Image
Image

Janja Janja Bomoabomoa yabainika.

Wakati fukuto la bomoabomoa likiendelea katika maeneo mbalimbali nchini, imedaiwa kuwa mamia ya watu wanaooneka kwenye maeneo ambayo nyumba zimebomolewa, si waaathirika bali hukaa humo mchana tu.
Uchunguzi uliofanywa na Tambarare Halisi katika eneo la Mkwajuni, jijini Dar es  Salaam, umebaini kuwa matapeli hao wamefikia hatua ya kujenga vibanda kwenye vifusi ambavyo serikali ilibomoa nyumba za wahusika.
Licha ya kuwapo kwa matapeli hao, gazeti hili lilibaini pia kwamba watu wachache waliobomolewa nyumba zao katika eneo hilo, bado wanaishi hapo kutokana na kile walidai ni kukosa sehemu ya kwenda.
Wizara ya Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), lilibomoa zaidi ya nyumba 600 za wakazi wa eneo la Mkwajuni waliokuwa wamezijenga pembezoni mwa Mto Msimbazi. Juzi pia serikali ilivunja  vibanda 186 vilivyokuwa vimejengwa juu ya vifusi hivyo.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo,waliiambia Tambarare Halisi kwamba baadhi ya watu waliondoka eneo hilo hata baada ya bomoabomoa, lakini baada ya kusikia kuna uwezekano wa kupewa fidia, wakaamua kurudi.
 “Si kwamba hawa si wakazi. Walikuwa hapa na nyumba zao tunazifahamu, sema wenzetu kidogo wamefanikiwa kuhama lakini baada ya kusikia kuna kuorodheshwa majina,wamerudi ili wapate chochote kitu endapo serikali itatoa msaada,” alisema Fatma Abasi.
Alisema walio na mahitaji ya kweli hawakuondoka eneo hilo tangu Desemba 17 walipoanza kubomolewa.
Fatma ambaye awali alijenga kibanda  kilichoezekwa na mabati na mbao lakini kikabomolewa wiki iliyopita, kwa sasa amejiegesha kado ya bonde hilo akisubiri kupata msaada wa aina yoyote kutoka serikalini.
“Nina watoto wawili na mume, maisha tunayoishi ni ya kulala hapa unapopaona (mwonekano wa nzi na majitaka yaliyotuama) hakuna masaada wowote na sina pa kwenda na familia yangu ndiyo maana hadi leo nimekaa hapa,” alisema Fatma.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Mgasa Wambura, alikiri kuwapo kwa watu wasio waathirika akisema miongoni mwao ni waliofunga barabara ya Kawawa juzi kwa kuchoma matairi.
TATHIMINI YAFANYIKA
Jana alfajiri, NEMC na wizara husika, walifanya tathimini kwenye eneo hilo na kubaini kwamba ni watu saba pekee wanaolala katika eneo hilo tofauti na hali inayoonekana nyakati za mchana.
Watu hao saba waliokutwa eneo hilo, walikuwa wamepanga matofali na mabati na kujiifadhi ndani yake.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventure Baya, aliieleza kwamba walifanya tathimini hiyo alfajiri ili kutambua waathirika halali wa eneo hilo.
Naye Mwanasheria Mkuu wa NEMC, Heche Suguta, alisisitiza kuwa wakazi hao wanapaswa kuondoka eneo hilo kwa sababu wameshaelezwa kuwa ni eneo hatari.
“Tunachotaka ni kuwasaidia lakini badala ya kuondoka wanaendeleza matukio katika eneo hilo ili waonekane wanaonewa,” alisema Suguta.
POLISI WAKESHA KULINDA USALAMA
Wakati juzi kukiwa kumetokea tukio la wananchi wa eneo hilo kuchoma matairi barabarani na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara ya Kawawa, Jeshi la Polisi lililazimika kukesha eneo hilo hadi asubuhi ili kulinda usalama.
Wakazi wa eneo hilo, walilieleza gazeti hili kuwa Polisi waliokuwa kwenye magari mawili aina ya Land Rover Defender walikesha eneo hilo.
“Tulishangaa hadi asubuhi hapa kulikuwa na askari pamoja na magari yao wakilinda usalama wa hapa,” alisema Tabu Nasoro ambaye kwa sasa amejiegesha kwenye kibanda kilichoezekwa kwa vitofali na mabati chakavu.
Alibainisha kuwa askari pia walikuwa wakizunguka eneo hilo mara kwa mara ili kudhibiti uhalifu wa aina yoyote kutokea.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment