Image
Image

Chondechonde Agizo la Sefue lisiishie kwa madaktari Pekee.

JANA katika mtandao huu tuliandika agizo la Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue la kuwataka madaktari wote nchini,kuhakikisha wanatumia muda wao kazini na si kufanya mambo yao binafsi.
Agizo hilo ambalo alilitoa wakati anatembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kuwasilisha maagizo ya Rais John Magufuli, ni moja ya maagizo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa kutokana na unyeti wake.
Tumekuwa tukiandika malalamiko ya wananchi kuhusu matatizo yanayosababishwa na madaktari wetu hasa pale wanapoamua kwa makusudi kutumia vibaya muda wao. Matumizi haya mabaya ya muda huo, kumesababisha watu kuichukia Serikali kutokana na kushindwa kupata huduma katika hospitali zake.
Imekuwa haingii akilini kuona kwamba watu waliosomeshwa kwa kodi za umma wa Tanzania kwa makusudi kuitumia vibaya kauli ya Serikali ya kuwaruhusu kuwa na shughuli binafsi.
Kutokana na hali hiyo, tunapenda kumuunga mkono Katibu Mkuu kwa maagizo yake kwa madaktari hao huku tukiwaomba wawaonee huruma Watanzania ambao hawana fedha za kwenda katika kliniki zao.
Ni vyema katika kurejesha imani na matumaini ya wananchi wa Tanzania, madaktari, wauguzi, wafamasia, watu wa maabara na watumishi wote wa umma nchini kuwajibika kwa wananchi kwa kuwatumikia.
Kuwajibika kwa namna hii si kuburuzana, kwani ni ukweli kuwa upo mkataba wa wao na mwajiri wao wa kuwatumikia wananchi katika saa zilizokubalika. Ndio kusema madaktari wasiowajibika na kutumia muda wao wa kazi serikalini kuhudumia wagonjwa wao binafsi hawatufai na wanastahili kupewa adhabu ili watu waone matunda ya kodi zao.
Tunaamini wafanyakazi wote wa Afya wameona umuhimu wa agizo hilo hasa kwa kuzingatia umuhimu wa afya za wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuendeleza gurudumu la maendeleo la taifa hili.
Kwa kasi tuliyo nayo ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati, ni vyema watumishi wote wakashiriki kikamilifu katika kuendeleza majukumu waliyokubali kuyabeba kwa uadilifu na umahiri mkubwa ili kila mmoja aweze kutoa mchango wa dhati kwa maendeleo ya taifa.
Na katika hili tunamuomba Katibu Mkuu Kiongozi asichoke kufuatilia uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma ili wananchi waone matunda ya ulipaji kodi wao na huduma wanazostahili kuzipata kutoka serikalini. Hata hivyo, hili lisiwe la hospitali za Serikali pekee bali kila mahali ambapo Serikali ina mkono wake katika kuhudumia wananchi wake katika sekta ya afya na nyinginezo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment