotaka kuwekeza.

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameendelea kueleza msimamo wake wa kutaka Tanzania yenye viwanda kwa kusisitiza kuwa hatakubali kuwepo kwa urasimu kwa watu wanaotaka kuwekeza nchini.
Amekemea pia utaratibu wa baadhi ya watumishi serikalini kuwazungusha watu wanaotaka kuwekeza kwa kauli za ‘njoo kesho’ akisema, katika uongozi wake, hataruhusu vitendo hivyo.
Akihutubia umati wa wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Samora, mjini Iringa, Magufuli alisema atakapoingia madarakani, atataka kuona kiwanda cha usagishaji cha NMC cha mjini Iringa kinafanya kazi mara moja.
“Nataka serikali ya wachapakazi,” alisema na kumuita mwekezaji mzalendo wa kiwanda cha ASAS, Salim Abri, huku akisisitiza kwamba, nchi inahitaji wawekezaji wanaotengeneza ajira kama huyo.
Akizungumzia mafanikio ya serikali yake, Magufuli alimsuta Mchungaji Peter Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema aliyemaliza muda wake) kutokubali kusema ukweli juu ya mafanikio yaliyopo Iringa.
“Lakini leo mchungaji, tena mchungaji wa bwana, mchungaji wa kondoo anasema hakuna chochote,” alisema Magufuli na kutaja maeneo kadhaa yanayodhihirisha maendeleo ya nchi ikiwamo, huduma za mawasiliano, barabara na ujenzi wa nyumba bora.
Alihoji wanaodai hakuna chochote kilichofanyika, wanashindwa kuona hata suala la amani kuwa pia ni sehemu mafanikio? “Shukurani ya punda ni mateke,” alisema. Magufuli aliendelea kusisitiza msimamo wake juu ya uwajibikaji na kusema, kwenye kazi hatokuwa na blabla.
Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi, mgombea huyo wa urais alisema, lengo ni kuhakikisha kila anayefanya kazi vizuri, anafaidi badala ya kuwapo tofauti kubwa ya mishahara. Alisema ndiyo maana imeundwa tume ya kupitia mishahara ili wafanyakazi wanaofanya vizuri wanufaike na siyo kuhangaika na mwisho wa siku, kuichukia serikali yao.
Alisema utaratibu wa watu wachache wanaopata fedha za rushwa na kudhulumu watu wa chini, kuharibu eneo moja na kuhamishiwa lingine, hataukubali katika serikali yake kama ataingia madarakani.
Mgombea urais huyo alisisitiza kwamba anataka kuleta mabadiliko ikiwa ni pamoja na kutekeleza ilani ya chama inayotaka zitengenezwe ajira asilimia 40. Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, akihutubia mkutano huo, alisema Watanzania hawataki Rais wa majaribio Nape ambaye alisema CCM siyo chama kinachoongozwa na malaika, alikiri kuwa kina upungufu wake lakini pia kina mambo mengi mazuri.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment